BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

TOCHI YA MOROGORO: WATOZA USHURU MAEGESHO YA MAGARI, ACHENI KUDHALILISHA WATU.

Gari ndogo likiwa limefungwa unyororo kando ya barabara ya Old Dar es Salaam eneo la kutokea daladala ziendazo nje ya Manispaa ya Morogoro na wafanyakazi wa kampuni ya kutoza ushuru ya maegesho ya magari, hata hivyo kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wamiliki wa magari kutokana na adha hiyo isiyofuata taratibu. Juma Mtanda.

Ally Mkoreha, Morogoro.
Vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wa wananchi wanaotumia magari, vinavyofanywa na baadhi ya vijana walioajiriwa na kampuni zinazotoza ushuru wa maegesho ya magari, katika mji wa Morogoro, vinazidi kuota mizizi na kuwa kero kubwa. 


Unyanyasaji na udhalilishaji huo, unatokana na vitendo vya vijana hao, kufunga kwa minyororo na kuyakokota magari ya watu pengine bila hata sababu za msingi. 


Mbaya zaidi, wanafanya hivyo kwa ubabe mkubwa unaoambatana na kuharibiwa kwa magari ya watu. 


Inavyoonekana, vijana hao wanataka kuihamishia Mjini Kasoro Bahari, kadhia iliyokuwa ikifanywa na wafanyakazi wa kampuni inayotoza ushuru wa maegesho ya magari, katika Jiji la Dar es Salaam. 


‘Big Up’ sana kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mecky Said Sadiq kwa kukomesha kadhia iliyokuwa inadhalilisha watu na hasa wanawake na raia wa kigeni. 


Matukio kadhaa ya hivi karibu ya watumishi wa kampuni moja ya kutoza ushuru wa maegesho katika mji wa Morogoro, ndiyo yanayotusukuma kuandika katika safu hii. 


Tunaandika kwa sababu matukio hayo, yameashiria udhalilishaji, unyanyasaji na kudharauliwa kwa watumiaji wa magari wasiokuwa na hatia. 


Lakini pia matukio hayo, yameashiria kuamsha hasira za wananchi wasiopenda namna magari ya watu yanavyofungwa minyonyoro na kukokotwa, bila kutumia busara. 


Katika moja ya matukio yaliyotokea wiki iliyopita, wafanyakazi wa kampuni ya kutoza ushuru, walilifunga kwa minyonyoro gari lililokuwa limeegeshwa kando kando ya barabara baada ya kuishiwa mafuta. 


Baada ya kutambua kuwa gari lake limeishia mafuta tena likiwa mbele ya Kituo cha Teksi kilichoko karibu na Daraja la Shani, mmiliki alilitoa nje ya barabara na kuliegesha kando. 


Hatua hiyo ilifuatiwa na kuwaarifu madereva teksi kwamba gari lilikuwa limeishiwa mafuta na kwamba anayafuata katika Kituo cha Gapco ambacho hakiko mbali na mahali alipoegesha gari. 


Madereva walimwelewa na hata wakachukua jukumu la kusaidia kumlindia gari lake. 


Kwa bahati mbaya mtu huyo, hakupata mafuta katika Kituo cha Gapco, lakini msamaria mmoja alimsaidia kumpeleka katika kituo kingine cha mafuta na baada ya muda mfupi, alirejea akiwa na mafuta kwenye galoni. 


Jambo la kushangaza, alipofika mahali ambapo gari lake aliliegesha, mwananchi huyo alishitushwa kuwaona watoza ushuru, wakiwa wameshalifunga gari lake kwa kutumia minyongoro eti kwa madai kuwa liliegeshwa pasipostahili. 


Hata hivyo, vijana hao walizungukwa na wananchi walionekana kuwa ni wenye hasira, wakipinga gari hilo kukokotwa. 


Mwenye gari aliwataka watoza ushuru kuliachia gari lake, lakini kwa ubabe walimparamia, naye akajibu mashambulizi huku umati mkubwa wa wananchi wakionyesha hamu ya kutaka kumsaidia. 


Katika tukio hilo, mmiliki wa gari alichaniwa fulana aliyokuwa ameiva na mkono wake wa kushoto, ulipata mchubuko. 


Hakika, tunadiriki kusema huu ni udhalilishaji na unyanyasaji mkubwa wa watu. Hivi katika akili za kawaida, watumishi hao wanategemea gari lililoishiwa mafuta barabarani libebwe mgongoni. 


Lakini pia gari lile halikuwa katikati ya barabara kwamba pengine lilikuwa linasababisha usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara, mabavu yaliyotumika ni ya nini. 


Tunawashukuru sana askari wa Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani, kwa busara zao zilizosaidia kutuliza jazba za wananchi, vinginevyo usalama wa vijana hao na hata magari yaliyokuwa katika eneo hilo, ungekuwa hatarini. 


Tukio hilo, lilitanguliwa na kukamatwa gari la mhadhiri mwanamke katika Chuo Kikuu cha Mzumbe. Gari hilo lilikamatwa na kufungwa minyororo likiwa limeegeshwa katika maegesho ya wateja wa Benki ya CRDB Tawi la Masika. 


Gari hilo lilikokotwa hadi katika Yadi ya kampuni ya utozaji ushuru licha ya watu kuwaambia watoza ushuru kuwa gari liliburuzwa kwa uonevu maana lilikutwa katika maegesho ya CRDB. 


Lilipofuatwa, bamba la gari lilikutwa limeharibiwa na uharibifu huo haukufidiwa kabisa. 


Jamani, huu kama si uonevu na udhalilishaji tuuite nini. Tunawasihi watumishi wa kampuni hiyo wawe waungwana na wanaotumia busara, ili kuepusha hasira za watu wanaonyesha kuchoshwa na unyanyasaji.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: