VIBAKA WAMSHURUTISHA ASKARI WA JKT KISHA KUMUUA KWA DHANA ZA JADI JIJINI DAR ES SALAAM.
WATU watano wanasadikiwa kuwa wamekufa baada ya kuibuka kwa vurugu zinazohusishwa na vibaka katika eneo la Mbagala Kongowe Mzinga katika Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam. Polisi wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo, ingawa hawakutoa taarifa kamili kwa kuhofia kuharibu uchunguzi na kuahidi kuwa watatoa taarifa kamili ya vurugu hizo leo.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Sebastian Zakaria, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini alibainisha kuwa hawezi kutoa taarifa kamili kwa kuwa bado wanaendelea na uchunguzi.
“Siwezi kukupatia taarifa kwanza bado hatujaiandaa lakini pia ni mapema mno…hatutaki kuharibu uchunguzi, lakini kuna watu tumepata majina yao tunawatafuta, kesho (leo) tutawapatia taarifa kamili ya tukio hili,” alisisitiza Kamanda Zakaria.
Alikiri kuwa katika eneo hilo la Mbagala Kongowe Mzinga, kumetokea vurugu hizo na matukio mawili ya mauaji na kwamba bado uchunguzi unaendelea kuhusu tukio hilo.
Hata hivyo, chanzo chetu cha habari kilieleza kuwa, vurugu hizo ziliibuka tangu usiku wa kuamkia jana, ambapo inadaiwa raia mwema aliyefahamika kwa jina la Mwarami aliuawa kwa kupigwa mapanga na kuchomwa kisu eneo la moyo na watu wanaosadikiwa kuwa vibaka.
Mwarami pia anadaiwa kuwa alikuwa ni askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), aliuawa na vibaka hao kutokana na tabia yake ya kupambana na uhalifu katika eneo hilo, ambapo mtu yeyote anapoibiwa, yeye huchukua jukumu la kuwasaka vibaka hao na kurejesha mali kwa mhusika.
Chanzo hicho kilibainisha kuwa, kutokana na tabia hiyo iliyomjengea umaarufu Mwarami katika eneo hilo la Mzinga, vijana wanaojihusisha na ukabaji na kupora walichoshwa na usamaria wake na hivyo juzi waliamua kumshambulia.
Inadaiwa kuwa siku ya tukio, Mwarami kama kawaida alimsaidia mtu aliyevamiwa na kuibiwa na vibaka hao na kumrejeshea mali zake, ndipo vijana hao walimvamia akiwa kijiweni na kumshambulia kwa mapanga na kumchoma kisu, kisha kukimbia.
Baada ya shambulio hilo, Mwarami alikimbizwa hospitali, lakini alikufa kabla ya kufika hospitali kwa matibabu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, vijana hao wanaokadiriwa kuwa ni wanane baada ya kumshambulia Mwarami walikokimbilia walishambuliwa na wananchi wenye hasira na wanne kati yao kuuawa na miili yao kwenda kutupwa eneo la Tuangoma ambako ilichukuliwa jana na askari wa jeshi hilo kulazimika kuingia mtaani kutawanya vijana wote kwenye vijiwe mbalimbali maeneo ya Kongowe.
Kutokana na mashambulizi hayo, jana eneo la Kongowe Mzinga hali ya usalama ilibadilika na kugeuka eneo la vurugu kiasi cha Polisi kuamua kutumia mabomu ya machozi na kupiga risasi hewani ili kutuliza ghasia hizo.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment