KIJANA WA MKOA WA RUKWA ABUNI NDEGE
NOVASTUS Nkoswe ni kijana mwenye umri wa miaka 28, mkazi wa Kijiji cha Mbuluma, Kata ya Msanzi wilayani Kalambo mkoani Rukwa.
Alipopata taarifa juu ya kongamano la uwekezaji la Ukanda wa Ziwa Tanganyika lililofanyika hivi karibuni mjini Sumbawanga, mkoani Rukwa, alipata shauku ya kushiriki. Kongamano hilo lililojumuisha mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma, lilifunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mohammed Gharib Bilal.
Lengo kuu la kongamano hilo ilikuwa kunadi fursa nyingi za uwekezaji ambazo hazijawekezwa ipasavyo mkoani Rukwa na katika ukanda huu wa Ziwa Tanganyika. Fursa hizo ziko katika Sekta za Viwanda, Madini, Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Afya, Elimu, Utamaduni, Michezo, Usafiri na Usafirishaji katika maeneo ya barabara, anga na majini katika Ziwa Rukwa na Tanganyika.
Nkoswe baada ya kuambiwa kwamba kwenye kongamano hilo watu binafsi na taasisi mbalimbali wanaonesha bidhaa mbalimbali zikiwemo za ubunifu, hakujali, akaona asibaki nyuma. Akaona hiyo ni fursa kwake kuonesha kipaji chake ambacho hata hivyo anasema, hakijapata uwezeshaji wa kuingia kwenye orodha ya vijana wabunifu wa vifaa vyenye manufaa kwa jamii zaidi ya kuwa fundi baiskeli maarufu kijijini kwake.
“Kuna ndugu yangu, alikuta naunda ‘ndege’ akanipa fomu akaniambia kuna maonesho ya wajasiriamali yanafanyika mjini Sumbawanga. Niliona hii ndiyo fursa na kwa bahati nikawa nimekamilisha ndege yangu, nikaanza safari ya kuja kuonesha kifaa changu hiki hapa kwenye maonesho,” anasema Nkoswe.
Akaamua kujitosa ndani ya uwanja wa Nelson Mandela Mjini Sumbawanga ambako kongamano hilo lilifanyika. Anasimulia kwamba, awali alikuwa ametengeneza pikipiki aina ya bajaj kwa kutumia mbao. Lakini baadaye akaona abadilishe muundo. Wakati anaambiwa taarifa juu ya maonesho kwenye kongamano hilo, alikuwa ametenganisha hiyo bajaj na kuanza kuunda chombo mithili ya ndege.
Kutokana na kazi yake ya ufundi baiskeli, alimudu kukusanya vyuma mbalimbali ambavyo baadhi yake, vilipatikana kutokana na shughuli yake ya ufundi baiskeli na vingine alivinunua. Alipata injini kutoka kwenye pikipiki chakavu aliyoinunua kwa mtu kijijini. Aliunda chombo hicho na kukiwekea mbawa, na vikata upepo mithili ya ndege ya kusafiria.
Kwa mujibu wake, alitumia takribani miezi miwili kuunda chombo hicho. Akakiwasha kikakubali, hatimaye akaanza safari ya kutoka kijijini kwake kwenda mjini Sumbawanga kushiriki maonesho hayo. Anasema aliweka lita nne za mafuta. Ilimchukua takribani saa 8 kutoka kijijini Mbuluma akiwa safarini.
“Niliendesha mwenyewe, njiani nilikuwa nikisimamishwa na watu mbalimbali waliokuwa wakishangaa kutokana na muundo wake,” anasema Nkoswe. Kijana huyu ambaye aliishia darasa la sita mwaka 2003 katika Shule ya Msingi Mbuluma, anasema alimudu kufika na kuingiza chombo hicho ndani ya uwanja wa maonesho. Kila aliyekikuta pembezoni mwa uwanja huo, hakuacha kushangaa.
Wakubwa kwa wadogo, walikusanyika kushangaa chombo hicho kilichotengenezwa na kufunikwa kwa karatasi za nailoni huku kikiwa na kiti kimoja cha dereva.
Anasema alianza kutengeneza chombo hicho Julai 11 mwaka huu na kumalizika ndani ya mwezi. Nkoswe ambaye anajuta kwa kutoendelea na masomo, akiwa uwanjani hapo, yeyote aliyetaka kushuhudia chombo hicho kinavyotembea, alipaswa kumpa fedha kidogo kuanzia Sh 500.
Baada ya kupokea fedha, aliingia na kuwasha chombo hicho kilichobatizwa ‘ndege ya ardhini’. Kilitembea mita kadhaa hali ambayo ilivuta watu mbalimbali wakiwemo watoto waliozunguka nacho kila kilipokwenda. “Hii hela ninayopata kutoka kwa baadhi ya watu wanaotaka kuona chombo kinavyotembea, ndiyo inanisaidia kumudu kukaa hapa mjini,” alisema Nkoswe.
Kwa mujibu wake, kufika kwake kwenye maonesho hayo, kulilenga kusaka wafadhili ambao wanaweza kuona umuhimu wa kumwendeleza. “Nina kipaji cha ufundi. Ni akili niliyozaliwa nayo. Lakini nimekuja kufikiri, kama ningeenda shule ningekuwa mbali,” anasema Nkoswe akitamani kupata wafadhili wa kumwendeleza.
Ingawa anatambua wazi kwamba chombo hicho hakiwezi kutumika kwa usafiri wa watu wengi, anaamini ubunifu na utaalamu wake wa kuunganisha vifaa kiasi cha kuwezesha kutembea barabarani, akipata wa kumwendeleza, anaweza kufanya mambo makubwa. Kijana huyu mwenye mke na watoto watatu, bado ana ndoto za kufanya mambo makubwa kupitia ufundi.
Anatamani kujiendeleza katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) lakini anasema kikwazo ni gharama za kujisomesha. Anasema shughuli yake kubwa ya kutengeneza baiskeli pamoja na kulima, vinamwezesha kutunza familia, ikiwemo kusomesha watoto wake wasije kuishia njiani kama ilivyokuwa kwake.
“Kama napata mtu wa kunisaidia, ningeomba nisaidiwe kupanuliwa mawazo katika ufundi hasa wa mitambo. Ningekuwa na uwezo wa kutosha, ningejiendeleza lakini sasa nikisema nikajisomeshe, hawa watoto wataishi maisha gani,” anasema. Nkoswe anatoa mwito kwa vijana hususani walioko shuleni, kukazania masomo wasije kukatisha ndoto zao za maisha. “Kwa kweli nashauri vijana, wenye nafasi ya kusoma, wasome hasa wasifanye kama mimi nilivyofanya,” anasema Nkoswe.
Katika kuelezea masikitiko ya kutoendelea na shule, anasema angekuwa na elimu ya kutosha, angeweza kubobea na kufahamika kitaifa kwa ubunifu wake. Lakini sasa, anasema anatumia akili za kawaida za kuzaliwa nazo zinazohitaji elimu ya masuala ya sayansi na teknolojia.
Anaamini kama angejiendeleza kitaaluma, angeweza kufanya maajabu kwa kutengeneza vitu ambavyo vingemletea umaarufu na kuleta manufaa kwa taifa. Ukiacha kwamba hana utaalamu, pia kutokusoma kumemnyima fursa ya kiuchumi kwani licha ya kuwa na mawazo ya kufanya mambo makuu, mtaji wake siyo mkubwa wa kufanikisha haya.
Mbali na utaalamu katika masuala ya umakenika kiasi cha kuwa maarufu kijijini kwa kutengeneza baiskeli, Nkoswe anasema kipaji kingine alicho nacho ni cha uchoraji. Anafichua siri ya kukatisha masomo ya shule ya msingi. Anasema mara nyingi, mwalimu yeyote alipoingia darasani, alikuwa na tabia ya kumchora.
Na mara nyingi, tabia hiyo iliwaudhi walimu akawa anaadhibiwa kwa viboko ambavyo ni miongoni mwa mambo yaliyomfanya akatae shule. “Sikujua kwamba shule ina umuhimu mkubwa sana katika maisha,” anasema Nkoswe. Ingawa ana ndoto za kufanya makuu akipata msaada, ana wasiwasi kutokana na kuishi kijijini ambako anaamini ni vigumu kufikiwa na mfadhili yeyote.
Hata hivyo anaomba msaada wa kuendelezwa na yeyote atakayeguswa kwa kuwasiliana naye kwa namba 0753834952.
0 comments:
Post a Comment