BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

TANZANIA YATIKISWA NA MATUKIO MATANO KATIKA SERIKALI YA RAIS KIKWETE TANGU ACHUKUE MADARAKA.


Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai (kulia) akiwakabidhi ripoti ya akaunti ya Escrow, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe (katika) na makamu wake Deo, Bungeni mjini Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herman


Dodoma.
Bunge jana lilikabidhi ripoti ya uchunguzi wa IPTL kwa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ili ipitie na kutoa mapendekezo bungeni, hatua ambayo inatazamiwa kusababisha mtikisiko wa tano katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.


Ripoti hiyo iliyoandaliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), katika vitabu vitano, ilikabidhiwa na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe huku akimpa masharti ya kuipitia kwa siri, kinyume na Zitto alivyokuwa ameahidi kuwahoji watuhumiwa katika kikao cha wazi.


Ripoti hiyo inatokana na uchunguzi maalumu wa fedha zilizochotwa katika akaunti ya escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), iliyokuwa inatunza fedha za gharama za uwekezaji (capacity charge) kwa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL baada ya kutokea mgogoro wa kibiashara baina yake na Tanesco.


Tanesco ililalamika kuwa ilikuwa inailipa zaidi IPTL kinyume na gharama za uwekezaji hivyo kuamuliwa na Mahakama kuwa fedha ilizokuwa inatakiwa kulipa ziwekwe katika escrow hadi upatikane ufumbuzi wa mgogoro huo.


Hata hivyo, kesi hiyo ilipohukumiwa Februari mwaka huu, ikibainisha kweli Tanesco ilikuwa inailipa zaidi IPTL, ilibainika kuwa fedha zilizokuwa katika akaunti hiyo Sh 306 milioni zilikwishachotwa na IPTL kwa ruksa ya baadhi ya viongozi wa Serikali.


Kutokana na hali hiyo, ripoti hiyo inaweza kuondoka na vigogo waliohusika na kashfa hiyo, kama ilivyowahi kutokea katika kashfa nyingine nne zilizoitikisa Serikali ya Awamu ya Nne ya inayoongozwa na Rais Kikwete



Richmond
Kashfa kubwa iliyotikisa nchi katika kipindi cha awali cha Rais Kikwete ilikuwa ni Richmond ya mwaka 2006. Hii ilitokana na tatizo kubwa la uhaba wa umeme na Serikali kulazimika kutafuta njia za dharura za kutatua tatizo hilo, zikiwamo zilizodaiwa kukiuka taratibu na sheria.


Baada ya kashfa hiyo kuchunguzwa na taarifa kutolewa bungeni, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa alilazimika kujiuzulu baada ya kutakiwa ajipime kutokana na mazingira ya kashfa hiyo.


Wengine waliong’oka madarakani ni mawaziri wa Nishati na Madini kwa vipindi tofauti, Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha.


EPA
Mwaka 2008 iliibuka kashfa nyingine ya wizi wa mabilioni katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (Epa) katika BoT na vigogo kadhaa walitumia mbinu chafu kuchota zaidi ya Sh133 bilioni katika akaunti hiyo.


Katika wizi huo ulioitikisa nchi, wahusika walitajwa kutumia vivuli vya siasa kupitisha nyaraka bila kufanyiwa uhakiki. Ilimalizika kwa baadhi yao kufikishwa mahakamani na wengine ambao hawakutajwa kusamehewa na Rais Kikwete wakidaiwa kurejesha fedha walizoiba.


Katika kipindi hicho, yalipofanyika mabadiliko ndani ya Baraza la Mawaziri aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakia Maghji hakurudi huku Gavana wa BoT, Daudi Balali akitimuliwa.



Ripoti ya CAG 2012
Mei 2012 ilipotolewa Ripoti ya CAG na kujadiliwa bungeni, ulitokea mtikisiko mkubwa uliowang’oa mawaziri sita na manaibu wawili.


Waliong’olewa ni Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Omary Nundu (Uchukuzi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Mustafa Mkulo (Fedha) na William Ngeleja (Nishati na Madini) na manaibu waziri wawili; Athumani Mfutakamba (Uchukuzi) na Dk Lucy Nkya (Afya).


Operesheni Tokomeza Ujangili
Mwishoni mwaka jana, matokeo ya Operesheni Tokomeza Ujangili (Otu), iliyoanzishwa na Serikali nayo ilizua mtikisiko mwingine uliowang’oa madarakani mawaziri wanne ambao wizara zao zilielezwa kushindwa kusimamia vizuri utekelezaji wa operesheni hiyo.


Mawaziri waliong’olewa ni Khamisi Kagasheki wa Maliasili na Utalii, Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.


PAC yapewa rungu
Katika makabidhiano ya ripoti yaliyoshuhudiwa na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi na wajumbe wengine watatu wa PAC, Ndugai alisema; “Naielekeza kamati yako ifanye uchambuzi na kutoa maoni na mapendekezo katika kila hadidu rejea.


“Katika kufanya uchambuzi kamati ijikite zaidi katika kufanya uchambuzi wa CAG na Takukuru.”


Ndugai alisema katika uchunguzi wake, CAG aliwahoji wote waliohusika na jambo hilo na kisha kuwasilisha taarifa yake kwa Takukuru kwa hatua zaidi.


“Kamati ifanye kazi kwa kuzingatia kanuni ya tatu na nne kwa kuzingatia nyongeza ya saba ya kanuni za Kudumu za Bunge za mwaka 2014 na kifungu cha tisa kifungu kidogo cha kwanza na cha 31 vya Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge, Sura ya 299,” alisema.


Alisema ni matumaini yake kwamba baada ya kumaliza kazi ya kutoa maoni na mapendekezo, taarifa iwasilishwe kwake (Ndugai) ili ajiridhishe kabla ya kuwasilisha bungeni.


“Nimemwelekeza Katibu wa Bunge, asimamie na awape ushirikiano unaotakiwa ili kazi yenu iweze kuwa ya ufanisi na yenye kiwango,” alisema.


Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah aliikabidhi PAC watendaji wanne ambao wataisaidia kufanya kazi hiyo.


Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Zitto alisema kamati yake itazingatia maagizo ya Ndugai kutokana na masuala ya kimahakama yaliyomo ndani ya ripoti hiyo.


“Kwa hiyo PAC haitakuwa na utaratibu wa kawaida ambao tunafanya tunapowaita watu wakati wa kuhoji mahesabu yao. Nimeshtuka kidogo maana Bunge limeipa nguvu sana PAC katika jambo hili kwa kuwaelekeza kutumia sheria namba tatu. Sisi tutaitumia nguvu hiyo kutenda haki katika jambo hili zima, haki kwa Watanzania na watu ambao wametajwa kuhusika katika jambo zima.”


Zitto alisema ripoti hiyo inaonyesha jinsi taasisi za kiuwajibikaji zinavyofanya kazi, mambo ambayo huwezi kuyaona katika nchi nyingine.


“Bunge liliagiza kupitia kamati yake ya PAC tangu Machi, 20 2014, baada ya kuona taarifa hiyo katika Gazeti la The Citizen, tukachukua hatua na kuagiza ukaguzi ufanyike. Baadaye jambo hili likaibuka bungeni, Waziri Mkuu (Mizengo Pinda) alipojibu hoja ya mheshimiwa (David) Kafulila, akaagiza tusubiri uchunguzi ambao PAC umeagiza.”


Alisema jambo hilo linajenga imani kubwa kuwa nchi inaendeshwa kwa taratibu na imeondoa hofu ya baadhi ya watu kuwa taarifa hiyo haitafika katika kamati kujadiliwa.


Alisema kwa msingi huo, Bunge linajaribu kukwepa mbinu zinazoweza kutumiwa na watu kuzuia kupelekwa mahakamani.


Akizungumzia wafadhili ambao wamejitoa kusaidia nchi, Zitto alisema; “Uhusiano kati yao na Serikali ni wao, sisi PAC hatuwezi kuwasemea. Bunge linasimamia uwajibikaji lakini kwa vyovyote vile kama wasiwasi wao ulikuwa ni taarifa ya PCCB na CAG kutofanyiwa kazi mmeona dhahiri hapa kwamba tumeifanyia kazi.”


Alipoulizwa iwapo siku 10 zinatosha kukamilisha kazi, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe alisema ni nyingi kwa sababu kamati hiyo ni makini na ina wataalamu waliobobea.


The Citizen lasifiwa
“Nataka nikiri bayana hata sisi PAC tulikuwa hatujui kama fedha hizi zimechotwa, it was just one paper, The Citizen (ilikuwa ni gazeti moja) waliandika investigative story (habari ya uchunguzi), mwenyekiti wangu (Zitto) aliiona akaileta kwenye kamati tukamuita Gavana akathibitisha ni kweli fedha zimechotwa,” alisema Filikunjombe.


Alisema kamati ilichukua hatua na kutaka waandishi wa habari kujivunia kazi yao nzuri waliyoifanya kwa kuwa ni mafanikio yao.



IPTL waibuka
Baada ya kukabidhiwa kwa ripoti hiyo jana katika Viwanja vya Bunge, alionekana Meneja Uhusiano wa IPTL, Sylvester Joseph ambaye alisema amefika hapo kufuatilia kama ripoti hiyo imewasilishwa na akasema kampuni hiyo itatoa ushirikiano kwa Bunge itakapohitajika kufanya hivyo.


Membe na wafadhili
Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema leo anatarajia kukutana na wahisani waliogoma kutoa misaada inayofikia Dola 560 milioni za Marekani kwa Serikali kutokana na kashfa ya IPTL.


Membe aliyasema hayo Dar es Salaam jana baada ya kufungua mkutano wa kwanza wa kimataifa wa Sauti ya Sayansi ya Jamii, unaokutanisha wasomi kutoka Afrika, akisema wahisani hao walitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya kashfa hiyo ya IPTL ambayo tayari imechukuliwa.


“Waligoma kutoa misaada hiyo hadi waone Ripoti ya CAG, sasa tayari imetoka, hivyo nitakutana nao kesho (leo) ili niweze kujua wanasemaje, bado wataizuia au watatoa?”


Alisisitiza kuwa uamuzi huo wa wahisani umeathiri kwa namna fulani utekelezaji wa Bajeti ya Serikali, hivyo hatua kali zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo.


“Hatuwezi kuacha kuchukua hatua tukikuta madudu humo kwenye Ripoti ya CAG kwa sababu imetugharimu, hatuko tayari kuzikosa fedha hizo za wahisani,” alisema.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: