
Baadhi ya wauguzi wakila kiapo cha utii na uaminifu wakati wa maadhimisho ya siku ya wauguzi iliyofanyika Zanzibar hivi karibumi.
“Wauguzi licha ya kufanya kazi katika mazingira magumu,lakini baadhi ya watu wanatuchukulia kuwa ni jeuri. Hata hivyo, tunafanya kila tuwezalo kuokoa maisha ya wagonjwa. Baadhi ya watu hutuchukulia kama jaa la kutupiwa lawama za kila aina.
Wauguzi tumezoea kutupiwa lawama kutoka kwa watu wasiothamini kazi zetu, tunaendelea kufanya kazi lengo ni kuwahudumia wagonjwa kwa uwezo wetu wote,” alisema Hawa Mahmoud muuguzi katika hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar.
Akizungumza katika mahojiano maalum wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani mjini Zanzibar hivi karibuni,Hawa alisema kuwa:
“ Wauguzi tumekuwa tunafanya kazi kubwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja.Muuguzi mmoja anahudumia wagonjwa 50 wodini kwa siku. Tunafanya kazi katika mazingira magumu, lakini hatuna posho tunazopata zaidi ya mshahara wetu,” alisema muuguzi huyo.
Hawa amekuwa akifanya kazi ya uuguzi kwa muda wa miaka 15 sasa anasema, wauguzi wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii lakini ukweli ni kwamba wao miongoni mwa wataalamu wasio na bahati kwa jamii na kutafsiriwa kuwa ni jeuri wasiopenda wagonjwa huku maslahi yao ni si ya kuvutia.
Anasema kuwa, wana kazi kubwa pengine kuliko hata daktari kwa sababu daktari akishamfanyia vipimo mgonjwa kazi zilizobaki zinatekelezwa na muuguzi.
Wauguzi wa Zanzibar hivi karibuni, wameadhimisha siku yao katika namna ambayo ni kama wanahisi kutengwa.
Maadhimisho hayo yalipambwa kwa nyimbo, kusomwa risala kutoka kwa wauguzi ukiwa ni mwendelezo wa ujumbe unaotolewa kwa takriban miaka mitano sasa ukigusia ukosefu wa posho ya mazingira magumu, mishahara duni, kuelemewa wagonjwa na kukosekana kwa baadhi ya vitendea kazi.
Sherehe hizo za wauguzi hapa Zanzibar kwa muda wa miaka mitatu sasa, hazipati mgeni rasmi wanayemtarajia ili asikilize changamoto zinazowakabili. Mwaka huu walimualika mke wa Rais wa Zanzibar, Mwanamwema Shein ambaye hakuhudhuria badala yake aliwakilishwa na Naibu Waziri wa Habari, Bihindi Hamad Khamis.
Miongoni mwa majukumu ya muuguzi ni kuhakikisha anamhudumia mgonjwa kwa kumpa dawa, chakula, kumsafisha na huduma nyingine muhimu.
“Wakati mwingine, unawahudumia wagonjwa hadi unachanganyikiwa…. wodi zina waguzi wawili, lakini kuna wagonjwa zaidi ya mia moja wanaosubiri huduma,”alifafanua Hawa.
Ugumu wa mazingira anayofanyia kazi muuguzi, wakati mwingine huonekana kama ni jeuri kwa sababu ya uchovu kazi zao kutokana na uzito wake huku baadhi ya wagonjwa au familia ya mgonjwa hawawathamini kwa kiwango cha kuwakatisha tamaa watendaji.
Hawa alisema, kama kuna wauguzi wenye hulka ya jeuri hao ni wachache, lakini wengi wao wana huruma na nidhamu ya kazi ya kuwahudumia wagonjwa.
Raifa Simai muuguzi katika hospitali hiyo amekuwa akiifanya kazi hiyo kwa muda wa miaka 10 sasa, anasema nyakati nyingine amekuwa akifanya kazi katika mazingira magumu kwa kukosa baadhi ya vitendea kazi.
Upungufu huo, wa vifaa tiba na dawa anasema, umekuwa ukiwawia vigumu katika utendaji wa kazi zake, lakini amekuwa akijitahidi kufanya kazi kadri inavyowezekana.
Kutokana na uhaba wa wauguzi katika hospitali hiyo, wamekuwa wakijitolea kufanya kazi hata muda wa ziada bila ya malipo.
“Tukiadhimisha siku hii ya wauguzi, bado tunakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinapaswa kutatuliwa,”alisema.
Kuhusu baadhi ya familia za wagonjwa wanaofikishwa hospitalini kutibiwa, anasema kuwa huwa hawaridhiki na huduma wanazopata wagonjwa wao na kuishia kutoa lawama
“Wakati mwengine familia za wagonjwa wanaolazwa hapa muda wa kuwaangalia wagonjwa ukiisha na kuwaambia waondoke huwa wanagoma, hasa nyakati za usiku.Wanataka kubaki na wagonjwa wao, ili wawahudumie maana kazi ya kuwahudumia wagonjwa ni yetu wauguzi, lakini huwa tunaelemewa na kazi nyingi hata kusababisha huduma nyingine tushindwe kuwahudumia ikiwemo kuwapa chakula,”alisema.
Kumhudumia mgonjwa ni pamoja na kumbembeleza ale chakula, ahimizwe kunywa dawa, lakini baadhi ya kazi zinatushinda kutokana na uchache wetu muuguzi mmoja anahudumia wagonjwa 50 wanaosubiri huduma zake.
“Wauguzi tupo wachache, hata hivyo tunahakikisha tunatimiza wajibu wetu wa kuwahudumia na kuokoa maisha ya wagonjwa tunaowahudumia kadri tunavyoweza,”alisema.
Muuguzi Mkuu wa hospitali ya Mnazi Mmoja Margaret Sylvester Tayari, akizungumzia malalamiko ya wauguzi, alikiri kuwa ni kweli wanafanya kazi katika mazingira magumu, lakini kwa kuwa kazi ya uuguzi ni wito wanaendelea kujitolea kwa moyo mmoja.
Aliwataka wauguzi wote nchini wasivunjike moyo, hivyo waendelee kuwahudumia wagonjwa kwa imani kuwa malipo halali ya kazi zao watayapata kwa Mungu.
Muuguzi mmoja alifahamisha kuwa, anatakiwa kwa wastaan kuwahudumia wagonjwa watano, lakini kutokana na uchache wa wauguzi na wingi wa wagonjwa katika hospitali hiyo wanajikuta wanalazimika muuguzi mmoja kuwahudumia wagojwa kati ya 50 hadi 60 kwa siku.
Alisema baadhi ya wanajamii wana mtazamo hasi kwa wauguzi na kuwaona kama ni makatili wasiopenda wagonjwa jambo ambalo sio kweli.
Kimsingi, aliwashauri wauguzi wasijali lawama wazotupiwa na baadhi ya watu waelewe kuwa wauguzi ni chachu ya mabadiliko, hivyo waendelee kufanyakazi kwa bidii na wasijali lawama na wazichukulie kuwa ni kama changamoto kwao.
Aliitaka jamii itambue kuwa wauguzi ni binadamu kama wengineo, wana upendo na imani katika mioyo yao, hivyo wawape ushirikiano na wanapopeleka wagonjwa hospitali wazingatie taratibu zilizowekwa.
“Kuna baadhi ya familia za wagonjwa ni wakaidi ukiwaambia muda wa kuangalia wagonjwa umekwisha au mgonjwa anapatiwa matibabu ondokeni hawataki wanalazimisha wakae ili waendelee kumuona mgonjwa wao”alisema.
Alisema wakati umefika changamoto zinazowakabili wauguzi zitatuliwe ili afya bora iwe kwa watu wote, kwa sababu mazingira ya kazi yakiwa mazuri kwa wauguzi afya itakuwa bora kwa kila mtu.
Pia ni muhimu kuwepo kwa uwiano wa mishahara kati ya madaktari na wauguzi kutokana na kiwango cha elimu.
Hospitali ya rufaa ya Mnazi Mmoja inajumuisha hospitali ya wazazi Muembe Ladu na hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongo Chekundu ina wauguzi 278 na inahudumia wagonjwa zaidi ya elfu 10.
Katibu Mkuu, Wizara ya Afya Zanzibar, Muhammed Saleh Jidawi alisema kuwa, serikali itaendelea kuzifanyia kazi changamoto za wauguzi kadri uwezo wa kifedha unavyoruhusu.
Alisema wanafahamu uchache wa wauguzi, kwa sababu linatokana na nafasi za ajira zinazotolewa na Idara ya Utumishi.
“Wizara ya Afya tumekuwa tukijitahidi kila uwezo unaporuhusu kuwaondolea changamoto wafanyakazi wa wizara hii,”alisema Jidawi.
Maadhimisho ya Sikukuu ya Wauguzi hufanyika Mei 12 kila mwaka ikiwa ni kumkumbuka muanzilishi wa fani ya uuguzi duniani Florence Nightngale aliyezaliwa mwaka 1820 na kufariki 1910 . Alifanya kazi katika mazingira magumu lakini hakukata tamaa.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:
Post a Comment