BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

CCM KUCHUKUA HATUA ZAIDI KWA VIGOGO WAO WALIOTAFUNA FEDHA ZA ESCROW, KUKIONA CHA MTEMA KUNI.

http://www.bongocelebrity.com/wp-content/uploads/2014/01/75f2Nape-Nnauye.jpgKatibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.

IMEELEZWA kuwa, maamuzi yote ya kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM kilichokutana juzi, kujadili masuala ya kimaadili kwa wanachama wake wanaotajwa kuhusika katika sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), yatafikishwa katika Kamati Kuu ya Chama kwa hatua zaidi.

Hayo yalibainishwa jana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akiwa katika Ofisi Kuu ya CCM- Kisiwandui mjini hapa, ambapo alisisitiza kuwa, taarifa za kikao hicho hazitangazwi kwa vyombo vya habari au kwa umma.

Juzi Kamati Ndogo ya Maadili, ilikutana jijini Dar es Salaam chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula ili kujadili na kuchukua hatua dhidi ya wanaCCM wanaotajwa kuhusika katika sakata la Escrow.

Kikao cha Kamati ya Mangula kilikuwa kinatekeleza agizo la Kamati Kuu, iliyokutana Zanzibar mwishoni mwa wiki chini ya Rais Jakaya Kikwete ili kujadili masuala mbalimbali ya chama hicho na ilipofika katika suala la Escrow, ndipo ikaagiza Kamati Ndogo ya Maadili ikutane Januari 19, 2015 huku ikiwataka watuhumiwa wenye dhamana katika chama wajipime.

Nape, akizungumza jana alisema kutokana usiri wa kikao cha Kamati ya Mangula, baadhi ya watu wamekuwa wakijaribu kupotosha ukweli wa mambo kuhusu taarifa za kikao hicho na kuzua taharuki kubwa kwa jamii.

“Taarifa za kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili kwa ajili ya kushughulikia viongozi wa chama waliotajwa katika sakata la Escrow, zitapelekwa katika kikao cha Kamati Kuu na sio kutangazwa kwa waandishi wa habari au umma,” alisema.

Alisema hizo ndizo taratibu za CCM na kwamba chama hicho kimejipangia ratiba yake kwa mujibu wa vikao vya chama.

Nnauye alisema hayo kufuatia kuwepo kwa taarifa mbalimbali kuhusu kikao hicho na maamuzi yake kwa ujumla, ambapo alisema ni taarifa za uzushi mtupu, zenye lengo la kupotosha jamii.

Baadhi ya wanaCCM wanaotuhumiwa kunufaika na fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, Mbunge wa Sengerema, Ngeleja na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye amevuliwa madaraka kutokana na sakata hilo.

Profesa huyo ni mbunge wa Muleba Kusini. Wataka Urais waonywa Aidha, Nnauye alisema CCM inawaonya watu wenye nia ya kugombea nafasi za urais kupitia CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu na wapambe wao, kuacha kusambaza taarifa za uzushi ambazo nia yake kukigawa chama.

Akifafanua, Nnauye alisema wagombea hao kwa kuwatumia wapambe wao, wamekuwa wakitoa taarifa za uongo za kila siku kwamba chama kinatarajia kukaa kikao kuwajadili wao.

“Nataka niseme kwamba CCM ina shughuli nyingi, sio kupoteza muda kuwajadili wagombea hao...tunawapa tahadhari kuacha kutoa taarifa za uzushi ambazo zinawaweka katika wakati mgumu,” alisema.

Alisema uvumi unaosambazwa na wapambe hao, unawaweka wakati mgumu wagombea wa nafasi za urais ambao wamejitangaza wakati muda wa kufanya hivyo haujafika kwa mujibu wa ratiba ya kalenda ya CCM.

Alisema CCM bado haijatoa ratiba ya mchakato wa kuwania nafasi za uongozi za juu, ikiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano, wabunge na wawakilishi.

“Ratiba ya wagombea wa nafasi za juu za urais bado haijatolewa na CCM, hivyo watu wasidanganyane,” alisema.

Ndani ya CCM, licha ya orodha ndefu ya makada wanaotajwa kutaka kuwania Urais kupitia chama hicho, wengine sita walishaonywa na kutakiwa kutoanza mchakato mapema huku wakiwekwa chini ya uangalizi maalumu katika kipindi cha mwaka mmoja kinachoisha mwezi ujao.

Hao ni pamoja mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira.

Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano na Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja. Akaunti ya Tegeta Escrow ilianzishwa ili kutunza fedha za malipo ya tozo ya uwekezaji kwa IPTL, yaliyokuwa yanafanywa na Tanesco.

Kabla ya mzozo kuhusu ukokotoaji wa tozo hiyo kuibuka na kuanzishwa kwa akaunti hiyo, Tanesco ilikuwa inalipa tozo hiyo moja kwa moja kwa IPTL. Kwa ujumla, akaunti hiyo iliundwa ili kuhifadhi fedha za IPTL wakati suluhu inatafutwa kuhusu kiwango cha tozo.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: