WATU zaidi ya 40 wanaodhaniwa kuwa majambazi, wameteka mabasi sita ya abiria yanayofanya safari kati ya Jiji la Arusha na Nairobi, Kenya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema atalitolea ufafanuzi leo.
Kamanda Sabas, alisema mabasi hayo yalitekwa juzi saa 8 usiku, baada ya kufika eneo la Mbuga Nyeupe, Wilaya ya Longido, Mkoa wa Arusha.
Taarifa zilizopatikana jijini Arusha, zinasema baada ya majambazi hayo kuteka mabasi hayo yaliyokuwa yakitoka Nairobi kuelekea Arusha, waliwapora mali na fedha abiria wote waliokuwamo.
Taarifa hizo, zinasema majambazi hayo yalifanikiwa kufanya uhalifu huo baada ya kuweka mawe barabarani, na baada ya kuyateka mabasi hayo, waliwaamuru abiria wote kushuka na kulala chini, huku wakipekuliwa na kutakiwa wasalimishe mali zote walizokuwa nazo.
Dereva wa moja ya mabasi yaliyotekwa, mali ya Kampuni ya Perfect Trans, Joseph John, aliwaambia waandishi wa habari kuwa majambazi hayo yalikuwa na silaha za jadi yakiwamo mapanga na mashoka.
“Kundi la majambazi lilikuwa kubwa, yaani walikuwa kama watu arobaini hivi, wametufanyia unyama wa kutisha kwa sababu wanawake walivuliwa nguo na vito vya thamani na wanaume tukivuliwa viatu na kuporwa kila kitu.
“Mimi ndiye nilikuwa dereva wa kwanza kufika na basi katika eneo hili, nilipoona mawe yamepangwa katikati ya barabara, nilisimama ili kujua kilichokuwa kikiendelea.
“Baadaye nilipokuwa nikijaribu kuyakwepa yale mawe, nilipigwa jiwe usoni hali iliyonifanya nishindwe kuendesha gari.
“Wakati wa tukio hilo, baadhi ya wahalifu hao walikuwa hawakufunika nyuso zao na tukio hilo lilidumu kwa zaidi ya dakika 20, kwani kila walipokuwa wakimaliza kupekua abiria wa basi moja, waliwaamuru warudi ndani ya basi na kuhamia katika basi jingine,” alisema Joseph.
Dereva mwingine, Jabir Athumani wa basi jingine la Kampuni ya Perfect, alisema baadhi ya majambazi hayo yalikuwa yakiwataja kwa majina baadhi ya abiria na kuwaamuru watoe fedha walizokuwa nazo.
“Kwahiyo, tunaomba vyombo vya ulinzi na usalama vifuatilie tukio hili kwa umakini wa hali ya juu ili kuwanasa wahusika,” alisema Jabir.
Pamoja na hayo, alisema kuna haja Jeshi la Polisi kurudisha ulinzi uliokuwa ukifanywa na magari ya doria yaliyokuwa katika barabara ya Arusha–Namanga ulioondolewa Aprili, mwaka jana.MTANZANIA
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment