DK WILLIBROAD SLAA APONGEZWA KWA HOTUBA YA KUMCHAMBUA MGOMBEA URAIS KUPITIA UKAWA EDWARD LOWASSA.
Dk Willbrod Slaa
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa amepongezwa kwa hotuba yake mbele ya waandishi wa habari juzi Dar es Salaam huku wanaomshambulia wakitakiwa waache na kama hawatafanya hivyo basi watajitokeza watu na kumsemea.
Katika hotuba yake aliyoitoa juzi hadharani kwa mara ya kwanza tangu atoweke Julai 28, mwaka huu baada ya Lowassa kukaribishwa ndani ya Chadema na baadaye katika umoja wa vyama vinne (Ukawa), Dk Slaa aliishukia Chadema kwa kumkaribisha ‘kiholela’ Lowassa akisema si mwanasiasa safi kimaadili.
Dk Slaa alimchambua Lowassa kuwa ni kiongozi asiyeaminika na kuwa alihusika katika kashfa ya Richmond wakati akiwa waziri mkuu miaka minane iliyopita na kusababisha kujiuzulu kwake Februari 2008.
Kufuatia hotuba hiyo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Acts of God, Askofu Pius Ikongo alimpongeza Dk Slaa kwa kuwa mkweli na kuwataka maaskofu wanaomshambulia wamuache ajibiwe na viongozi wenzake wa kisiasa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Askofu Ikongo alisema Dk Slaa amekuwa mkweli, muwazi na amethibitisha kweli kwamba alikuwa mtumishi wa Mungu na bado ni mtumishi wa Mungu.
“Tangu Dk Slaa amekaa kimya nilikuwa nasubiri sana aongee na alipozungumza nilikuwa natamani kujua atazungumzia nini ila nimefarijika sana kwa maneno yake kwa sababu angesafisha mafisadi nisingemuelewa kabisa,” alisema Askofu Ikongo.
Aliongeza: “Nampongeza sana Dk Slaa kwa kusimamia maneno yake ya kupinga ufisadi. Binafsi ningemshangaa sana kama angesimama kuwasafisha mafisadi wakati alitembea nchi nzima kupinga ufisadi.”
Alimtia moyo kwamba hiyo ni vita kati ya mafisadi na wanaochukia ufisadi na pia akamtia moyo kwa kuwa kuna baadhi ya maaskofu wamejitokeza kumshambulia wakitaka awataje kwa majina maaskofu anaodai wamepokea fedha.
“Kwa kauli za maaskofu hao wanaonesha kwamba ni watu wanaofunika uovu, kwa kuwa hata kipindi cha sakata la Escrow wapo maaskofu waliosema mimi nimetumwa kwa kutaka tuwawajibishe maaskofu waliotajwa kuchukua mgawo wa Escrow,” alieleza kiongozi huyo wa imani.
Alisema “kama wanataka Dk Slaa awataje hao wanaodaiwa kuchukua rushwa, kwanza watuambie walichukua hatua gani kwa maaskofu waliotajwa kuchukua mgao wa Escrow… Nje ya hapo haina haja ya kuwataja maana hakuna hatua ya kuchukuliwa.”
Kwa upande wake, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Kabwe Zitto, aliwataka watu wajadili hoja kwani Dk Slaa hayupo katika karatasi ya kura, na kwamba itafika mahali watatoka na kuungana na Slaa kuwasema walio kwenye karatasi hiyo.
Kwa mujibu wa Zitto, watu wanahangaika na Slaa, ingawa wengine akiwamo yeye waliamua kukaa kimya. “Kwa kuwa watu wameamua kumtukana Dk Slaa ni lazima tutoke kulinda haki yake ya kusema. Tutatoka na tutaungana na Slaa kuwasema walio kwenye Ballot. Slaa hayupo kwenye Ballot. Mwacheni. “Jadilini hoja zake sio kumjadili yeye. Eti hata watu wasio na rekodi yoyote ya kupambana na ufisadi nchi hii leo wanainua midomo yao kumsema Slaa. Mmeanza. Tutamsaidia Slaa, tutamaliza,” alisema.
Zitto alimaliza kwa kusema: “Sina mapenzi na Slaa. Alihusika kuniletea shida kubwa ya kisiasa nilipokuwa napigania misingi. Hata hivyo, naipenda zaidi Tanzania kuliko tofauti zangu na Slaa. Ni lazima aheshimiwe na alindwe.”
Naye Kada wa CCM na Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu wenye Ulemavu, Amon Mpanju, akiwa katika mkutano wa kampeni mjini Mtwara jana, alimshukuru Dk Slaa, kwa kitendo alichoita cha kishujaa na mapenzi mema kwa nchi yake, pale alipoelezea tuhuma za ufisadi za Mgombea Urais wa Chadema, Lowassa.
Mpanju ambaye ni mlemavu asiyeona, alisema Dk Slaa ameelezea ufisadi aliodai ulifanywa na mgombea huyo wa Chadema tangu alipokuwa Mbunge mpaka Waziri Mkuu.
“Ikulu si mahali pa kupeleka genge la wezi… Ni mahali pa kupeleka mtu atakayeleta maendeleo kwa wote na huyo si mwingine ni Dk John Magufuli,” alisema.
Mpanju pia alilalamikia baadhi ya vyombo vya habari na wahariri wake kwa madai ya kuonesha tabia kuwa wamenunuliwa kutokana na kutotoa uzito katika mambo ya maana yaliyozungumzwa na Dk Slaa.
Aidha, katika taarifa yao kwa vyombo ya habari jana, Chadema ilisema kuwa, “Tumemsikia Dk Slaa.”
Katika taarifa ya aya tatu iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, ilisema kuwa kwa sasa chama hicho kimeelekeza nguvu, akili na nyoyo kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu na kushinda uchaguzi huo ili kuleta mabadiliko.
“Tumemsikia Dk Slaa. Kwa sasa nguvu, akili, mioyo na miili ya wapiganaji wa Chadema imeelekezwa kwenye kampeni, kushinda uchaguzi huu kwa ajili ya kuleta mabadiliko ambayo Watanzania wanayahitaji sana, wanayaunga mkono na wako tayari kuyapigia kura hapo Oktoba 25, kwa sababu wakati wake ni huu,” ilisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia, alidai Dk Slaa amejishushia hadhi kwa kuwadanganya wananchi jambo aliloliita ni kama kuendesha siasa za mitaroni.
Mbatia alidai masuala mengi aliyoyazungumza Dk Slaa juzi ni hoja nyepesi na za uongo ikiwemo kauli kuwa hakugombea nafasi ya Urais hivi karibuni Chadema kabla ya kujiunga kwa Lowassa.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment