BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAFANYAKAZI WA KAMPUNI YA RELI (TRL) WACHONGEANA KWA WAZIRI DK MWAKYEMBA, WATAJANA NAMNA WANAVYOFANYA WIZI KUIIBIA KAMPUNI.

 
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe.

WAFANYAKAZI wa Kampuni ya Reli (TRL) wameamua ‘kufunguka’ baada ya kuanza kutaja mtandao wa wezi ndani ya kampuni hiyo, unaoshiriki kurudisha nyuma jitihada za Serikali za kufufua shirika hilo muhimu kwa uchumi wa nchi.


Jana Kamati ya Uchunguzi iliyoundwa na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, ilitakiwa kukabidhi ripoti yake baada ya kumaliza siku saba za uchunguzi, ili kutoa nafasi kwa waziri huyo kuchukua hatua, ikiwemo kuwajibishwa viongozi wa shirika hilo, wanaotuhumiwa kuhujumu maendeleo yake.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Malima Bundala alisema mbele ya wafanyakazi na Dk Mwakyembe, kwamba baada ya kuzungumza na wafanyakazi wengi, walitajiwa majina ya baadhi ya wafanyakazi na tuhuma zao, zikiwemo za wizi na uchunguzi zaidi ukabaini ni mtandao mkubwa kuliko walivyotarajia.

“Tumezungumza na wafanyakazi wengi tu, tumepewa taarifa na tuliozungumza nao unaambiwa fulani na fulani ni wezi wa mafuta, lakini ukifuatilia unakuta kuna watu wengine wanahusika hawako peke yao, hivyo inabidi utafute namna ya kugundua na hao wengine,” alisema Bundala.

Muda zaidi
Kutokana na hali hiyo, Bundala aliomba kuongezewa muda, ambapo kamati yake ilipewa siku 21 nyingine, kuhakikisha inakamilisha uchunguzi wake.

“Tumeona badala ya kutibu maumivu kwa kumeza panadol, halafu pakipoa tusahau, sasa tutibu ugonjwa na siyo maumivu. Pia kuna hoja ambazo zinazidi kuibuka, hivyo tunaomba mtuvumilie ili tuwasikilize wote wenye hoja, wanaotuhumiwa na wengine,” alisema Bundala.

Baada ya kusikiliza ombi la Bundala, Dk Mwakyembe aliridhia ombi hilo na kuwaongezea siku 21 na kuwataka wafanyakazi wavute subira ili kamati hiyo imalize kazi yake.

“Kamati imeomba kuongezewa muda kwa sababu bado kuna mazito zaidi, kwa sasa hatuwezi kumhukumu mtu moja kwa moja tusubiri kamati imalize uchunguzi wake ndiyo tutajua namna ya kufanya,” alisema Dk Mwakyembe.

Alifafanua kuwa Serikali inataka kuhakikisha kampuni hiyo inarudi katika nafasi yake ya kujenga uchumi wa Taifa.

Aliwataka wafanyakazi hao wasiwe waoga wa kutoa taarifa na pia wawe tayari kusema ukweli, kwani kufanya hivyo kutasaidia kubaini wale wanaokwamisha kampuni hiyo.

Alisema kampuni hiyo tangu ibinafsishwe mwaka 2007, imekuwa ikizidi kushuka mwaka hadi mwaka, hali iliyosababisha kuwa na hali mbaya na tegemezi.

Vitisho
Aidha, Dk Mwakyembe alisema amepata taarifa ya kiongozi mmoja wa TRL, ambaye anadaiwa kumfuata mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo na kumwambia kuwa ana kiherehere, atashughulikiwa.

Alionya kuwa kufanya hivyo ni utovu wa nidhamu na mhusika huyo atachukuliwa hatua za kusimamishwa kazi moja kwa moja bila kusubiri uchunguzi.

Tuhuma
Kabla ya kuundwa kwa kamati hiyo, wafanyakazi wa shirika hilo walianza kujiandaa kwa mgomo, ambao kabla ya kufanyika, Dk Mwakyembe alikutana nao kusikiliza kero zao.

Katika mkutano huo, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli (TRAWU), Erasto Kihwele alitaja viongozi watano aliodai kuwa wamekuwa mizigo na kwamba ndiyo wanaowakwamisha katika utekelezaji wa majukumu.

Kihwele alitaja viongozi hao kuwa ni Mkurugenzi wa TRL, Amani Kisamfu, Kaimu Mkurugenzi, Pascal Mafikiri, Ofisa Rasilimali Watu, Pius Kaberehe, Ofisa Mawasiliano aliyetajwa kwa jina moja la Nduezabura na Mhandisi aliyetajwa kwa jina mmoja la Masai.

Kihwele alizungumzia pia suala la nyongeza ya mshahara na malimbikizo ya fedha kwa wafanyakazi hao na kumwomba Dk Mwakyembe kulipatia ufumbuzi haraka.

Baada ya kusikiliza wafanyakazi hao, Dk Mwakyembe alisema hawezi kuhukumu viongozi hao, kabla ya kuchunguza kwanza tuhuma hizo, hivyo aliunda kamati hiyo na kuipa wiki moja iliyoisha jana, kuja na majibu ya matatizo ya wafanyakazi hao, ikiwa ni pamoja kubainisha vyanzo vipya vya mapato na ili hatua zichukuliwe, ikiwemo kuwajibishwa kwa viongozi watakaotiwa hatiani.

ATCL
Ushuhuda wa Bundala wa kuwepo kwa makubwa kuliko walivyotarajia, unaiweka TRL katika orodha ya mashirika ya Wizara hiyo kufumuliwa na Dk Mwakyembe.

Mwanzoni mwa Juni 2012, Dk Mwakyembe alitengua uteuzi wa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Paul Chizi, ambapo alisema hatua hiyo ilitokana na tuhuma nyingi zilizokuwa zikikabili uongozi wake, ikiwemo kuingia kwa siri mkataba wa ukodishaji wa ndege bila kuijulisha wizara.

Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, mkataba huo uliisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 69 ambazo zilitokana na matengenezo ya ndege hiyo pamoja na riba.

Mbali na Chizi, Dk Mwakyembe pia aliwasimamisha kazi Mwanasheria wa shirika hilo, Amini Mziray, Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Justus Bashara na Kaimu Mkurugenzi wa Biashara, Josephat Kagirwa.

TPA
Baada ya mabadiliko hayo ya ATCL, mwaka huo huo Dk Mwakyembe aliwasimamisha kazi vigogo wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa tuhuma za ufisadi, na kufikisha idadi ya wafanyakazi aliowasimamisha kazi katika Mamlaka hiyo kufikia 23.

Baadhi ya waliosimamishwa kazi na nyadhifa zao kwenye mabano walikuwa Bakari Kilo (Mkurugenzi Uhandisi), Raymond Swai (Meneja Uhandisi), Florence Nkya (Mkurugenzi wa Mipango) na Mahebe Machibya (Meneja Ununuzi na Ugavi).

Wengine ni Teophil Kimaro (Meneja Ununuzi), Mary Mhayaya (Afisa Uhandisi Mkuu), Ayoub Kamti (Mkurugenzi wa Tehama), Mathew Antony (Meneja Kitengo cha Kontena), Maimuna Mrisho (Mkurugenzi wa Mifumo wa Menejimenti).

Wengine ni Fortunatus Sandalia (Askari kitengo cha Ulinzi), Fadhili Ngolongo (Kitengo cha Marine), Mathew Antony (Meneja Kontena), Mohamed Abdullah (Kitengo cha Mafuta), Kilimba (Idara ya ulinzi) na Owen Rwebu.

Mwakyembe alisema katika ripoti ya uchunguzi, iligundulika kwamba baadhi ya vigogo wa Bandari wanamiliki kampuni ambazo zinafanya kazi za TPA.

Pia, alisema kuna mtandao mkubwa unaofanywa kwa watu mbalimbali kwa kushirikiana na vigogo wa bandari ili kufanikisha wizi katika bandari.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: