WATANZANIA WAISHI NA UGONJWA WA MAWE NDANI YA FIGO BILA KUJITAMBUA.
Dar es Salaam. Hospitali ya Aga Khan imezindua kampeni ya kupima ugonjwa wa mawe katika figo, ikiwa ni baada ya kubaini kuwa Watanzania wengi wanaishi na maradhi hayo bila kujitambua.
Akizungumza na gazeti hili hospitalini hapo, Mtaalamu Mshauri wa Mfumo wa Mkojo, Dk Ali Akbar Zehri alisema, wamebaini watu wengi wanaopata matibabu wanagundulika kuwa na mawe kwenye figo bila kujitambua kutokana na kutoona dalili ama kuchelewa kuonekana.
Alisema kutokana na hali hiyo, wamezindua kampeni ya kupima, kutoa ushauri bure kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ili kuwapa watu uelewa wa ugonjwa huo, vipimo, ushauri na jinsi ya kujizuia.
Dk Zehri alizitaja baadhi ya dalili za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na maumivu, maambukizi kwenye njia ya mkojo, kusikia kichefuchefu na kutapika, kukojoa mkojo uliochanganyika na damu, homa, muwasho kwenye figo unaosababishwa na usaha katika figo, uvimbe kwenye figo na kushindwa kufanya kazi sawasawa.
“Watu wengi wana tatizo hili lakini hawatambui mapema kutokana na kutokupima mapema, lakini wakipima wanapata uelewa, hivyo ugonjwa ukiwa katika hatua za awali itakuwa rahisi kwao kubaini na hatimaye kuanza tiba, ” alisema Dk Zehri.
Mtaalamu wa vipimo vya magonjwa mbalimbali katika hospitali hiyo, Dk Monique Leischner alisema kuwa, mawe katika figo yapo ya aina mbalimbali ikiwamo madogo ambayo dalili zake hujificha na makubwa ambayo huonekana wazi.
Pasco Mbagala ni miongoni mwa waliojitokeza kupima ugonjwa huo katika siku ya kwanza ya uzinduzi ambapo alisema kuwa aliona tangazo katika televisheni na kuamua kupima ili kuona kama ana tatizo au hana.
Naye Valentine Kazwaga alisema kuwa alitumiwa ujumbe na rafiki yake akimuonyesha tangazo hilo, hivyo akaamua kwenda kupima.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment