JAJI JOSEPH WALIOBA AWATAJIA WATANZANIA RAIS AJAYE 2015 ANAFAHAMIKA LAKINI AMTAJA.
Jaji Warioba.
Dar es Salaam. Wakati Taifa zima likiwa katika kitendawili cha kumjua kiongozi wa nchi atakayepatikana baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema Rais ajaye anafahamika.
Akizungumza katika mahojiano maalumu jana, Jaji Warioba alisema si kazi ngumu kwa Watanzania kumfahamu rais ajaye kwa kuwa katika miaka 50 tangu tupate uhuru, Watanzania wanazijua sifa za kiongozi bora.
Jaji Warioba alisema; “Tatizo la kumjua rais afaaye tunalikwepa lakini linafahamika. Wanaotumia fedha na lugha chafu katika kampeni na hao ndiyo wasiotakiwa.”
“Katika miaka 50 tunazijua sifa za kiongozi bora. Hapa tunakwepa tatizo tu. Tatizo ni matumizi ya fedha na lugha chafu katika kampeni,” alisema Jaji Warioba ambaye pia ni waziri mkuu mstaafu.
Hadi sasa wanasiasa zaidi ya 20 wakiwamo wa CCM na upinzani wamekuwa ama wanatajwa au wameonyesha nia ya kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Ukiacha wale wanaotajwa, wanasiasa waliotangaza nia hiyo kutoka CCM ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangala na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, huku Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed akitangaza nia kupitia ADC.
Akifafanua zaidi, Jaji Warioba alisema kila mtu anaweweseka kuhusu kiongozi anayefaa ingawa ni kazi rahisi kumjua kutokana na ujuzi tulionao wa miaka zaidi ya 50 ya uhuru.
Kadhalika, Jaji Warioba alisema viongozi wa Serikali hawana budi kuangalia taswira ya uchaguzi mkuu ujao kupitia uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao umeonekana kuwa na kasoro zilizosababisha vurugu.
“Nchi hii ina amani na tujitahidi kuilinda amani yetu. Katika uchaguzi huu tufanye kila tuwezalo kuweka maandalizi yenye umakini,” alisema Warioba na kuongeza: “Nasisitiza amani. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni funzo.”
Tetesi kuwania urais
Hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari, likiwamo gazeti la chama tawala, viliripoti tetesi kuwa Jaji Warioba anaandaliwa kuwania urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), tetesi ambazo kiongozi huyo alizikanusha vikali.
Jaji Warioba alisema amelitumikia Taifa kwa muda mrefu na aling’atuka kwa mapenzi yake, hivyo hawezi kurudi tena katika siasa.
“Nimetukanwa sana, nimebezwa, nimekejeliwa kwa mambo mengi lakini ukweli ni kuwa nilifanya uamuzi wa kung’atuka katika siasa miaka 20 iliyopita na siwezi kubadili uamuzi wangu,” alisema.
Akizungumzia baadhi ya wanasiasa kutumia jina lake katika majukwaa na baadhi kumkashifu kwa madai kuwa alimsaliti Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Jaji Warioba aliwataka wanaofanya hivyo wasitumie jina lake kusafisha njia zao katika siasa.
“Nimeitumikia nchi hii kwa miaka 30, kuanzia mwaka 1966 hadi 1995 nikang’atuka. Niliufanya uamuzi huo miaka 20 iliyopita, nikabaki katika uongozi wa chama nako nikaachia ngazi 2002. Mjue kuwa nilifanya hayo kwa umakini mkubwa,” alisema.
Utata Kura ya Maoni
Katika mahojiano hayo, pia Jaji Warioba alizungumzia mchakato wa kuboresha Daftari la Wapigakura na Sheria ya Kura ya Maoni kuwa mwingiliano wake hasa katika kipindi cha uchaguzi utaleta mkanganyiko.
Akizungumzia mkanganyiko huo, Jaji Warioba alisema sheria inaweka utaratibu maalumu wa mchakato wa kura ya maoni ambao alisema hautaendana na ratiba ya uandikishwaji katika daftari hilo.
“Kwa utaratibu uliowekwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itamaliza kazi Machi na wakati huo kura ya maoni imepangwa kufanyika Aprili. Kwa hali hiyo hatuna uhakika kama Tume itakamilisha kazi yake katika kipindi hicho,” alisema.
Jaji Warioba alisema Sheria Kura ya Maoni Na. 3 ya mwaka 2014 inasema kuwa wananchi wanatakiwa kupewa elimu ya kura ya maoni kwa kipindi cha miezi miwili na mwezi mmoja wa kampeni lakini hadi sasa hakuna ratiba inayoeleweka, jambo ambalo linaleta mwingiliano.
“Hii ni Januari, kama watafuata sheria na kuanza kutoa elimu kwa kipindi cha miezi miwili, ina maana itakuwa ni Aprili na Mei, ukijumlisha mwezi mmoja wa kampeni ambao ni Juni ina maana kura itapigwa Julai. Ikumbukwe kuwa mwezi huo mbio za uchaguzi zitakuwa zimepamba moto,” alisema. Kura hiyo ya maoni imepangwa kufanyika Aprili 30.
Jaji Warioba alisema ni vyema kama mchakato wa Katiba mpya ukaenda kama sheria inavyosema kwani kinyume na hapo mambo yataharibika na pengine vurugu zinaweza kutokea katika uchaguzi mkuu.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju hakupatikana kuzungumzia utata huo wa kisheria.
Kuhusu matumizi ya BVR
Kadhalika, Jaji Warioba alisema kwa matumizi ya teknolojia BVR katika hatua ya maboresho ya daftari la kudumu la wapigakura, kwa uzoefu alio nao, vifaa hivyo vina utata mkubwa hivyo unahitajika umakini mkubwa.
“Nilikwenda Malawi mwaka 2004 nikaona utaratibu wa BVR umeleta changamoto kwa sababu tu ni teknolojia mpya. Inahitajika elimu ya kina kabla ya matumizi yake,” alisema Jaji Warioba.
Alitoa mfano wa utata wa BVR kuwa iwapo mpigakura atafanya udanganyifu na kujiandikisha mara mbili au zaidi (hata kama atatumia majina tofauti), mashine itafuta majina yaliyozidi na kubaki na taarifa zake katika kituo kimoja tu.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema tume hiyo imeshazifanyia majaribio mashine hizo katika majimbo matatu na zimeonyesha ubora na upungufu ulikuwa mdogo huku zile zenye kasoro zikifanyiwa marekebisho.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment