BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

DK WILLBROAD SLAA AWEKEWA MIKAKATI KABAMBE YA KUMALIZWA KISIASA KUPITIA KIKOSI KAZI CHA WATU WATANO, WAPI MZEE JAMES MAPALALA ?.


ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa, ameundiwa kikosi kazi maalumu cha watu watano ili ‘kummaliza’ kisiasa, Raia Tanzania, imebaini.

Kwa mujibu wa taarifa za uhakika ambazo gazeti hili limezipata na ambazo zinathibitishwa na baadhi mawasiliano ya baruapepe, kikosi hicho kinajumuisha watalaamu mbalimbali, chini ya uratibu wa baadhi ya viongozi wa juu wa vyama vinavyounda umoja maalumu, maarufu kwa jina la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Hatua hiyo, imejitokeza mara baada ya Dk. Slaa, Jumanne ya wiki iliyopita kuzungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kueleza nini hasa kilichotokea ndani ya Chadema, kiasi cha kumlazimu kujiuzulu nafasi yake ya Katibu Mkuu na vile vile kujivua uanachama wa chama hicho.

Miongoni mwa mawasiliano ya kimkakati ambayo gazeti hili limeyanasa yanasema; “Kukiwa na a well designed damage-control and engagement strategy (mkakati shirikishi madhubuti wa kupunguza madhara), Dk. Slaa anaweza kuishia walikoishia akina Michael Nyaruba, James Mapalala, Awesu Daddi na wengineo, enzi hizo ( 1990s).”

Hatua za kuchukua
Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili imezipata zinaeleza kwamba kati ya hatua zilizopendekezwa na ambazo tayari zimeanza kufanyiwa kazi dhidi ya Dk. Slaa ni pamoja na kuunda kikosi hicho maalumu cha watu watano.

Taarifa zinabainisha zaidi kwamba kikosi hicho kinachoendesha kazi zake kimya kimya, kinahusisha wataalamu wa taaluma mbalimbali ambazo ni pamoja na zinazohusiana na masuala ya mawasiliano kwa umma, na hususan mawasiliano yanayolenga kampeni za kisiasa.

“Hawa wanapaswa kuandaa majibu dhidi ya maelezo yoyote ya Dk. Slaa, bila kujali usahihi, watafute namna ya kupotosha pale inapobidi ili hatimaye umma upoteze imani na Slaa. 


Kikosi kinaweza kushiriki vipindi vya mijadala katika redio na televisheni na wakati mwingine kupenyeza hoja zao kwa waandaaji wa vipindi hivyo, na baadaye kuendelea kumu-engage proactively (Dk. Slaa) kwa lengo la kuhakikisha anakuwa ignored na umma (political society) wa Tanzania na pengine kumfanya aonekane adui wa mabadiliko mbele ya macho ya umma (political reform public enemy).

“Kikosi-mkakati hicho kinaweza hata kufanya utafiti na ku-expose the inner motives za harakati za Dk. Slaa, zikiwamo zinazomhusu mkewe Josephine. Tunaweza kutafiti taarifa kuhusu mkewe na kuzihakiki, vyovyote itakavyokuwa, kuzianika hadharani kupitia vyombo ya habari rafiki, vinavyounga mkono Ukawa katika kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu,” yanaeleza mawasiliano yaliyonaswa na gazeti hili.

Taarifa hiyo, inazidi kuweka masharti kwa viongozi wa Chadema, hususan viongozi wakuu wa chama hicho, kwamba wasijibu chochote alichokisema (Dk. Slaa) au atakachokisema baadaye, isipokuwa kazi hiyo waache ifanywe na kikosi-mkakati cha wataalamu hao wa mawasiliano ya kampeni za kisiasa.

“Team ya Kampeni ya mgombea urais wa Ukawa ishauriwe, isijiingize kujibu chochote alichokisema au atakachokisema Dk. Slaa kuhusiana na mgombea urais wa Ukawa au wajumbe wa timu ya kampeni yake. Kama kuna suala au hoja yoyote ipelekwe katika kikosi-mkakati cha wataalamu wa mawasiliano ya kampeni za kisiasa kuandaa na hata kutoa majibu,” inaeleza sehemu ya mawasiliano hayo.

Hata hivyo, tayari hadi sasa sharti hilo la kutaka viongozi wakuu wa Ukawa kutozungumza chochote dhidi ya hoja za Dk. Slaa ni kama limepuuzwa kwa kuwa tayari wenyeviti wenza wa Ukawa, Freeman Mbowe wa Chadema na James Mbatia wa NCCR-Mageuzi, wamekwishakujitokeza hadharani kuzungumzia uamuzi wa Dk. Slaa kukutana na waandishi wa habari kufichua baadhi ya mambo ambayo anaamini hayako sawa ndani ya Ukawa, hususan namna Edward Lowassa alivyopokewa na hatimaye kupewa nafasi ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mbowe akiwa mkoani Rukwa, alisema hatua ya Dk. Slaa kujiondoa kwenye Chadema ni sawa na abiria aliyeshuka kutoka katika treni kwa kupitia dirishani wakati treni hiyo ikiwa bado haijafika mwisho wa safari, akiwa na maana bado kilele cha Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25, mwaka huu kufikiwa.

Naye Mbatia, ingawa alishindwa kujibu baadhi ya hoja muhimu za Dk. Slaa, alisema kiongozi huyo ana hasira za kukosa kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Ukawa. Miongoni mwa hoja ambazo Mbatia alishindwa kuzijibu dhidi ya Dk. Slaa ni usafi wa Lowassa kuhusu kashfa za Richmond.CHANZO:www.raiatanzania.co.tz
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: