BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

DK SHEIN AFUATA NYAYO ZA JK, SERIKALI YAKE YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR YAFUTA ADA YA WANAFUNZI SHULE ZA MSINGI

 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein akikagua gwaride la heshima la vikosi vya ulinzi na usalama wakati wa sherehe za miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizofanyika kwenye uwanja wa Amaan mjini Unguja jana. (Picha na Ikulu).

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imefuta ada ya wanafunzi wa shule za msingi, ikiwa ni utekelezaji wa dhamira ya mapinduzi ya kuwapatia wanafunzi wote elimu bure, kama ilivyoasisiwa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume.


Uamuzi huo ulitangazwa rasmi jana na Rais Dk Ali Mohamed Shein, wakati akihutubia wananchi katika uwanja wa Amaan mjini hapa katika kilele cha maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

“Kuanzia sasa Serikali inafuta ada ya wanafunzi wa shule za msingi walizokuwa wakitoa wazazi, ikiwa ni malengo ya kutekeleza dhamira ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwapatia wanafunzi wote elimu bure, kama ilivyoasisiwa na hayati Karume na kutangazwa Septemba 23, mwaka 1964,” alisema.

Alisema mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta za elimu, afya na usambazaji wa nishati ya umeme, ni mambo ambayo yalikuwa moja ya vipaumbele, vilivyowekwa katika Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Alisema katika mikakati ya malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, kama yalivyoasisiwa na jemedari Abeid Amaan Karume, serikali imeamua kuanzia sasa kufuta malipo ya ada ya fedha, walizokuwa wakitoa wazazi kwa wanafunzi wa shule za msingi.

Kwa upande wa sekta ya afya, Dk Shein alisema serikali itahakikisha wajawazito wote wanaojifungua katika hospitali za Serikali, hawatozwi fedha kwa ajili ya kupata huduma hiyo.

Aidha, alisisitiza kwamba wazazi hawatachangia tena malipo ya ada kwa ajili ya mitihani ya kidato cha nne hadi cha sita, ambapo jukumu hilo litabebwa na serikali.

Alisema lengo ni kuona akinamama wanapata huduma bora za afya pamoja na kujifungua kwa salama kwa kutumia madaktari bora na wauguzi wenye sifa.

“Nilitoa kauli yangu kwamba wajawazito wapatiwe huduma bure za uzazi katika hospitali za serikali, kwa lengo la kuona kwamba vifo vinavyotokana na akinamama na watoto vinapungua,” alisema.

Hatua hiyo ya Zanzibar ya kutangaza elimu bure, imekuja wakati Rais Jakaya Kikwete akiwa pia amewahi kunukuliwa kwamba, Serikali inakusudia kufuta karo kwa wanafunzi wa shule za sekondari za serikali, ikiwa ni jitihada za kuinua elimu na kupunguzia wazazi mzigo.

Kulinda mapinduzi
Katika sherehe hizo zilizohudhuriwa na viongozi wakuu wa Serikali ya Muungano, wakiongozwa na Rais Kikwete, Dk Shein alitaka Wazanzibari kulinda Mapinduzi ya Zanzibar, ambayo ndiyo kielelezo cha wananchi kuondokana na utawala dhalimu na wazalendo walio wengi kushika hatamu ya kuongoza dola.

“Thamani ya Mapinduzi ya Zanzibar ni wananchi wazalendo kuishi huru katika nchi yao na kufanya shughuli za maendeleo bila ya kuingiliwa na mtu yeyote,” alisema.

Alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ambayo inatimiza miaka minne sasa, imepiga hatua kubwa ya kutekeleza dira ya maendeleo ya 2020.

Serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa, inaundwa na vyama vya CCM na CUF. Pia, Dk Shein alisema Zanzibar imepiga hatua katika mpango wa kukuza uchumi na kupambana na umasikini (Mkuza 11) na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2010-2015.

Mafanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ni pamoja na kukua kwa uchumi kutoka asilimia 6.4 mwaka 2010 hadi asilimia 7.4 . Matarajio zaidi ni uchumi kukua na kufikia asilimia 7.8 mwaka huu.

Aidha, alisema mafanikio ya ukuaji wa uchumi, yamekuja kutokana na kuweka mkazo zaidi katika ukusanyaji wa mapato na kuziba mianya yote inayovujisha mapato kupitia taasisi zake, ikiwemo Bodi ya Mapato (ZRB) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Alisema taasisi hizo, zimefanikiwa kukusanya Sh bilioni 484 mwaka 2011-2013, ambapo makusanyo yaliongezeka na kufikia Sh bilioni 997.

“Nazipongeza taasisi za ukusanyaji mapato nchini (ZRB) pamoja na (TRA) kwa kufanya kazi kubwa ya kukusanya mapato pamoja na kuziba mianya iliyokuwa ikivujisha mapato katika vyanzo mbali mbali,” alisema.

Aidha, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na mikakati yake ya kuhakikisha maeneo huru ya uchumi yaliyopo Fumba kwa upande wa Unguja, yanaimarishwa na kuendelezwa kwa ajili ya kuwakaribisha wawekezaji mbali mbali kuwekeza.

Alisema katika kipindi cha miaka minne, miradi ya maendeleo ya uwekezaji ipatayo 141, imepitishwa na mamlaka ya vitega uchumi na uwekezaji (ZIPA) na ajira za vijana 5,616 zitapatikana.

Alifafanua kwamba mafanikio ya uwekezaji yamekuja kutokana na kuwepo kwa mazingira ya amani na utulivu kwa wananchi na wageni wanaowekezaji nchini.

“Tumepiga hatua kubwa katika sekta ya uwekezaji nchini ambayo mafanikio yote hayo yamekuja kutokana na kuimarika kwa mazingira ya amani na utulivu... nawaomba wananchi kamwe wasichezee amani iliyopo kwa maslahi ya wachache,” alisema.

Aidha alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetekeleza ahadi zake za kuimarisha zao la karafuu katika mikakati ya mpango wa miaka 10 ya kufufua zao hilo kuwa la uchumi.

Akifafanua, alisema katika kipindi cha miaka minne Serikali imefanikiwa kupandisha bei ya karafuu kutoka Sh 5,000 hadi kufikia Sh 14,000 huku mkulima akipata faida ya asilimia 80 ya karafuu inayouzwa katika soko la dunia.

Alisema ongezeko la ununuzi wa karafuu, limeimarika ambapo jumla ya tani za karafuu 11,477 zilisafirishwa nje ya nchi. Mafanikio hayo yametokana na Serikali kudhibiti magendo ya karafuu kutoka kwa baadhi ya wakulima wasiokuwa waaminifu.

“Wakulima wa karafuu sasa wamepiga hatua kubwa ya zao hilo kwa kuingiza mapato mengi baada ya kukubali kuuza karafuu zao serikalini na kuachana na magendo yaliyokuwa yakilikosesha taifa fedha nyingi za kigeni,” alisema.

Mapema, Dk Shein alisema kwamba Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Muungano wa mwaka 1964, ndiyo dira ya mafanikio yatakayowawezesha Watanzania kupiga hatua kubwa ya maendeleo.

Uchaguzi, kura ya maoni
Wakati huo huo, Dk Shein alisema mwaka huu ni wenye matukio makubwa ya kihistoria, ikiwemo kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa, inayotarajiwa kufanyika Aprili 30 na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba.

Kwa mujibu wa Dk Shein, matukio hayo ni sehemu ya kielelezo cha kukua kwa demokrasia nchini. Alihimiza kuimarishwa kwa amani na utulivu. Alionya kuwa shughuli hizo zisitumike kama kigezo cha kuvuruga amani na utulivu wa nchi, ambao ni hazina kubwa kwa Watanzania.

“Natoa salamu zangu za mwaka mpya kwa wananchi kwa kuwataka kuimarisha amani na utulivu katika harakati za kisiasa na maendeleo zaidi kuelekea katika uchaguzi mkuu ambao utatuhakikishia kukomaa kwa demokrasia,” alisema.

Vikosi vya ulinzi
Katika sherehe hizo, Dk Shein alipokea salamu ya heshima kutoka vikosi vya ulinzi na usalama na kupigiwa mizinga 21.

Alikagua gwaride ambalo baadaye lilipita mbele ya viongozi wakuu. Gwaride hilo lilijumuisha vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Magereza, JKU, KMKM na Valantia.

Kikosi cha makomando wa JWTZ kilichopita mbele ya viongozi wakuu kwa mwendo wa kukimbia wa ukakamavu, kilivutia wananchi wengi ambao walishangilia.

Viongozi waliohudhuria Viongozi wakuu wa nchi, wakiongozwa na Rais Kikwete, walihudhuria sherehe hizo za miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Wengine ni Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Wengine waliohudhuria ni ni marais na mawaziri wakuu wastaafu wa Jamhuri ya Muungano.

Marais wastaafu ni Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa. Kwa upande wa Waziri wakuu wastaafu, ni Frederick Sumaye na Salim Ahmed Salim.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: