BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAZIRI MKUU WA ZAMANI JAJI JOSEPH WALIOBA NAMNA ALIVYOONJA KARAHA, SHUBIRI NA MAUDHI YA KATIBA.

http://zanzibardaima.files.wordpress.com/2012/06/joseph-warioba1.jpg 
Wengi hawakutarajia kuwa mdahalo muhimu wa kuichambua Katiba inayopendelezwa ungevunjika takriban nusu saa tu baada ya kuanzishwa kwake.


Historia nzuri ya midahalo iliyofanyika hapo awali katika Hoteli ya Blue Pearl au maeneo mengine katika hatua mbalimbali za mchakato wa Katiba Mpya, iliwapatia mori mamia ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam kuhudhuria mdahalo huo uliofanyika Jumapili iliyopita.


Hata hivyo, safari hii mambo hayakuwa ilivyotarajiwa. Wingu jeusi lilianza kutanda mapema katika mdahalo huo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, baada ya vijana wahuni kuanza kunyanyua mabango na hatimaye kuzua vurugu kubwa wakati Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba akihutubia.


Ni bahati mbaya ambayo wachambuzi wa masuala ya siasa nchini wanaona kuwa imetia doa sifa ya nchi katika demokrasia na kuibua udhaifu katika ulinzi na usalama.


Mapema baada ya mdahalo kuanza, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Joseph Butiku aliwataka washiriki wa mdahalo huo kutoa hoja zao kwa amani na kuvumiliana.


“Tupo hapa kujadili Katiba Inayopendekezwa kama Watanzania, Raia wa Tanzania…hatuongozwi na sheria au kundi lolote kama ilivyokuwa Bunge Maalumu au Tume ya Mabadiliko ya Katiba…nawaombeni washiriki kujadili kwa utulivu na kwa hoja,” anasema Butiku huku akishangiliwa na kuongeza;


“Tunachotaka hapa tuelewe vizuri Katiba Inayopendekezwa ili kesho tusimlaumu mtu wala wajukuu wasije kutulaumu, vizazi vijavyo pia visije kusema mlikuwa wajinga kufanya uamuzi.”


Bila ya kujua ambacho kingetokea dakika 30 baadaye, Butiku alizidi kuwapatia nguvu washiriki kwa kusema: “Hakuna kutishwa, kuogopa mtu, wala chama au kundi kusimamia msimamo wake na hakuna shinikizo.”


Pamoja na yote hayo, makundi na itikadi zilidumu na kuharibu mdahalo ule. Moja ya wanaotuhumiwa kuanzisha vurugu ni Katibu wa Hamasa wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Paul Makonda ambaye tayari amekanusha tuhuma hizo.


Vurugu hizo zilianzia upande wa kulia wa Ukumbi wa Crystal baada ya kikundi cha vijana wapatao 20 kunyanyua mabango wakati mdahalo ukiendelea. Kikundi hicho kinachodhaniwa kuwa ni cha vijana wa vyuo vikuu wa CCM, kilianza kuimba “CCM, CCM, CCM” baada ya baadhi ya washiriki kuanza kuwanyang’anya mabango hayo. Hapo ndipo mvutano ulipoanza huku baadhi wakirusha viti na kumzongazonga Jaji Warioba.


“Wamechana mabango yetu…walichokifanya ni kuvunja uhuru wetu wa kutoa mawazo,” anasema mmoja ya vijana hao aliyejitambulisha kwa jina la John Ndumbaro na kuongeza;


“Warioba anapingana na Katiba inayopendekezwa lakini sisi tunaipenda na ndiyo maana tumekuja na ujumbe wa kuielewa, kuipenda na kuikubali.”


Asilimia kubwa ya mabango yalikuwa ujumbe unaofanana wa “Katiba inayopendekezwa tumeisoma, tumeielewa na tunaiunga mkono.”


Awali ilidhaniwa kuwa vijana hao wametumwa na CCM. Lakini Ndumbaro anaeleza kuwa nchi inawagusa watu wote na wao sio wafuasi wa chama chochote cha siasa isipokuwa ni watetea nchi. Katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM Nape Nnauye hataki kusemea jambo hilo kwa maelezo kuwa hayupo ofisini.


Baadhi ya wanaharakati na wananchi akiwamo Deus Kibamba hawataki kuamini kama kikundi kilichovuruga mdahalo ule ni matokeo ya hila za chama tawala.


“Sitaki kuamini kuwa wale vijana wahuni walitumwa na CCM, sitaki kuamini hata kidogo…hali ile ni ‘disaster’ (maafa),” anasema Kibamba na kuongeza;


“Hii ni laana kubwa ndiyo maana mvua mwaka huu zinashindwa kunyesha…ni laana…kumsukuma mtu kama Warioba kama mtoto mdogo, haivumiliki hata kidogo.”


Iwapo hali ya uvunjifu wa amani itaendelea, Kibamba anasema itajenga hofu miongoni mwa wananchi na kufanya watu wawe wanahudhuria katika mikutano ya Katiba kama Ubungo Plaza na Kibandamaiti, Zanzibar wakiwa wamebeba bastola.


Kibamba ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata) anasema: “Ulinzi na Usalama umekwisha kabisa. Hutegemei eneo waliopo viongozi wa kitaifa kama Warioba mtu akathubutu kunyanyua kiti au mzee kama Rais Mwinyi akapigwa kibao kirahisi bila ya walinzi kuzuia. Tayari Rais Jakaya Kikwete ameonya kampeni za mapema na kubainisha kuwa muda uliopangwa kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni haujafika licha ya ukweli yenye mwenyewe akisema anaamini Katiba Inayopendekezwa itapitishwa.


“Ni fedheha kwa taifa. Warioba ni Makamu wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu halafu vijana wanashindwa kumheshimu…hii ni ‘crisis’ (dhoruba) kwa taifa,” anasema Mtafiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Patience Mlowe.


Mtafiti huyo analaani vijana kutumika kisiasa na kuongeza kuwa ifikie kipindi watu wakubali kutofautiana kimawazo na kuwaomba wana-CCM watulie kwa sababu vyama na Tume ya Mabadiliko ya Katiba walishafanya yao hivyo ni muda wa kupeana elimu.


“Sisi kama Taasisi za Kiraia tunahofu sana na kile kilichotokea na tunaweza kuzomewa kama walivyofanya jana (juzi) kwenye mdahalo. Hii inarudisha nyuma demokrasia na harakati za NGOs.


“Hata hivyo, tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi, hatutarudi nyuma, tutafanya kazi zetu bila kumwogopa mtu na tunaitaka Serikali ihakikishe hali hiyo haijirudii tena,” anaongeza Mlowe.


Umoja wa Katiba ya wananchi nao wanalaani kitendo alichofanyiwa Warioba na kubainisha ni jitihada za baadhi ya waovu kuzuia wananchi kupata elimu ya Katiba Inayopendekezwa.


“Hamtaki kusikiliza hoja za Warioba mnamfanyia vurugu…nani ana hatimiliki ya fikra, naona tunajidanganya. Mama Tanzania inahitaji upendo, amani na utulivu na hata kama watu wakiondoka nchi inaendelea,” anasema Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia.


Ili utoaji wa elimu juu ya Katiba Inayopendekezwa ufanikiwe ni lazima pande mbili zinazokinzana zivumiliane na kubishana kwa hoja. Matumizi ya vurugu kama njia ya kupaza hoja haziwezi kukuza demokrasia na kuwapatia Watanzania Katiba Inayopendekezwa.


Wapiga kura ndiyo watakaoamua upande gani kati ya mbili zinazovutana kwamba uko sahihi na kuunga mkono na siyo watu kugombea hoja kupitia hoja zitakazotolewa na pande zinazounga mkono Katiba hiyo na wale wasioiunga.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: