Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mufindi, Paulo Ntinika (mwenye bluu) alipokuwa akisikiliza tuhuma dhidi yake.
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Paulo Ntinika, amejikuta akilazimika kutoka katika kikao cha Baraza la Madiwani na kwenda kupumzishwa hospitalini, baada ya madiwani kumtuhumu moja kwa moja kwa matumizi mabaya ya zaidi ya Sh milioni 291.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Peter Tweve, fedha hizo ni za ujenzi, zilizoongezwa na watendaji wa halmashauri hiyo kinyume na maelekezo ya Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2005.
Katika kikao kilichofanyika mwishoni mwa wiki, baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo, wote wa CCM, walitoa kauli za kumkataa Mkurugenzi huyo, wakidai amepoteza sifa ya kuendelea kushika wadhifa huo.
Kabla ya kikao hicho hakijafikia uamuzi dhidi ya wahusika wote, waliotajwa kusababisha hasara ya fedha hizo, hali ya afya ya Ntinika, ilibadilika ghafla, ikabidi atolewe nje ya ukumbi na kukimbizwa katika hospitali ya wilaya hiyo kwa matibabu.
Baada ya kupewa ushauri na matibabu, Ntinika alipumzishwa kwa muda usiojulikana. Hatua hiyo ilifanya kikao hicho, kumteua Mweka Hazina wa halmashauri hiyo, Athumani Kihamiya, kukaimu nafasi ya Mkurugenzi.
Wakati hayo yote yakitokea, wanahabari waliohudhuria kikao hicho, walitolewa nje baada ya baraza hilo la kawaida kugeuzwa na kuwa Kamati Maalumu ya Baraza hilo, iliyojadili taarifa ya Kamati ya Ukaguzi ya Wilaya kwa siri.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Julai hadi Septemba 2014, baadhi ya barabara zinazohusishwa na malipo ya nyongeza, zilitajwa kuwa ni Kibengu hadi Kipanga yenye urefu wa kilometa 37, barabara ya Kipanga B hadi Uhafiwa na barabara ya Mkuta Ludilo hadi Ilasa ya kilometa 21.
Kwa mfano, taarifa hiyo ya ukaguzi inaonesha kuwa barabara ya Kibengu hadi Kipanga Januari 1, 2014 kikao cha zabuni kilikaa na kutoa kazi ya nyongeza yenye thamani ya Sh milioni 21.9 kwa ajili ya matengezo yake na kufanya thamani ya kazi yote kuwa Sh milioni 314.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa badala ya Sh milioni 21.9 kupitishwa na Bodi ya Zabuni, kazi hiyo iliongezwa tena Sh milioni 85.
“Tumeazimia wahusika wote waliofanya matumizi nje ya utaratibu, wachukuliwe hatua za kinidhamu. Wakati hayo yakiendelea tunaomba wananchi wawe na subira kuona ni taratibu zipi zitafuatwa,” alisema Tweve.
Alisema Kamati ya Fedha, ndiyo itakayofanya kazi ya kubainisha watumishi wanaohusika na tuhuma hiyo na taarifa yake ya kile kitakachopatikana, itatolewa Novemba 24, mwaka huu.
Alisema sula la Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuendelea au kutoendelea na nafasi yake hiyo, litaamriwa na mamlaka za juu ambazo tayari zimejulishwa kuhusu kile kinachoendelea wilayani humo.
Tweve alisema halmashauri hiyo itatoa taarifa kwa mamlaka zingine zinazohusika, ili wahusika watakaobainika kuhusika wachukuliwe hatua nyingine za kisheria.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment