Askari wa Bunge wakimtoa nje mbunge wa Nyamagana Ezekia Wenje, baada ya kumsimamisha kushiriki vikao vya Bunge vilivyobaki, kutokana na kutoheshimu mamlaka ya Spika. Picha na Emmanuel Herman
Dar/Dodoma. Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano ambalo uhai wake unaisha Julai 9, linaonekana dhahiri kwenda mrama baada ya wabunge 23 kumlazimisha Spika kuwatimua kikaoni wakipinga kuwasilishwa kwa miswada mitatu kwa hati ya dharura.
Kwa siku tatu mfululizo, Spika Anne Makinda amekuwa akipata shida kuendesha chombo hicho cha kutunga sheria kutokana na mbinu waliyogundua wapinzani ya kupiga kelele kukwamisha shughuli za Bunge.
Juzi, kiongozi huyo wa Bunge aliamua kuwapeleka wabunge 11 mbele ya Kamati ya Maadili kwa makosa ya kudharau kiti chake na chombo hicho kikaibuka na adhabu ya kuwafungia wabunge wanne kutohudhuria vikao vyote vilivyosalia, wengine wawili kufungiwa vikao viwili.
Jana, hali iliendelea kuwa ya mapambano baada ya wabunge hao kuhoji uhalali wa adhabu hiyo, huku wakihoji sababu ya miswada hiyo kuwasilishwa kwa dharura.
Ezekia Wenje, mbunge wa Nyamagana, aliendelea kubishana na Spika na kusababisha atangaze kumzuia kushiriki vikao vitano, uamuzi uliosababisha wabunge wengine wa upinzani kusimama na kupiga kelele wakitaka nao waadhibiwe.
Spika Makinda alisema kuwa ametumia kanuni ya 74(i) kuwatimua wabunge hao kwa kushindwa kuheshimu kiti kwa kupiga kelele.
Wakati wabunge waliopewa adhabu wakiongezeka, wenzao ambao hawakuwapo sasa wamehamasishwa kwenda mjini Dodoma kuendelea na walichokiita mapambano, hali inayoweza kusababisha Bunge hilo likavunjwa likiwa limepukutika wabunge wa upinzani.
Sakata lilivyoanza
Kabla ya kikao kuanza jana asubuhi, Wenje aliomba mwongozo wa Spika na baada ya kupewa nafasi, alipinga adhabu waliyopewa wabunge saba juzi akisema wameonewa na kuhoji sababu za mbunge wa Mbozi, David Silinde kuzuiwa kuingia wakati hakutajwa kwenye taarifa ya Kamati ya Maadili iliyopendekeza adhabu hizo juzi.
Hata hivyo, Spika Makinda alimjibu kuwa hilo lilitokana na makosa ya uchapaji, lakini Silinde alimtaja na ni miongoni mwa waliokuwa wakifanya vurugu juzi na aliitwa kuhojiwa kwenye maadili.
Wenje aliendelea kupinga huku akibishana na Spika, ndipo zogo likaibuka upya na Spika akaagiza atolewe nje ya Ukumbi wa Bunge na asihudhurie vikao vitano kuanzia jana.
Baada kufukuzwa Wenje, wabunge wa upinzani na walisimama wote huku wakipiga kelele.
Kila mmoja alikuwa alipaza sauti akisema“tutoe wote, tutoe wote”, na ndipo Spika aliposema: “Haya ondokeni…ondokeni.”
Hali iliendelea kuchafuka baada ya taarifa na maombi ya miongozo kuzidi kumiminika kutoka kwa wabunge wa upinzani.
Mbunge wa Chakechake, Mussa Kombo aliomba mwongozo na katika moja ya maelezo yake, alimwambia Spika anaongoza Bunge kama vita.
“Kombo (Mussa), nilidhani unajiheshima kumbe huna heshima kabisa. Wenje namtoa nje na kwa mujibu wa kifungu cha 75, hatahudhuria vikao vitano vya Bunge, na ninyi wengine mkitaka tokeni,” alisema Makinda aliyesema pia kuwa posho zao zitakatwa.
Baada ya Wenje kutoka, wabunge walisimama na kupiga kelele tena na wakati huo tayari Spika alishamwita Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene aanze kusoma muswada, lakini kelele hizo zilifunika sauti yake.
Ndipo Spika akawaambia: “Haya simameni wote hivyo hivyo niwaandike majina.”
Baada ya makatibu kuandika ndipo makinda alipotoa tamko la kuwasimamisha kuhudhuria vikao vitano.
“Kwa mujibu wa kanuni ya 74 (1), Spika anaweza kutaja majina ya wabunge waliopiga kelele ndani ya bunge na ataomba majina hayo yawasilishwe kwenye kamati ya uongozi, sasa naomba kuwataja wafuatao,” alisema Spika.
Aliwataja waliotolewa jana kuwa ni Mussa Kombo, Masoud Abdallah, Rebeca Mngodo, Sabrina Sungura, Said Khatib Haji, Gervas Mbasa, Anna Mary Komu, Profesa Kulikoyela Kahigi, Pauline Gekul, Mariam Msabaha, Joyce Mukya, Cesilia Pareso na Grace Kiwelu.
Wengine ni Mchungaji Israel Natse, Mustapha Akonay, Conchesta Rwamlaza, Seleman Bungala, Rashidi Ali Abdallah, Hamad Ali Hamad, Riziki Juma, Asa Hamad na Salum Khalifan Barwan.
Spika alisema wabunge hao watafikishwa mbele ya Kamati ya Maadili, lakini akiwa anamalizia akageuza kauli yake na kusema wamezuiwa kushiriki vikao vitano.
Baada ya kutangaza adhabu hiyo, Spika Makinda alitangaza kuahirisha kikao cha Bunge, na tangazo lake likapokewa kwa kelele za shangwe kutoka kwa wabunge hao wa vyama vya upinzani waliokuwa hawajatoka ukumbini.
Hali hiyo ilimfanya kiongozi huyo wa chombo cha kutunga sheria, kubatilisha tena uamuzi wake na kuwataka wabunge hao kuondoka kwanza na baadaye kumpa nafasi Simbachawene kuendelea kuwasilisha muswada.
Walipotoka wabunge hao, Waziri Simbachawene alianza kusoma Muswada Sheria ya Petroli na Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Uchimbaji wakati Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba aliwasilisha Muswada wa Sheria ya Usimamizi Mapato ya Mafuta na Gesi yote ya 2015.
Sehemu kubwa ya mjadala wa miswada hiyo ilikuwa ni kumsifu Spika Makinda kwa kile walichokiita kuwa ni uvumilivu na kulaani kitendo cha wabunge wa vyama vya upinzani.
Wengine wapanga vurugu
Habari ambazo Mwananchi ilizipata baadaye jana, zilidai kuwa baadhi ya wabunge wa upinzani ambao hawakuwapo bungeni, nao wamepanga kuendeleza mapambano hayo Jumatatu kwa kutumia staili hiyo ya kusimama na kupinga uamuzi huo ili na wao wafukuzwe.
Waliofukuzwa wanena
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) Tundu Lissu alisema kuwa uongozi wa Bunge umekuwa ukibadilisha ratiba mara kwa mara ilimradi tu miswada hiyo ipitishwe kwa lazima.
Masoud Abdallah Salim (Mtambile) alisema hukumu yao ilikuwa ya uonevu na haikuzingatia kanuni za Bunge, bali iliegemea upande mmoja wa Serikali.
Akizungumzia hali hiyo, Christowaja Mtinda (viti maalum), alisema wananchi wanatambua kila kinachoendelea mjini Dodoma na hawatakuwa tayari kuunga mkono uovu wa aina hiyo.
“Hapa tumeonewa, kwani tulipaswa kupelekwa mbele ya Kamati ya Maadili, lakini tunashangaa kuona mama huyu ametoa hukumu ya moja kwa moja,” alisema mbunge wa viti maalumu, Lucy Owenya.
Mbunge wa Bukombe, Profesa Kulikoyela Kahigi alisema adhabu hiyo itawasaidia wabunge wote wa upinzani kwani muda huo tayari kila mmoja alipanga safari ya kwenda jimboni kwake.
Rebecca Mngodo (viti maalumu), alisema uamuzi waliopewa jana haukuwa katika sehemu yake kwa kuwa kiongozi (Spika) ndiye alikuwa amevunja kanuni lakini wameadhibiwa wao.
Mapema kabla ya kuanza kwa mivutano hiyo, Spika alitoa maelezo marefu kuhusu nini kilichomfanya awafukuze wabunge juzi pamoja na adhabu nyingi huku akieleza kuwa walitumia njia isiyo sahihi katika kuwasilisha maoni yao.
Ngwilizi apiga msumari
Katika hatua nyingine, mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Brigedia Generali Mstaafu Hassan Ngwillizi, alimaliza utata na kusema David Silinde amefungiwa kuhudhuria vikao vyote vilivyosalia wakati mbunge wa Rombo, Joseph Selasini na mbunge wa Donge, Khalifa Suleiman Khalifa wakipewa onyo kali baada ya kukiri na kujutia kosa.
Alisema Ali Rashid Abdallah alijumuishwa kwenye adhabu iliyokuwa imetolewa na Spika asubuhi baada ya kuhusika na vurugu na wabunge wenzie hivyo kamati isingeweza kubatilisha adhabu hiyo.
Viongozi wao walonga
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa, alisema kitendo cha kuwaadhibu wabunge hao ni uonevu kwa kuwa hawakupewa haki ya kuwakilishwa na wakili wala ya kujitetea licha ya kuwa walikuwa na nia ya kupigania masilahi ya Taifa.
“Nchi ipo pabaya, Serikali ipo kwenye hali mbaya, kinachogombewa na wabunge hao ni miswada mizito yenye masilahi mazito ya Taifa, sasa inakuwaje inaingizwa bungeni kwa hati ya dharura,” alisema.
Dk Slaa alisema iwapo miswada hiyo mitatu ingepewa muda wa kujadiliwa kama wabunge hao walivyotaka, ingekuwa na tija kubwa kwa uchumi wa sasa na kwa vizazi vijavyo.
Alimtaka Rais Kikwete kutoingia kwenye mtego wa kusaini mikataba ya wawekezaji inayohusu gesi au mafuta kwani kwa kawaida huwa imejawa na maneno matamu na baadaye kuliharibu Taifa.
Naibu katibu mkuu wa CUF- Bara, Magdalena Sakaya alisema Ukawa imebaini mbinu ya serikali kulazimisha kupitishwa kwa miswada hiyo kwa haraka akisema ni kwa masilahi yao binafsi.
“Tumegundua kuwa wanataka miswada hiyo ipitishwe kwa namna yoyote ile ili Serikali ijayo ikute imeshasainiwa,” alisema.
Alisema miswada nyeti kama ya Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi, Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji Katika Uchimbaji na Sheria ya Petroli, haikutakiwa kujadiliwa kwa haraka kwani inagusa maisha ya Watanzania moja moja kiuchumi.
Wakati huohuo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju ameomba kutengua kanuni ya 28 fasili ya 15 ili Bunge lifanye kikao leo kuanzia saa 5:00 asubuhi hadi saa 9:00 na siku ya Sabasaba kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 8:00 bila vipindi vya maswali na majibu.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment