BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WALIOCHOTA FEDHA ZA AKAUNTI YA TEGETA ESCROW KUFILISIWA MALI, MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI KUVULIWA CHEO NA KAMATO YA ZITTO KABWE..

http://freemedia.co.tz/daima/wp-content/uploads/2014/11/zitto1.jpg
MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, amesema kamati yake itatoa hoja ya kuanza mchakato wa kikatiba wa kumvua ujaji, Mwanasheria Mkuu wa Tanzania, jaji Frederick Werema.

Mbali na dhamira ya kutaka jaji Werema avuliwe ujaji pia, Zitto amesema kamati yake itapendekeza watu wote waliohusika katika kashfa ya wizi wa akaunti ya Tegeta Escrow, wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufilisiwa mali zao.

Zitto, alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na Tanzania Daima Jumapili, kuhusu sakata la Escrow linaloendelea hivi sasa.

Majibu ya Zitto yalitokana na maswali ya gazeti hili yaliyotaka kujua hatua zitakazopendekezwa na kamati yake baada ya kukamilisha kazi ya kupitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali(CAG), juu ya akaunti ya Tegeta Escrow.

Alisema kimsingi kilichofanyika katika tukio hilo ni zaidi ya wizi wa kawaida na kwamba wahusika ni vema wakafilisiwa mali zao kisha wachukuliwe hatua nyingine za kisheria.

“Suala hili sio wizi wa kawaida bali ni ‘money laundering’. Kwa hiyo kufilisiwa ili kurejesha fedha hizo ni hatua nyingine itakayopendekezwa”alisema Zitto.

Alisema hatua hiyo itakuwa ni fundisho kwa wengine huku akikumbushia matukio ya wizi wa fedha za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje(EPA) na sakata la kampuni ya kufua umeme wa Richmond.

Alisema kamati yake bado inaendelea na kazi na kwamba walichogundua ni kuwa fedha zilizokuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow zilikuwa za umma na kwamba kampuni ya Pan Africa Power Resources (PAP) hawakuwa na uhalali wa kuchukua fedha hizo.

“PAC bado inaendelea na kazi. Watu wote ambao wamehusika katika wizi huu tutapendekeza wawajibishwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.”alisema

Tishio kwa wabunge

Baadhi ya wabunge wanaonekana vinara wa kusimamia suala hilo wanaelezwa kutishia maisha ambapo mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, ameshatoa ripoti polisi

Wasiwasi wa usalama wa wabunge hao umeongezeka zaidi baada ya taarifa kuwa mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM), kulishwa sumu akiwa safarini nchini Uingereza

Mkono inadaiwa ndiye anayejua sakata la IPTL kwakuwa kwa muda mrefu amekuwa akishiriki kwenye kesi akisimamia Tanesco na wizara ya Nishati na Madini

Mbunge huyo anadaiwa kuvujisha siri ya uchotwaji wa fedha hizo kwakuwa Wizara ya Nishati na Madini mwanzoni mwa mwaka huu haikuingia makataba wa kuitumia kampuni ya uwakili ya mbunge huyo

Hata hivyo Mkono, mwenyewe mara kadhaa alishakanusha madai ya kushiriki kwenye kuvujisha siri za ufisadi huo wala kuwa nyuma ya sakata hilo.TANZANIA DAIMA
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: