EDWARD LOWASSA KUJENGA BANDARI NA RELI ZA KISASA HUKU AKIIPONDA SERIKALI YA JK MKOA WA KIGOMA.
Mgombea Urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa akimnadi mgombea Ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Daniel Rumenyela wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Mwanga Community Center, mkoani Kigoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Kigoma. Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa amewaahidi wakazi wa mkoa wa Kigoma kuwa atajenga bandari ya kisasa ikiwa watamchagua kuwa rais wa awamu ya tano katika uchaguzi mkuu ujao.
Lowassa ambaye alitua mjini hapa kwa chopa akitokea Nguruka na Kalinze alikofanya mikutano ya kampeni, alisema mbali ya bandari pia atajenga reli ya kati ya kisasa (standard gauge).
Lowassa aliipiga kijembe Serikali akidai imekumbuka shuka kumekucha, baada ya hivi karibuni Waziri wa Uchukuzi, Samwel Sitta kusema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho kuanza ujenzi wa reli hiyo.
Katika mkutano huo wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Mwanga Community Centre, Lowassa alisema:
“Ninataka mnipe kura nikafanye mabadiliko ya kweli kwa kila Mtanzania. Nitahakikisha unafanyika uvuvi wa kisasa katika Ziwa Tanganyika na Bandari ya Kigoma lazima ijengwe iwe ya kisasa.”
Lowassa anayegombea urais kwa tiketi ya Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa alitumia dakika 11 kuzungumza na wananchi hao, akisema akiwa rais atahakikisha Watanzania wanajenga nyumba bora na kuwa na makazi ya kisasa.
“Tutatunga sera kuhakikisha tunaondoa nyumba za nyasi nchi nzima. Lazima tufanane na mataifa mengine, hatuwezi kubaki nyuma kila siku,” alisema.
Awali ilizuka hali ya sintofahamu katika uwanja huo kutokana na wananchi waliokuwa wamekaa nyuma ya uwanja huo kuonekana kupingana na kilichokuwa kikizungumzwa na viongozi wa Chadema kwa kunyoosha mikono juu, lakini mara baada ya Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe kupanda jukwaani na kuzungumza, hali ya kupinga ilibadilika wakaanza kuwashangilia.
Mbowe alisema kuwa lengo la Ukawa ni kuipeleka CCM likizo kutokana na kushindwa kuwaletea maendeleo wananchi. “Hatuwezi kujenga umoja kwa kutumia vyama 20, tutajenga taifa kwa kuuganisha nguvu na kushirikiana. Vyama vya mageuzi kazi yake kubwa ni kupambana na chama kilichopo madarakani.”
Mkoa wa Kigoma ni kati ya mikoa ambayo ni ngome ya vyama vya upinzani, ushindani umeongezeka zaidi baada ya aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema, Zitto Kabwe kujitosa kugombea ubunge jimbo la Kigoma Mjini kwa tiketi ya ACT-Wazalendo kupambana na kada wa zamani wa Chadema, Dk Amani Kaburou anayegombea kupitia CCM.
Lowassa alisema akichaguliwa atafuta michango na ada ya shule, kubadili mfumo mzima wa elimu ili uwe na manufaa kwa wananchi na kuwawezesha vijana kujiajiri.
Aidha, alisema ataanzisha kilimo cha umwagiliaji, kuwawezesha vijana kupata ajira, kufufua kilimo cha michikichi kwa kuanzisha viwanda vya kuzalisha mafuta ya mawese kutokana na zao hilo.
“Umeme ni kero kubwa sana, lakini nawaahidi kuwa nitalishughulikia kuhakikisha kuwa umeme unakuwa si kero tena. Kama niliweza kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika mikoa mbalimbali sitashindwa kutoa maji katika Ziwa Tanganyika kuwafikia wananchi wa Kigoma,” alisema Lowassa.
Mbunge wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi aliyemaliza muda wake, David Kafulila alisema Kigoma ni ngome ya upinzani na itadhihirika katika uchaguzi mkuu, huku akisisitiza kuwa mwaka huu ni wa mabadiliko na kwamba wanashindana na CCM isiyokubalika kokote.
“CCM imepoteza uhalali kitaifa na kimataifa na hata misaada kutoka nje haipati tena. Marekani imezuia misada ya Dola 700 milioni. Lowassa ana sababu na sifa zote za kuwa rais wa nchi hii. Ukimtizama na kumsikiliza unaona anatosha kuunganisha Waislamu na Wakristo, Watanzania na raia wa nchi nyingine,” alisema Kafulila.
Alisema Lowassa ana rekodi ambayo haina shaka na tangu ajiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008 Serikali ya Awamu ya Nne imeyumba.chanzo:MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment