WAFANYA BIASHARA WA MADAWA YA KULEVYA WABUNI BINU MPYA ZA KUSAFIRISHWA WAKITUMIA SIMU NA CHAJA KUINGIZA TANZANIA.
Dar es Salaam. Usafirishaji na utumuaji dawa za kulevya unapigwa vita kila kona ya dunia. Lakini magenge ya watu wanaozalisha na kusafirisha dawa hizo wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kufanikisha biashara hiyo haramu.
Hali hiyo inazilazimisha mamlaka za kiusalama katika mataifa nazo kuumiza vichwa ili kutafuta mbinu za kung’amua, kukamata na kudhibiti usafirishwaji wa dawa za kulevya ambao hunufaisha matajiri wachache, huku kundi kubwa la wananchi hasa vijana likiteketea.
Tanzania ni moja ya mataifa ambayo yanapambana na uingizaji, usafirishwaji na utumuaji dawa za kulevya kupitia Kikosi Maalumu cha Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya, chini ya Jeshi la Polisi katika Wizara ya Mambo ya Ndani.
Katika mahojiano na gazeti hili, mkuu wa kikosi hicho, Godfrey Nzowa anaeleza kuwa ingawa waingizaji na wasafirishaji wa dawa za kulevya wamekuwa mstari wa mbele katika kubuni mbinu mpya ili kuhakikisha wanafanikisha uingizaji dawa za kulevya nchini kikosi chake hakitarudi nyuma kupambana na uhalifu huo akiongeza kwamba wamebaini mbinu zote za wahalifu hao.
Polisi wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya wakifungua dawa zilizokamatwa jana kwenye jahazi liitwalo Kunarak-Iran lililokutwa katika Bahari ya Hindi eneo la Tanzania likiwa na kilo 201 za heroini, pamoja na raia wanane wa Iran na Wapakistan wanne. Picha na Michael Jamson
Anasema, awali, ilizoeleka watu hao kutumia njia kadhaa ikiwamo kumeza kete au kuhifadhi kwenye mabegi ya nguo, lakini sasa njia hizo hutumika mara chache, badala yake wamebuni mbinu nyingine.
Anataja baadhi ya mbinu hizo ‘mpya’ kuwa ni pamoja na kutumia simu za mkononi na ‘chaja’ zake kuhifadhia dawa, hivyo kuwa vigumu kuwabaini.
“Wanazifungua simu na kutoa mashine za ndani kisha kupakia dawa za kulevya, mtu wa kawaida akaziona ni simu na ni vigumu kujua ndani kumewekwa nini,” anasema Kamanda Nzowa na kuongeza:
“Pia huchukua betri za simu na kuziharibu kisha kujaza dawa hizo kwenye ujazo sawa na betri kisha kuzifunga upya kama betri halisi, mbinu hizo tumezibaini.”
Nzowa anataja mbinu nyingine walizobaini: “Wengine wanachukua viazi mbatata bandia na kuweka dawa za kulevya, kisha huzichanganya na viazi halisi.”
Mbinu nyingine ni dawa hizo kuchanganywa na gundi ya maji. Gundi hiyo ikisafirishwa salama hadi eneo husika basi hufunguliwa na kutenganishwa na dawa hizo.
“Siyo hizo tu, wanatumia hata marumaru za kusakafia kusafirisha dawa za kulevya. Dawa hizo zinawekwa katikati ya vigae vilivyopangwa kitaalamu. Mara nyingi mizigo yao huisafirisha kupitia njia ya maji (bahari) kwa sababu huko ndiko mizigo hubebwa kwa wingi tofauti na njia ya anga.
Hawa jamaa hawana tofauti na wale wanaosafirisha bangi kutoka Arusha kuja Dar es Salaam, juu yake wanaweka kabeji huku chini wakiweka dawa hizo.Mtu mwingine anaagiza magari kadhaa, lakini kati ya magari hayo, moja anahifadhi dawa hizo katika sehemu ya ‘waterpump’ (pampu ya maji ya gari husika) au ‘power window’ za bandia ambazo zikifika hung’olewa na kubakia zile halisi.”
Anafafanua kuwa licha ya wasafirishaji kutumia mbinu hizo, kikosi chake kipo imara kupambana na suala hilo, ndiyo maana katika kipindi cha kuanzia Mei mwaka jana, hadi Mei mwaka huu, wamefanikiwa kuwakamatawa watuhumiwa 44.
Anasema kuwa kati ya watuhumiwa hao, 21 ni raia wa kigeni na 23 ni Watanzania, kati yao wanawake wakiwa sita.
Nzowa anaeleza kuwa watuhumiwa hao walikamatwa sehemu tofauti ikiwamo bandarini na viwanja vya ndege.
“Wao wanatumia mbinu hizo mpya na sisi tuna vifaa vya kisasa vya kuwabaini kama wamebeba dawa hizo. Hawa 44, wote walifikishwa mahakamani na baadhi yao walikutwa na kiasi kikubwa cha dawa za kulevya,” anasema Kamanda Nzowa.
Taarifa pia zinaonyesha kuwa, mbinu nyingine zinatotumika kusafirishia dawa hizo ni kuzishonea kwenye mikanda ya suruali au kwenye mabegi na ya hivi karibuni ni kuzilowanisha dawa hizo kwa maji na kuzifyonza kwa taulo ambalo hukaushwa na kusafirishwa, kabla ya kukusanywa upya baada ya kupenya kwa kulikung’uta.
Soko la dawa hizo
Kamanda Nzowa anabainisha kuwa kiwango kikubwa cha dawa hizo kinachoingizwa nchini, huwa safarini kupelekwa Afrika Kusini kuliko na soko kubwa.
Anataja maeneo mengine ambayo pia ni soko kubwa la dawa za kulevya kuwa ni China katika mji wa Hong Kong na Bara la Ulaya na Amerika, huku akisema Tanzania inafanywa kama njia za kupitisha dawa hizo.
“Mfano mtu anatoka Karachi, Pakistan ambako dawa hizi zinatoka, hawezi kwenda moja kwa moja Afrika ya Kusini, lazima atabainika kwa sababu hati yake ya kusafiria inaonyesha anatoka sehemu ya chanzo ndiyo maana wanachepuka na kuja hapa nchini. Mara nyingi dawa aina ya heroin ndiyo inayopitishwa nchini kwa sababu usafirishaji wake ni rahisi hasa katika njia za majini. Cocaine inapitishwa zaidi magharibi mwa Afrika.
Kwa nini zinapita Tanzania?
Kamanda Nzowa anaeleza kuwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya pia wapo makini katika kuangilia nchi zinazalisha zao gani kwa wingi kama la biashara duniani.
“Mfano hapa Tanzania tunalima sana kahawa kama zao la bisahara, hivyo hizi dawa zikija zinafanyiwa utaalamu wa kuchanganywa na zao hilo. Njia hiyo inakuwa rahisi kupeleka nchi husika kwa kigezo kuwa ni kahawa inayosafirishwa,” anasema Kamanda Nzowa.
Ugumu wa kuzikamata
Akizungumzia changamoto katika kupambana na wasafirishaji wa dawa hizo Kamanda Nzowa anataja uwepo wa mipaka mipana kati ya Tanzania na nchi nyingine akisema hali hiyo inayosababisha kuwapo kwa ugumu wa hapa na pale kuwabaini wahusika wakuu.
“Mipaka yetu ni mipana, unaweza kusema ninalinda hapa, kumbe kule kwingine wajanja wanapishitisha dawa kama kawaida. Kingine, baadhi yao wanasafirisha malighafi za kutengenezea dawa za kulevya,” anasema Kamanda Nzowa na kuongeza:
“Hizo malighafi zinatumika kutengeneza dawa hizo na zikipita kwenye mashine za ukaguzi inakuwa vigumu kubainika, kikubwa kinachotusaidia katika vita hiyo ni kuwa na taarifa na kiintelejensia.”
Vigogo wa dawa za kulevya
Alipoulizwa kama kuna ukweli wa uwepo wa watu wanaotajwa kuwa ‘vigogo’ walio nyuma ya biashara hiyo, Nzowa anaeleza:
“Vigogo kwa tafsiri ya dawa za kulevya ni wale wanaoagiza dawa hizo kuanzia zaidi ya kilo 200 na kuzisambaza sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi. Katika lugha ya kwetu, hawa tunawaita vigogo. Baadhi yao tulishawakamata miaka ya nyuma na bado wengine tunaendelea kuwatafuta.
Vigogo siyo wanasiasa au viongozi wa Serikali kama watu wanavyodhani.”
Anafafanua: “Vilevile vigogo ni watu ambao wanakuwa na mtandao karibu dunia nzima katika biashara hii na ukifuatilia historia zao, utabaini walianza kufanya kazi hiyo kwa kumeza kete kabla ya kuacha na kuwa waagizaji wakubwa.”
Siri ya mafanikio
Kuhusu mafanikio ya kikosi chake Kamanda Nzowa anaweka wazi siri ya mafanikio katika kupambana na suala hilo ni kuwa na uhusiano na mawasilino bora kutoka kwenye nchi zinazodaiwa kutengeneza dawa hizo na zile zinazopelekewa mzigo.
“Sasa hivi mtu akisemekana kabeba mzigo kutoka nchi yoyote kupitia hapa nchini, sisi tunapata taarifa kutoka nchi husika na kuwakamatawa, iwe majini au nchi kavu,” anasema Nzowa.
Mikakati ya kikosi
Kiongozi huyo anasema kwamba kikosi chake hakitarudi nyuma katika kupambana na wote watakaobainika kufanya biashara hiyo haramu na sheria itachukua mkondo wake. Anaeleza kuwa kwa kuzingatia jukumu walilonalo, imewapeleka vijana kadhaa nje ya nchi kwa ajili ya semina na mafunzo zaidi ya jinsi ya kupambana mbinu mbalimbali za kuzuia dawa hizo.
“Katika mafunzo hayo yanayowashirikisha vijana kutoka nchi mbalimbali, pia Watanzania wanapata fursa ya kubadilishana mawazo na nchi nyingine zinavyofanikiwa kuzuia dawa za kulevya,” anasema.
Kutishiwa maisha
Anasema katika kutekeleza kazi yake ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya hukumbana na vitisho kutoka kwa watu mbalimbali, lakini anaeleza kuwa kamwe hatorudi nyuma katika kutimiza wajibu wake.
“Siku zote ninamwamini Mungu katika kazi hii. Misukosuko haikosekani, hebu fikiria unakamata mzigo wa thamani ya Sh200 milioni, hivi huyu mhusika atakuchukuliaje wewe? Lakini wakae wakijua mimi sitishiki na vitisho vyao na havitanirudisha nyuma kamwe. Havina nafasi kwangu kwa sababu nimemtanguliza Mungu.”
Wito
Anawaasa Watanzania kutambua kwamba kila mmoja ana jukumu la kupiga vita dawa za kulevya. Anasema kufanya hivyo kutaongeza kasi ya mapambano na hatimaye kuwakamata vigogo wote wa biashara hiyo. Anawashauri vijana kutojiingiza katika biashara hiyo na kwamba sasa kuna mtandao mpana unaosaidia kupata taarifa za wahusika kuanzia mwanzo hadi mwisho wa harakati zao.
“Vijana msithubutu kujiunga katika harakati hizi, mfano mzuri ukitoka katika mji wa Karrach na dawa za kulevya basi ujue taarifa zako zipo mezani kwangu na tutakunasa popote pale, labda uende nchi nyingine,” anasisitiza Kamanda Nzowa.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment