BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

BUNGE LA BAJETI KUANZA LEO, WASOMI WANENA KUWA NI BUNGE LA KUONYESHANA MBWEMBWE ZA UCHAGUZI MJINI DODOMA.


Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alipokuwa akiwasili kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma mwaka jana kuwasilisha bajeti ya mwaka 2014/2015.


Dodoma/Dar.
Bunge la Bajeti ya Serikali ya 2015/16 linaanza leo mjini Dodoma kwa mwendo wa mchakamchaka kutokana na kuongezwa saa mbili kila siku ili limalizike Juni 27.



Saa za mjadala katika vikao zimeongezwa ili kuziba pengo la siku 12 zinazopungua na kutoa fursa kwa wabunge kuchangia bajeti za wizara na Bajeti Kuu ya Serikali ndani ya siku 44 ikilinganishwa na siku 56 zilizotumika kupitisha bajeti ya mwaka 2014/15 na miaka ya nyuma.


Kutokana na hali hiyo, wachambuzi wa bajeti, wachumi na wanasiasa wamesema hawatarajii kuona jipya isipokuwa mipasho inayolenga Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.


Serikali imepanga kukusanya na kutumia Sh22.4 trilioni katika mwaka wa fedha 2015/16 ikiwa ni nyongeza ya Sh2.6 trilioni ikilinganishwa na Bajeti ya mwaka 2014/15 ambayo ilikuwa Sh19.8 trilioni.


Kwa miaka iliyopita, baadhi ya wizara zenye majukumu mengi zilikuwa zinatengewa siku mbili au tatu, lakini safari hii hali itakuwa tofauti kwa kuwa zitajadiliwa kwa siku moja tu au mbili kulingana na mjadala utakavyokuwa na mapumziko yatakuwa Jumapili pekee.


Mkurugenzi wa Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa wa Bunge, Jossey Mwakasyuka alisema badala ya Bunge kuanza saa 3.00 asubuhi hadi saa 7.00 mchana na baadaye saa 11 jioni hadi saa 1.45 usiku; sasa litaanza 3.00 asubuhi hadi saa 8.00 mchana na kuendelea saa 10.00 jioni hadi saa 2.00 usiku.


“Ili kuendana na muda, tumeongeza saa kadhaa ili kumaliza shughuli zote zilizopangwa. Siku za Jumamosi zitahesabika kama siku za kazi kama kawaida.” alisema.


Alisema Bunge hilo litamalizika Juni 27 lakini akaongeza: “Tumeacha siku tatu za dharura, kuanzia Juni 28 hadi 30 ili kama kuna jambo lolote la muhimu litajitokeza Bunge linaweza kuendelea kwa muda huo wa siku tatu.”


Alisema kutokana na mabadiliko ya uwasilishaji, ni lazima bajeti iwe imesomwa kabla ya kuanza utekelezaji wa bajeti ya mwaka unaofuata Julai Mosi.


“Inawezekana tukapata kiongozi wa kulihutubia Bunge au katika upitishaji wa bajeti za wizara akidi isitimie na kulazimika shughuli husika kuendelea siku inayofuata. Zamani Bunge la Bajeti lilikuwa likianza Juni hadi Agosti, lakini kwa mabadiliko haya sasa lazima limalizike Juni,” alisema.


Alisema bajeti zote za wizara hadi kufikia Juni 10 zitakuwa zimeshasomwa, Juni 11 itasomwa Bajeti Kuu ya Serikali na kuanza kujadiliwa.


Alisema ratiba hiyo pia inaweza kuvurugika utakapoanza mfungo wa Ramadhani.


Alisema kuchelewa kuanza kwa Bunge kumetokana na kuahirishwa kwa tarehe ya Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa.


“Kama mtakumbuka Katiba Inayopendekezwa ilikuwa ipigiwe kura Aprili 30, sasa baada ya kutangazwa kuwa imeahirishwa, tuliamua kupanga upya ratiba,” alisema.


Alisema Bunge hilo litavunjwa kwa tangazo la Serikali linalotolewa na Rais na si Mkuu huyo wa Nchi kulihutubia Bunge na kulivunja: “Waziri Mkuu, Mizengo Pinda atalihutubia Bunge Juni 27.”


Maoni ya wasomi
Profesa Prosper Ngowi kutoka Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema mbali na Bunge hilo kutekwa na mijadala ya kuelekea uchaguzi ujao, mambo mengine yanayotarajiwa ni wabunge wengi kuonyesha mbwembwe za kuhoji mambo yanayohusu masilahi ya wananchi katika majimbo yao.


Alisema wabunge watakuwa na hoja za kuibana Serikali juu ya miradi mingi iliyokwama katika bajeti zilizopita kutokana na kiwango kidogo cha fedha kilichowasilishwa.


Hoja hiyo iliungwa mkono na Profesa Humphrey Moshi kutoka Idara ya uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) akisema wabunge watahoji utekelezaji wa bajeti iliyopita kwa kuangalia uhalisia wake na mipango ya bajeti itakayojadiliwa kwa Bunge.


“Kila mbunge anatamani kuona mradi wa maendeleo ukikamilika katika jimbo lake, lakini ukiangalia fedha ambazo zimekuwa zikitengwa ni kidogo na za utegemezi, kwa hivyo ningeshauri kwa sasa wangejadili na kushughulikia viporo vya miradi, badala ya kuanzisha vingine wakati kuna madeni ya makandarasi,” alisema.


Mwenyekiti wa Jukwaa la Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi Tanzania (CEOs), Ali Mufuruki alisema hatarajii kuona jambo lolote jipya zaidi ya mijadala ya kuelekea Uchaguzi Mkuu.


“Ninachotegemea kwa sasa ni kuona sehemu kubwa ya mapato yakitumika kwa shughuli za kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao,” alisema.


Wabunge wanena
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila alisema bajeti hiyo haina matumaini kwani miradi ya maendeleo katika bajeti inayomalizika Juni 30 haikutekelezeka kwa asilimia 80.


“Kukwama kwa msaada wa kibajeti zaidi ya Dola 500 milioni kutoka kwa wahisani, kukwama kwa mkopo wa kibiashara ambao siyo kawaida kabisa ambapo Serikali ilitarajia kukopa Dola 800 milioni na kuambulia 300 milioni ni ushahidi tosha wa namna Serikali inavyopumulia mashine,” alisema.


Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamisi Kigwangalla alisema muda wa kuijadili bajeti ni mfupi hali ambayo hujitokeza kila mwaka wa uchaguzi lakini haiwezi kuwanyima wananchi fursa ya kuijua bajeti ya nchi yao.


Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi alisema bajeti hiyo haina jipya, huku akitolea mfano mpango wa Serikali wa kuboresha reli kwa mwaka mmoja wakati ilishindwa kufanya hivyo kwa miaka 50.


Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa alisema tatizo la bajeti hii ni kupunguzwa kwa asilimia 50 fedha za maendeleo... “Unapopunguza fedha za maendeleo wakati tunaambiwa bwawa la umeme la Mtera maji yamepungua hapo si tutegemee kurudi kule kwa Aggreko na Symbion kuuziwa umeme wa ghali.”


Hata hivyo, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema fedha za maendeleo ambazo zimepungua zitapatikana kabla ya Juni 30, mwaka huu... “Niwathibitishie wananchi kuwa fedha hizi zitapatikana bila matatizo yoyote.”MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: