BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HUYU NDIYE MKULIMA MWENYE ELIMU YA MSINGI ANAYECHUKUA FOMU YA KUGOMBEA URAIS LEO MKOANI DODOMA.



Mkulima kutoka Kigoma, Elidephonce Bilohe akiondoka baada ya kushindwa kuchukua fomu kutokana na kutokamilisha malipo ya ada ya fomu hizo. Hata hivyo, alikamisha baadaye na atachukua fomu leo Picha na Edwin Mjwahuzi


Dodoma.
Makada watatu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwamo wa darasa la saba, jana walijitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kuomba kuteuliwa na chama hicho wagombee urais.



Waliojitokeza ni Dk Mwele Malecela, Dk Hamis Kigwangalla na Elidephonce Bilole mwenye elimu ya darasa la saba ambao walifika Makao Makuu ya CCM kati ya saa nne asubuhi na saa saba kwa staili tofauti kwa ajili ya kuchukua fomu hizo.


Hata hivyo, Bilole (43) aliyetembea kwa miguu huku akiwa amebeba chupa mbili za maji, mfuko wa plastiki na begi dogo jeusi, hakuweza kuchukua fomu kutokana na kufika katika ofisi hizo akiwa hana Sh1 milioni za malipo.


Baadaye alifanikiwa kulipa ada hiyo na sasa amepangiwa kuchukua fomu yake leo saa 10.00 jioni.


“Nilikuwa Benki ya CRDB, nikaitwa ofisi za chama nikaona nije ili nisikilize wito, kabla ya kuchukua fedha kwanza,” alisema Bilole aliyefika peke yake kwenye ofisi hizo.


Bilole alisema anajua Mungu atamwezesha kukabiliana na watu wengine walioomba ridhaa ya chama kuwania nafasi hiyo.


Alipoulizwa sababu ya kufika pekee yake katika ofisi hizo, alisema hajawahi kuwa na makundi ambayo yameonekana kwa makada wengine... “Nadhani naweza ndiyo maana nimejitokeza kuwania nafasi hii. Nitawavusha kuwapeleka kwenye nchi ya ahadi,” alisema na kuongeza kuwa alijiunga na chama hicho mwaka 2003 huku akiahidi kuhakikisha anainua uchumi wa nchi kwa kutumia rasilimali zilizopo.


Bilole ni nani?
Bilole alizaliwa Januari 21, 1971 katika Kijiji cha Mtala wilayani Kasulu mkoani Kigoma na anajishughulisha na kilimo.


Dk Kigwangalla ataja vipaumbele vyake
Baada ya kuchukua fomu hizo, Dk Kigwangalla alieleza vipaumbele vitatu alivyosema atavitekeleza. Aliyataja mambo hayo kuwa ni kupunguza wigo wa walio nacho na wasionacho, kukabiliana kisayansi na mabadiliko ya tabianchi katika uchumi na kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.


“Tanzania ya leo haiwezi kuendelea kwa fikra zilezile, watu walewale… tunalia na amani, umoja na upendo, lakini bado kuna haja ya kuwa na mabadiliko. Lazima tufikiri upya, lazima kuwa na mustakabali mpya wa Taifa la Tanzania,” alisema Dk Kigwangalla.


Nitashughulikia afya, elimu na uchumi - Dk Malecela
Dk Malecela ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), alisema ameamua kuchukua fomu baada ya kujitathmini.


“Naona kuna maeneo ambayo ni vizuri yakatiliwa mkazo katika Ilani ya CCM. Eneo la kwanza ni upatikanaji wa huduma ya afya kwa watu wote, eneo la pili ni elimu ya ufundi ili vijana wakitoka shule wawe wabunifu na kuongeza chachu katika teknolojia na eneo la tatu linahusu uchumi,” alisema.


Kuhusu Muungano alisema: “Utaendelea kuthaminiwa na kulindwa na pale penye matatizo kwa pamoja tutajitahidi kuyafanyia kazi na hatimaye kuyatatua.”


Dk Mwele ambaye anakuwa mwanamke wa pili kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM katika nafasi hiyo baada ya Balozi Amina Salum Ali, alisema atashughulikia tatizo la rushwa kwa kubana mifumo inayotoa mianya ya uozo huo.


Dk Mwele ni nani?
Dk Mwele alizaliwa Dar es Salaam Machi 26, 1963. Alipata elimu ya msingi katika za shule za Arusha na Oysterbay jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1969 hadi 1975.


Baadaye alijiunga na elimu ya sekondari katika Shule za Zanaki, Dar es Salaam na baadaye Weruweru, Kilimanjaro kati ya mwaka 1976 hadi 1979.


Mwaka 1980 hadi 1982 alisoma kidato cha tano na cha sita katika Shule ya Sekondari ya Kilakala, Morogoro na baadaye akajiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kwa mwaka mmoja.


Alipata Shahada ya Kwanza ya Zoolojia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye Shahada ya Uzamili katika Elimu ya Wadudu kutoka Chuo Kikuu cha London, Uingereza na Shahada ya Uzamivu ya Vimelea vya Magonjwa (PhD), katika chuo hichohicho cha London.Amefanya kazi NIMR kwa miaka 27 na ana mtoto mmoja Naomi (14).MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: