SAKATA LA UCHOTAJI WA FEDHA AKAUNTI YA TEGETA (ESCROW) WATIKISA BUNGE LA TANZANIA, WABUNGE WA CCM NA UPINZANIA WACHACHAMAA KWELI KWELI..
WABUNGE jana waliungana bila kujali vyama vyao, kutetea kuwasilishwa bungeni na kujadiliwa kwa ripoti ya sakata la uchotaji fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa Mahakama imezuia.
Katika kile kilichoonekana kuwa wabunge wanataka mbivu na mbichi za sakata hilo ziwekwe hadharani, walisema hatua yoyote ya kuzuia suala hilo lisijadiliwe, inaweza kulivuruga Taifa na wao kulaumiwa.
Hata hivyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitoa angalizo kuwa ni vyema kuwapo kwa utulivu na kila mhimili kusimamia mamlaka yake, na busara kutumika.
Bunge liliingia katika mjadala baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), kuomba ufafanuzi kutokana na kauli ya Waziri Mkuu wakati wa kipindi cha Maswali ya Papo kwa Hapo.
Akijibu swali la Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde (Chadema), Waziri Mkuu Pinda alisema yeye kama Mwanasheria ingawa si Mwanasheria Mkuu, kuna kesi zaidi ya 10 mahakamani kuhusu hilo, hivyo si vyema kuanza mjadala utakaotibua suala hilo.
Alisema hiyo si mara ya kwanza kwa Bunge kutoshughulika na suala linaloendelea mahakamani.
Kauli hiyo ndiyo iliyomsimamisha Kafulila na wabunge wengine wawili, Esther Bulaya (Viti Maalumu – CCM) na Moses Machali (Kasulu Mjini – NCCR- Mageuzi), huku Kafulila akitaka uhakika wa kauli ya Waziri Mkuu kama ripoti hiyo itapelekwa bungeni kujadiliwa au la.
Kutokana na hali hiyo, Naibu Spika alitoa fursa kwa wabunge kadhaa kulijadili suala hilo kwa nia ya kumsaidia kufikia maamuzi, lakini wote waliosimama ukiondoa Waziri Mkuu, walitaka ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iwasilishwe bungeni na ijadiliwe.
Kwa sasa, ripoti hiyo inafanyiwa uchambuzi kwa njia ya uchunguzi na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) chini ya Kabwe Zitto, kabla ya kuwasilishwa bungeni.
Wa kwanza kumshauri Naibu Spika alikuwa Kafulila aliyesema kuwa suala hilo ni mtihani kwa Bunge, na ili nchi isiingie katika machafuko, ripoti hiyo haina budi kuwasilishwa ndani ya Bunge.
“Bunge ndicho chombo chenye mamlaka ya mwisho katika nchi, watu watatupima kama tunatosha kuisimamia Serikali kwa jinsi tutakavyoshughulikia suala hili. Bunge lazima liheshimiwe, hatuwezi kuwalinda watu wachache. Hiki ni kipimo cha uhalali wetu,” alisema.
Bulaya alisema Bunge lazima liheshimiwe, na kwamba “CCM haiwezi kukubali kuchafuliwa na watu wachache, kila mtu ale kwa urefu wa kamba yake. Ujangili, dawa za kulevya, Escrow marufuku.”
Naye Mbunge wa Longido, Michael Laizer (CCM), licha ya kukiri kuwa miongoni mwa wasiolifahamu vyema suala hilo, lakini alisema ni busara likajadiliwa na Bunge.
“Mimi silielewi vizuri, lakini ni jambo kubwa linaloumiza vichwa. Kuna minong’ono mingi, kuna orodha inatajwa ya wezi, hawajulikani ni kina nani, wengine wamo humo ndani. Naibu Spika tusifiche wezi, kila kitu kiwekwe waziwazi, tuelewe, wengine wanapiga siasa. Ije ripoti haraka, waliokula tuwaseme, halitupi raha,” alisema Laizer.
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alisema ni vyema ripoti ikawasilishwa ili kujua mwizi ni nani na kila mtu abebe msalaba wake.
“Huu ndio wasaa wa ukweli, wasaa wa uamuzi. Hapa kuna watu waliitana tumbili na mwingine mwizi. Sasa ni wakati mwafaka kujua mwizi ni nani na tumbili ni nani,” alisema Msigwa.
Naye James Lembeli wa Jimbo la Kahama (CCM), alisema kama Operesheni Tokomeza ilikwenda na baadhi ya mawaziri, kuna kigugumizi gani katika Escrow.
“Kila mtu atahukumiwa kwa matendo yake, kama ni mtego basi uteguliwe. Historia itakukumbuka Naibu Spika kwa jinsi utakavyoshughulikia suala hili,” alisema.
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR- Mageuzi), alisema lazima kuwapo na uadilifu na uaminifu, hivyo waliohusika na sakata hilo waende na maji, nchi itulie.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), akizungumza kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, alisema Mahakama haiwezi kulifundisha kazi Bunge wala kulielekeza nini cha kufanya kwani haina mamlaka hayo.
“Kama Bunge la Tisa linakumbukwa kwa jinsi lilivyoshughulika na suala la Richmond, Bunge hili litakumbukwa kwa suala hili la Escrow. Ripoti iletwe hapa, wa kusuka na kunyoa tumjue,” alisema Lissu.
Akizungumzia maendeleo ya kazi yao, Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, alisema wako tayari kuiwasilisha ripoti yao bungeni.
“Sisi hata kesho (leo) tunaweza kuiwasilisha bungeni. Jana tumewahoji CAG, Takukuru na TRA na wamemaliza kazi yetu. Rasimu ya kwanza inaandaliwa leo (jana) na kesho inaweza kuingia bungeni, tukalijadili hili ili liishe,” alisema Zitto.
Hata hivyo, Waziri Mkuu Pinda alisema si kazi ya Mahakama kuficha uozo, lakini ni muhimu kila mhimili wa Dola ukatenda mambo kwa mujibu wa Katiba.
“Hata mimi nataka yajadiliwe yaishe, lakini tutumie busara kubwa ili kuondoa mwingiliano na chombo kingine cha maamuzi kama inavyotakiwa,” alisema.
Akihitimisha mjadala wake, Naibu Spika Ndugai alifanya rejeo la kauli ya aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta akisema; “tukiwa viongozi hatuwezi kutengeneza umoja katika uozo.” Ndugai alisema kwa kutazama hali ya wabunge ilivyokuwa jana wakati wa kumshauri, aliahidi kuwa “tutatenda haki katika jambo hili.”HABARILEO
0 comments:
Post a Comment