BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

ANDREW CHENGE, PROF ANNE TIBAIJUKA KUWEKWA KITIMOTO NA BARAZA LA MAADILI, KASHFA YA ESCROW YAWATIBULIA MAMBO.


Andrew Chenge

MBUNGE wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kesho atasimama mbele ya Baraza la Maadili kujibu tuhuma za kukiuka maadili ya uongozi na kujipatia Sh bilioni 1.6 ambazo aligawiwa kutoka katika fedha za akaunti ya Tegeta Escrow.

Profesa Anna Tibaijuka ambaye alitimuliwa Uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi kutokana na kujipatia Sh bilioni 1.6 kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira atajibu tuhuma hizo kesho kutwa.

Ratiba iliyotolewa na Baraza la Maadili, jijini Dar es Salaam inaonesha kuwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, William Ngeleja ambaye pia ni Mbunge wa Sengerema, atasimama mbele ya Baraza hilo Jumatatu ijayo.

Wengine watakaopanda kizimbani ni Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma atakayehojiwa Jumatatu ijayo.

Wengine ni Mnikulu Shaban Gurumo atakayehojiwa Machi 4, akifuatiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Ufilisi na Udhamini (RITA), Philip Saliboko na Machi 6 atahojiwa Naibu Kamishna Upelelezi na Kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Loicy Appollo.

Ratiba hiyo inaonesha kuwa Machi 9 atahojiwa Mkurugenzi Mdhibiti Uchumi Mamlaka ya Usafiri wa Anga, Dk Benedict Diu akifuatiwa na Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Gulam Remtullah.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji mstaafu Hamis Msumi alisema ratiba ya kuwahoji viongozi, ilitakiwa kuanza jana ikianza na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo.

Hata hivyo, Gambo aliwasilisha barua kwamba anaumwa na atashindwa kuhudhuria.

Vievile, Gambo aliwasilisha cheti cha daktari akitakiwa kupumzika kwa wiki mbili, jambo lililosababisha Baraza hilo kuahirisha kusikiliza shauri lake hadi hapo litakapopanga kikao kingine.

Kutokana na kuanza kuwapandisha kizimbani watuhumiwa wa sakata la Escrow, Baraza litatoa uamuzi wa ama wahusika hao wafikishwe mahakamani, au la, kulingana na hatia watakazokutwa nazo.

Kashfa ya Escrow iliyonguruma mwaka jana bungeni, imesababisha baadhi ya watuhumiwa kujiuzulu nyadhifa zao na wengine kuvuliwa madaraka, akiwamo Profesa Tibaijuka aliyewekwa pembeni na Rais Jakaya Kikwete Desemba mwaka jana.

Chenge alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti na aliachia wadhifa huo hivi karibuni. Ngeleja aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na Mbunge wa Lupa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini , Victor Mwambalaswa, nao walijiuzulu hivi karibuni.

Chenge na Profesa Tibaijuka kila mmoja alipata mgawo wa Sh bilioni 1.6 huku Ngeleja akipata Sh milioni 40.4 kutoka kwa James Rugemalira wa VIP Engineering and Marketing Limited, zikiwani mgawo wa Tegeta Escrow.

Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mwaka 2006 kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya tozo ya uwekezaji (capacity charges), zilizokuwa zinalipwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kabla hazijakabidhiwa kwa anayelipwa, ambaye ni Kampuni binafsi ya kufua umeme ya IPTL.

Kabla ya hapo Tanesco ilikuwa inalipa moja kwa moja kwa IPTL. Ilifunguliwa ili kutoa nafasi kwa pande hizo mbili kumaliza tofauti zao kuhusu kiwango cha tozo hiyo.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: