BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

DK SLAA AMBOMOA NA KUFICHUA MAOVU YA MGOMBEA RAIS KUPITIA UKAWA EDWARD LOWASSA DAR ES SALAAM.

 
Mhe Edward Lowassa mgombe urais kupitia Ukawa.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, ambaye alikuwa mafichoni kwa zaidi ya mwezi mmoja, jana aliibuka na kuzungumza mambo mbalimbali huku akitoa hutuma zisizo na ushahidi dhidi ya watu kadhaa.
 
Dk. Slaa baada ya kutoa kauli mbalimbali katika mkutano wa waandishi wa habari, alitangaza rasmi kuachana na siasa.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya kitalii ya Serena, Dk. Slaa alisema ameamua kujing’atua katika siasa kutokana na kutoridhishwa na mambo kadhaa ndani ya Chadema ukiwamo uamuzi wa chama hicho kumpokea Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

UJIO WA LOWASSA
Dk. Slaa alikiri kuwa alihusika katika majadiliano ya kumpokea Lowassa, lakini wakati wakifanya hivyo, aliweka wazi msimamo wake juu ya namna ya kumkaribisha mwanasiasa huyo tangu hatua ya kwanza ya mazungumzo hayo.

Alisema baada ya jina la Lowassa kukatwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma kugombea urais, mtu wake wa karibu, Askofu Josephat Gwajima, alimpigia simu na kumuuliza kuwa mambo ya Dodoma yameiva nini kifuate?.

Alisema baada ya kupokea simu hiyo, alijibu kuwa asubiri hadi atakapowasiliana na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

“Nilikuwa ofisini kwangu... nikaenda ofisini kwa Mbowe na kumjulisha. Tukampigia simu askofu, akafika baada ya dakika 20, tukajadiliana,” alisema Slaa.

Alisema yeye alikuwa na msimamo wa kumsikiliza Lowassa anataka nini kwa kuwa Chadema ni chama cha siasa na hakikatai kumpokea mtu yeyote.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, baada ya kukubaliana, waliwateua vijana ili kujua wafuasi wa Lowassa wanataka kuja Chadema kufanya nini.

Alisema wakati wa majadiliano ya kumkaribisha Lowassa, yeye aliweka misingi ya kumtaka Lowassa kutangaza hadharani kuwa ameondoka chama chake CCM na kwamba, baada ya kutangaza hivyo, aseme vilevile hadharani kuwa anakwenda chama gani.

Pia, alisema alitoa masharti ya kumtaka Lowassa aitishe mkutano wa habari na kujisafisha kwa tuhuma zote zinazomkabili.

Dk. Slaa alisema misimamo hiyo yote aliyoitoa haikutekelezwa na Lowassa, badala yake alishangaa viongozi wa Chadema wanampokea.

Alisema aliweka msingi wa kumtaka Lowassa aeleze anakuja kujiunga na Chadema kama mtaji au vinginevyo na kwamba hilo swali aliliweka tangu siku ya kwanza ya vikao vya ndani vya chama chao.

“Lowassa anakuja Chadema kama Asset au Liability (mali au mzigo)... ijulikane suala siyo urais kwa kuwa sikuchukua fomu yoyote ya kugombea nafasi hiyo,” alisema Dk. Slaa ambaye kabla ya ujio wa Lowassa alikuwa akitajwatajwa kuwa atagombea urais kupitia chama hicho kama ilivyokuwa mwaka 2010.

Dk. Slaa alisema ili kujua kama ni Lowassa ni mali ama mzigo, anapimwa kwa kukidhi kigezo kuwa je, anahamia Chadema na nani? Peke yake? Na wafuasi hao ni wa aina gani? Au anakuja na viongozi serious (makini) ndani ya chama?”

Alisema jibu alilopewa ni kuwa Lowassa anakuja na wabunge wanaomaliza muda wao wasiopungua 50, wenyeviti wa mikoa wasiopungua 22 pamoja na wenyeviti 88 wa wilaya wa CCM.

Alisema alisubiri majina ya wafuasi hao wanaojiunga Chadema kwa muda mrefu, lakini hakuyapata.

Dk. Slaa alisema 25, Julai Chadema walikaa kikao na kumfuata nyumbani kwake na kumtaka kuitisha Kamati Kuu ya dharura Julai 27, kikao ambacho hatimaye alikiitisha bila kupata majibu ya Lowassa kuwa anakuja Chadema kama mali au mzigo.

Aliwataja washiriki wengine katika kikao hicho kuwa ni pamoja na Tundu Lissu, Mbowe na Askofu Gwajima kutoka saa 3:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri wakibishana kuhusu ujio wa Lowassa.

Alisema kikao hicho kilivunjika na wakaenda katika kikao cha Kamati Kuu kuanzia saa 9:00 alasiri hadi saa 12:00 jioni na kikao hicho kilivunjika kabla ya kuamuliwa kuundwa kamati ndogo ya kumshawishi Dk. Slaa akubaliane na maamuzi ya kumpokea Lowassa.

Alisema baada ya hapo aliamua kuandika barua ya kujiuzulu kwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Profesa Abdallah Safari, lakini iliishia kuchanwa.

Alisema alipoandika barua ya pili kwa makamu mweyekiti wa chama hicho Zanzibar na kumueleza kuwa anajiuzulu, alijibiwa kuwa anajisumbua bure kwani mambo hayo yalikuwa yameshapangwa.

Alisema kesho yake, picha ilitoka kwenye vyombo vya habari na viongozi wa Chadema walikanusha kuwa Lowassa hakuhudhuria kikao cha Kamati Kuu.

Dk. Slaa alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake iliyorushwa na vituo vitatu vya vya runinga takribani saa 1:15 kuwashambulia mawaziri wakuu wa zamani waliokihama CCM hivi karibuni na kujiunga katika kambi ya upinzani ambao ni Lowassa aliyeteuliwa na Chadema kugombea urais kwa tiketi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Frederick Sumaye.

Dk. Slaa alielezea mambo kadhaa yakiwamo madai kuwa aliwahi kupewa hongo ya Sh. milioni 500 na watu watatu ambao hakuwataja kwa nia ya kumfunga mdomo kuhusu kashfa ya Richmond.

Katika tuhuma hizo dhidi ya Lowassa, pia Dk. Slaa aliwataja makada wa CCM, Dk. Harrison Mwakyembe na Samuel Sitta kumsaidia katika kuueleza umma juu ya uhusika wa Lowassa katika sakata la Richmond.

Sitta alikuwa Spika wa Bunge wakati sakata la Richmond lilipoibuka bungeni na Lowasa kujiuzulu wakati Dk. Mwakyembe alikuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa na Sitta kuchunguza mkataba wa Richmond.


Alisema hivi sasa, Chadema inapokea makada walewale wa CCM waliokuwa wakiwatangaza kila uchao kuwa ni mafisadi na wengine wamepokewa kwa sifa ya kuwa ni wezi wazuri wa kura.
Alisema CCM imekuwa waoga kuchukua hatua kwa watu waliokiuka maadili akiwamo Lowassa aliyelelewa ndani ya chama hicho.

KUHUSU RICHMOND
Dk. Slaa alisisitiza kuwa mwaka 2008, Lowassa alihusika kwa asilimia zote katika suala la Richmond, lakini leo anakumbatiwa na kuitwa msafi.

Anasema yeye (Dk. Slaa) na Lowassa wana ugomvi baada ya kumwambia kuwa aeleze hadharani Richmond ni ya nani, jambo ambalo hajalitekeleza hadi sasa.

Alisema wakati kamati ya Harrison Mwakyembe inawasilisha ripoti bungeni, aliwahi kufuatwa (Dk. Slaa) na watu watatu waliotaka kumpatia rushwa ya Sh. milioni 500 ili ripoti hiyo isiingie bungeni, lakini alikataa.

Alisema suala la Richmond halikuanza katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete bali lilianza utawala wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa kutokana na dharura ya umeme.

Alisema baada ya kuingia Kikwete madarakani Februari 10, 2006, alipokea ripoti hiyo na kuiagiza kamati iendelee lakini ifuate sheria.

Alisema kipindi hicho waziri mkuu Lowassa alisimamia utekelezaji wa maauzi yote ya mkataba wa Richmond.

“Halafu leo Lowassa anakuja kutuambia kuwa hakuhusika, maana yake nini? Halafu amnawaeleza Watanzania kuwa asiye na ushahidi afunge mdomo,” alisema Dk. Slaa.

Alisema Kamati ya Mwakyembe ilitoa mapendekezo kuwa Bunge lijadili na lichukue hatua au Waziri Mkuu ajitathmini mwenyewe na achukue hatua kama anaweza kuendelea, lakini Lowassa alikimbia kwa kuwa aliona bunge lingemfukuza.

Hata hivyo, Lowassa amekaririwa akisema mara kadhaa kuwa hakuwahi kuhusika na ufisadi wowote bali kinachoelezwa ni jitihada za wapinzani wake kumchafua; na kwamba, kama kuna mtu ana ushahidi kuhusiana na madai hayo autoe hadharani.

Kadhalika, mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, David Silinde, alikaririwa juzi akisema kuwa ndani ya Chadema walimhoji Lowassa kwa zaidi ya wiki mbili na aliwaletea vielelezo kadhaa vikiwamo vya sauti kuthibitisha kuwa hakuhusika katika sakata la Richmond na ndiyo maana wakamkaribisha na kumteua kuwa mgombea wao wa urais.

KUWA LIKIZO
Kuhusu taarifa kuwa alipewa muda wa kupumzika Chadema na kuwa atakuwa na nafasi ya kurejea kuendelea na shughuli za chama wakati utakapowadia, Dk. Slaa alipinga taarifa hiyo na kusema hakuna ukweli wowote kuwa likizo na kwamba hakuwahi kupewa barua yoyote ya kwenda likizo.

Alisema ukweli wa jambo hilo ni kwamba yeye aliachana na siasa tangu Julai 28, mwaka huu baada ya kuona yale yaliyokuwa yakifanyika ndani ya chama chake hayamridhishi.

“Mimi sikuwa likizo. Mengi yalisemwa kwenye vyombo vya habari... sikuwahi kupewa barua na mtu yeyote kwenda likizo,” alisema Dk. Slaa.

KUFUNGIWA CHUMBANI NA MKEWE
Dk. Slaa alisema hakuna ukweli wowote wa yeye kufungiwa na mkewe Josephine na kwamba, maamuzi yote alikuwa akiyatoa yeye mwenyewe (Slaa) pasipo kushawishiwa na mtu. Anasema mkewe Josephine ni Mtanzania na aliwahi kukipandisha chama hicho tokea Januari 5, 2011.

Aliongeza kuwa hakuna ukweli wowote vilevile kuhusiana na madai kwamba alikuwa analipwa milioni saba kila mwezi ili kukitumikia chama hicho, bali ukweli ni kuwa mara zote alikuwa akitumia fedha zake mwenyewe na familia yake ilikuwa ikila mihogo.

“Mke wangu alizunguka nchi nzima katika harakati za ukombozi wa nchi kwa fedha zangu mwenyewe,” alisema Dk. Slaa.

AMVAA LOWASSA, SUMAYE
Alisema alitoa agizo la kumtaka Lowassa kuwaleta wabunge aliokuwa anaeleza atakuja nao Chadema, lakini wabunge hao hawakuja hadi pale walipoondolewa katika kura za maoni katika mchakato wa uteuzi ndani ya vyama.

Alisema Wwatanzania wote wanafahamu kuwa Sumaye na Lowassa hawakuwa watu safi na niliwahi kuwatuhumu mara kadhaa kwa ufisadi, huku akidai kuwa aliwahi kugombana na Sumaye baada ya kiongozi huyo kuchukua shamba la Magereza Kibaigwa na kulimiliki binafsi.

ASIYOYAFAFANUA DK. SLAA
Licha ya sehemu ya maelezo ya Dk. Slaa kueleza kwamba amekuwa akila mihogo na familia yake, hakueleza kwa kina jana ni kwa namna gani ameweza kuitisha mkutano na waandishi wa habari kwenye hoteli mojawapo ya hadhi ya juu jijini Dar es Salaam jana.

Aidha, Dk. Slaa hakueleza pia ni kwa namna gani alifanikiwa kurusha ‘live’ mazungumzo yake na waandishi wa habari jana kupitia vituo vya televisheni, tena kwa muda wa zaidi ya saa moja.CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: