BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

BUNGE LAENDELEA KUKOMAA NA IPTL MJINI DODOMA

http://freemedia.co.tz/daima/wp-content/uploads/2014/02/bunge5.jpg
BUNGE limesema ratiba ya Mkutano wake wa 16 na 17 itaendelea kama ilivyo na kwamba hakuna barua yoyote kutoka katika Mahakama inayolizuia kujadili ripoti kuhusu sakata la fedha za Tegeta Escrow.

Juzi, kuliibuka mabishano makali bungeni huku wabunge wakionesha hisia kuwa ipo barua kutoka kwa mhimili mwingine wa Dola, Mahakama ikilizuia Bunge kujadili sakata hilo lililoibua mjadala miongoni mwa jamii.

Wabunge hao walidai kuwa Mahakama haina uwezo wa kuwazuia kujadili suala hilo, na kwamba wanataka ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iwasilishwe bungeni kama ilivyopangwa.

Lakini jana tena Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati ikitoa maoni yake kuhusu Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Uzuiaji wa Vitendo Haramu dhidi ya Miundombinu ya Kudumu iliyojengwa chini ya Bahari ya Mwaka 1988, iligusia tena sakata ya Tegeta Escrow.

Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), katika taarifa yao hiyo, alidai suala la uchotaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, Serikali imedhihirisha wazi kwamba ufisadi ni sehemu ya maisha ya baadhi ya mawaziri na watendaji wa serikali.

“Mbaya zaidi ni pale inapoonekana wazi mhimili wa Bunge unaingiliwa na mhimili mwingine unaotajwa kuliandikia Bunge barua ya kutojadili sakata la Escrow, jambo ambalo ni dharau kwa Bunge,” alidai Machali.

Baada ya kumaliza kusoma taarifa hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora, George Mkuchika, alisimama na kuomba Mwongozo wa Spika kuhusu suala hilo kuingizwa katika mjadala ambao haupo wakati huo.

Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu aliyekuwa akiongoza kikao cha jana asubuhi, alisema hakuna barua yoyote iliyoandikwa na Mahakama kwenda kwa Bunge.

“Hakuna barua ya Mahakama iliyoandikwa kulizuia Bunge kujadili suala la Escrow. Uhusiano wa Bunge na Mahakama ni mzuri na wa kuheshimiana. Ratiba ya Bunge itakwenda vile vile,” alisema Zungu.

Kwa kauli yake, ni kwamba Bunge sasa wiki ijayo litajadili ripoti hiyo ya CAG ambayo kwa sasa inachambuliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na itakuja na mapendekezo yake kwa Bunge kama ilivyoagizwa na Spika.

Wakati akizungumza baada ya ushauri wa wabunge juzi kuhusu suala hilo, Naibu Spika Job Ndugai alisema suala hilo litapelekwa kwa Kamati ya Uongozi, huku akiahidi kuwa Kiti cha Spika “kitatenda haki.”

Naibu Spika Ndugai alifanya rejeo la kauli ya aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta akisema “tukiwa viongozi hatuwezi kutengeneza umoja katika uozo.” Ndugai alisema kwa kutazama hali ya wabunge ilivyokuwa wakati wa kumshauri, aliahidi kuwa “tutatenda haki katika jambo hili.”

Kwa mujibu wa Zungu, Kamati ya Uongozi itakutana leo saa nne asubuhi, na bila ya shaka, suala la lini mjadala wa Escrow ufikishwe bungeni, litajadiliwa na kupitishwa.

Katika ratiba ya sasa, ripoti ya CAG kuhusu Tegeta Escrow imepangwa kujadiliwa Novemba 27, mwaka huu, siku moja kabla ya Bunge kuahirishwa.

Sakata la Tegeta Escrow linahusu uchotaji wa Dola za Marekani milioni 200, huku taarifa za awali zikidai kuwa CAG amebaini kuwa madai ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa IPTL ni Sh bilioni 321, wakati fedha zilizokuwa kwenye akaunti ni Sh bilioni 306.

Akaunti hiyo ilifunguliwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) baada ya kuwapo kwa mgogoro wa kibiashara kati ya Tanesco na IPTL, kampuni inayofua umeme yenye mitambo yake Tegeta, Dar es Salaam.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: