RAIS KIKWETE.
Hizi ni baadhi ya kauli zenye utata na ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikinishangaza na wakati mwingine zinaniacha na maswali mengi zaidi na ambayo hayana majibu.
Hakuna shaka, huu ni uwajibikaji wenye kasoro, ambao kwa kiasi kikubwa unanichochea nifungue midomo yangu na kuzizungumzia kasoro hizo kwa uchungu.
Nimekuwa nikifuatilia kwa mfano baadhi ya kauli tata ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya viongozi wetu, zinanichosha.
Ziara za Katibu mkuu wa chama tawala (CCM), Kanali Abdulrahman Kinana zimekuwa zikiendelea katika maeneo mengi ya nchi yetu zikiacha nyuma mifano hai inayochekesha.
Ninamheshimu Kinana, akiwa mtendaji mkuu wa CCM, ni mtu makini ambaye nimeambiwa na watu walio karibu na ofisi yake kuwa anajitolea zaidi, kwamba anaishi bila kutegemea chama chake kwa mshahara, ninampongeza kwa dhati!
Ninaamini, huo ni uzalendo halisi, tena wa kipekee kwa mtu au kiongozi kuishi bila kujichotea fedha kutoka kwenye ruzuku ya chama chake ambayo hata kama ni mamilioni kwa mwezi, lakini chama hiki kinao viongozi wengi ,mtandao mkubwa ulioenea kote nchini, wenye kutaka fedha nyingi ili kuishi.
Hata hivyo, katika ziara hizo ambazo Kanali Kinana amekuwa akifuatana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, nimeshangazwa wakati mwingine na baadhi ya kauli zenye malalamiko, ambazo hazina majibu.
Nitazungumzia chache, hasa zile ambazo zinahusu utendaji duni wa Serikali, ile ile ya chama tawala, CCM ambayo imekuwa ikikumbushwa wajibu wake na wanaofanya hivyo ni Kinana na Nape wakiwa kwenye ziara hizo, ninawashangaa.
Najiuliza, kwa mfano wanapoitaka ichukue hatua ili kumaliza matatizo kama ya mapigano baina ya wakulima na wafugaji kule Kiteto, mkoani Manyara au kwingineko nchini, wamejiuliza hiyo ni serikali ya chama gani?
Nilidhani, badala ya kutoa maelekezo katika ziara zile kwa Serikali, Kinana na Nape wangeitisha mikutano ya viongozi wa Serikali kwa ruhusa ya mkuu wa nchi, Rais Jakaya Kikwete waelezane wapi wamekosea, nini kifanyike ili kumaliza matatizo kama ya Kiteto.
Si mara ya kwanza kuzungumzia utendaji duni wa Serikali, kwani kauli ya mawaziri mizigo ilianzia kwenye ziara zao, lakini hakuna hatua thabiti zilizochukuliwa ili kuhakikisha mizigo hiyo inatoswa baharini, kama ni safari ya meli au jahazi ili kunusuru chombo katika hatari ya kuzama.
Kuna usemi wa ‘kufaulisha’, hapa sizungumzii kufanya vyema kwenye mitihani au masomo, bali ni kupunguza mzigo au abiria waliozidi kwenye mabasi, magari, majahazi.
Ninaamini, baadhi yetu, hasa madereva wengi wanalifahamu vyema neno hilo kwani siku hizi kununua au kumiliki gari siyo tena ajabu, kila mmoja anayeamini kuwa amefanikiwa kimaisha, hufikiria kununua na kumiliki gari.
Ninaona kuwa badala ya kulalama, Kinana na timu yake wamshauri vyema bosi wao, Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa chama, akirejea kutoka matibabu yake kule Marekani, afaulishe mzigo ili tupone.
Ninaamini, abiria au wasafiri kwenye jahazi letu wamezidi na hata kwenye gari la Kikwete, yaani CCM ambalo lipo kwenye barabara mpya, lakini zenye kujaa tope, zinazoteleza wakati wa masika, ambazo hujaa vumbi wakati wa kiangazi, lazima hatua zichukuliwe.
Naamini, Kinana na wenzake katika uongozi wa juu wa CCM kitaifa watafanya hivyo, wakitambua kuwa wale walioachwa nyuma kuwasaidia hawafai.
Sidhani kuwa hawajui, wanajua, lakini ni kawaida wanasiasa wetu kuchekesha, nimewasikia baadhi yao wakipoteza muda kwenye mambo yasiyokuwa na mashiko, ambayo hayawezi kuwaongezea shibe Watanzania.
Watanzania, waishio mijini au vijijini, wanaumizwa na ugumu wa maisha, hawana uhakika wa mlo ulio kamili kwa siku, wanaposikia kauli kama hizo zinazotolewa na viongozi wetu, wanawashangaa.
Bila shaka wanawashangaa viongozi wetu wasio na majibu kwa maswali na matatizo yao ya ardhi yenye mizozo mingi, uhaba wa maji kwa miaka mingi licha ya ahadi za kuyafikisha kwetu, si zaidi ya umbali wa mita 50, ahadi ambayo imeshindikana kwa zaidi ya miaka 50 sasa.
Wanao ukosefu wa barabara nzuri za kuaminika, hasa vijijini licha ya mzalendo John Magufuli kuzipigia debe kila mwaka wakati wa bajeti. Hakuna umeme, wengi wanaishi kizani.
Wanazo shule za msingi, sekondari, mijini na vijijini ambazo kwa jumla hazina hadhi ya kuitwa shule, hazina walimu bora, wale wa kutosha na kukidhi mahitaji.
Hazina maabara kwa masomo ya sayansi, mradi ambao siku hizi umegeuka wa ulazima, unaumiza walimu wanaokatwa mishahara yao, sikubaliani nao.
Nimezisemea shule za umma zisizokuwa na walimu, sitanii katika hili kwani zimebakia shule kwa majina, baadhi yake zimebebeshwa majina ya viongozi wakuu au watakatifu, lakini kwa bahati mbaya hazilingani, wala hazitunzi heshima ya wenye majina hayo.
Niliuliza wiki chache zilizopita, sababu za msingi za wakubwa wanaosimamia sekta ya elimu nchini kufuta mafunzo ya cheti cha ualimu, nilichokitaja kwa jina la Daraja la III A, sikuwa natania.
Siku chache baadaye nikamsikia Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama, mwakilishi wa wapigakura wa Peramiho kule Songea, Ruvuma, akisema kuwa mafunzo hayo yataondolewa na vyuo vitafungwa.
Nikashangaa, nilipoambiwa kuwa wamiliki wa taasisi hizo watafute kitu cha ziada cha kufanya kwenye majengo yaliyokuwa vyuo vya ualimu Daraja IIIA, nikaumia.
Ninaumia hadi leo hasa kwa nia hii ya kulazimisha walimu wasome, eti wakajisomeshe, watarejeshewa gharama zao mbele ya safari?
Ninajiuliza, ni nani atawalipa gharama hizo, hasa kama Serikali tayari inabeba mzigo mkubwa, mzito sana wa madeni ya wazabuni ambao wamehudumia vyuo vyake, lakini ambao imekuwa kazi kuwalipa?
Jiulize, zitatoka wapi fedha za kuwalipa walimu wote kwa maelfu ambao wataamua kujisomesha na kupata Stashahada au Shahada na ambao baadhi yao wameanza?
Ninasubiri jibu sahihi kutoka kwa Jenista Mhagama, kuhusu wale wanaotaka kusoma ualimu, kujiendeleza, atuambie bajeti ya wizara kwa mwaka 2014/15 ilitenga kiasi gani kwa kazi hiyo?
Nikiachana na swali hilo kwa Mhagama na anijibu mkubwa wake, Dk Shukuru Kawambwa, ambaye ningetaka miadi kwake akipenda kwa mahojiano maalumu, awaeleze Watanzania walio wengi, mijini na vijijini wanaoteseka, kuumia.
Mbali ya elimu, nizungumzie huduma za afya, kwenye hospitali zetu nyingi zillizo karibu, mmejionea siku hizi zote zimeharibika.
Nyingi kati ya hizo zimegeuka vichaka, hazifai hata kujikinga na manyunyu ya mvua, jua la mchana linalowaka na kuwaunguza vichwa.
Bado zinaitwa hospitali au zahanati na vituo vya afya kwa majina, wakubwa wetu wanaosimamia sekta hiyo wamezibadili majina, zinaitwa za rufaa za mikoa, inasikitisha.
Ninasema, zitakuwa vipi hospitali za rufaa, bila dawa, vifaa tiba, wala pia haziwezi kutoa huduma yoyote ile inayostahili, hazina wataalam?
Ni aibu kuona gani dawa hata za kutuliza maumivu, tunaambiwa tukanunue wenyewe, je, zinafaa nini kuendelea kuitwa hospitali ?. MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment