BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

NILIKUWA NA SARATANI YA TEZI DUME: ANASEMA RAIS JAKAYA KIKWETE.


Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Inspekta Jenerali Ernest Mangu baada ya kuwasili katika uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam jana akitokea Marekani kwa matibabu. Wengine kutoka kulia ni Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Jenerali John Minja na Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), Jenerali Davis Mwamunyange (watatu kulia) na kushoto ni Mke wa Rais, Mama Salma. Picha na Rafael Lubava.


Dar es Salaam.
Rais Jakaya Kikwete amerejea nchini kutoka kwenye matibabu na kuwaeleza Watanzania kuwa alikuwa akiiumwa saratani ya tezi dume.

Rais Kikwete alisema binafsi hakutaka kufanya ugonjwa wake siri, lakini alishauriwa kutotangaza ugonjwa huo ili asiwatie wananchi hofu. Kwa sasa hali ya afya yake ni nzuri.


Kuhusu sakata la escrow, Rais Kikwete alisema hawezi kuyasemea kwa vile hana taarifa za kutosha kuhusu yanayoendelea Dodoma na kwamba pindi atakapopata yanayojiri huko ataweza kuyasema kama ataona kuwa kuna haja ya kuyasema.


Rais Kikwete ambaye hakuwepo nchini kwa takriban siku 20 akiwa kwenye matatibabu, alisema kuwa Septemba 27, 2013 alibainika kuwa na ugonjwa wa saratani ya tezi dume, lakini alikaa nayo kwa zaidi ya mwaka mmoja bila kufanyiwa upasuaji kutokana na shughuli nyingi za kikazi.


“Uchunguzi wa kipimo cha PSA (Prostate-Specific Antigen) ulibaini nina tatizo la tezi dume ambalo lilizidi kiwango kinachotakiwa mwilini. PSA yangu kwa zaidi ya miaka mitatu ilikuwa inapanda kwa kiwango kikubwa hali iliyoashiria kuwa kuna tatizo ambalo linahitaji matibabu,” alisema.


Alisema madaktari walimshauri kufanya upasuaji lakini alilazimika kuomba kufanyiwa Julai 2014, ili kupata muda wa kupokea Rasimu ya Katiba. Hata hivyo, kwa vile Bunge la Katiba halikuisha kama ilivyotarajiwa na kwamba hadi Julai Bunge lilikuwa halijamaliza kazi yake, aliomba kufanyiwa Novemba 2014.


Rais Kikwete alisema madaktari walimshauri kuwa asikose kufanyiwa mwezi huo kwa vile akichelewa sana saratani inaweza kusambaa hadi viungo vingine vya mwili.


Alisema kuwa kufanikiwa kufanyika kwa upasuaji kumempa nafuu sana na kumeshusha mizigo miwili aliyokuwa anayo. Alisema kuwa hofu ya kwanza aliyokuwa nayo ni baada ya kuambiwa kuwa ana saratani. Hivyo alikuwa ana hofu kwamba ugonjwa huo ungeweza kuenea sehemu nyingine mwilini.


Rais Kikwete alisema mzigo wa pili ni kutokana na jambo hilo kukaa nalo peke yake kwa muda mrefu. Alisema kuwa alimwambia mkewe baada ya miezi minane na kumtaka asimwambie mtu hadi atakaposema mwenyewe.


Hivyo kitendo cha kukaa na ugonjwa huo bila ya kumwambia mtu ulikuwa ni mzigo mkubwa na kwamba hata mkewe aliweza kutunza siri ya ugonjwa wake mpaka siku nne kabla ya kwenda kufanyiwa upasuaji.


Alisema kuwa aliliambia Baraza la Mawaziri kuhusu ugonjwa wake siku nne kabla ya kufanyiwa upasuaji.


Pia, Rais Kikwete alisema anamshukuru Mungu kwa kuwa madaktari katika Hospitali ya Johns Hospkings iliyoko Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani wamethibitisha kuwa yu mzima, ingawa atapaswa kupumzika kwa wiki nne kabla ya kuendelea na majukumu yake ya kawaida.


Akizungumza kwa utulivu, kiongozi huyo wa nchi, alisema haumwi maradhi ya busha kwa kuwa tezi dume na busha ni magonjwa tofauti na hayafanani.


Rais Kikwete alisema anasumbuliwa na saratani na kwamba ingawa hakuwa akipata maumivu makali, ugonjwa huo ulikuwa ukimletea mawazo mengi.


“Mimi ninajua ni saratani, lakini sijui unaendelea huko ndani. Nilikuwa nakwenda Shinyanga, Geita, Simiyu lakini ndani ya moyo wangu kuna jambo kubwa linanisokota,” alisema.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: