Wahandisi wakila kiapo cha uadilifu jijini Dar
es Salaam jana wakati wa mkutano mkuu wa 15 wa Mwaka kwa bodi ya
makandarasi katika kuleta maendeleo ya uwekezaji nchini. Picha na Said
Khamis
Dar es Salaam. Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli amewataka wahandisi wanaofanya kazi chini ya kiwango na kudhalilisha taaluma hiyo wajiondoe mapema kwa kuwa endapo atapata ridhaa ya kushika dola hatawavumilia.
Dk Magufuli ambaye ni Waziri wa Ujenzi alisema hayo jana wakati akifunga mkutano wa wahandisi jijini Dar es Salaam. Alisema hatakubali kufanya kazi na wahandisi wanaoitia doa taaluma hiyo, hivyo ni vyema wakajitoa mapema kwani hawataendana na kasi ya utendaji wake.
Mgombea huyo wa urais alisisitiza kuwa maendeleo ya nchi yoyote duniani yamekuwa yakitegemea uwapo wa wahandisi, hivyo, endapo atashinda atahakikisha wanatumika ipasavyo kupandisha uchumi wa taifa.
“Ninawafahamu vizuri wahandisi kwa kuwa nimefanya kazi nanyi kwa muda mrefu. Niseme wazi kuwa sitawaangusha, nitakuwa nanyi bega kwa bega kuhakikisha taaluma hii inazidi kukua na kuheshimika,” alisema.
“Kama inavyofahamika kilichopo mbele yetu ni kazi, watakaokuwa tayari kufanya kazi kwa juhudi na uaminifu tutakuwa pamoja ila wale wachache wanaoitia doa taaluma hii ni bora wakajitoa mapema,” alisisitiza.
Magufuli alieleza kuwa anatambua changamoto ya utendaji wa wahandisi wilayani kuingiliwa na wanasiasa hivyo atafanya kila linalowezekana kutenganisha taaluma hiyo na siasa.
“Wahandisi wa halmashauri najua mnakutana na changamoto ya taaluma yenu kuingiliwa na siasa, hilo nitalishughulikia na nawaahidi mishahara yenu itakuwa mikubwa ila kuipata lazima mfanye kazi kubwa pia,” alisema.
“Siwezi kuwaangusha hata kidogo. Siku za nyuma nilikuwa naagizwa lakini endapo nitashinda nitakuwa natoa maagizo na nitahakikisha nitakayoagiza yanakuwa na faida kwa wahandisi na Watanzania kwa ujumla.”
Akijipigia chapuo kwa wahandisi Dk Magufuli aliwataka kumchagua rais anayeifahamu taaluma hiyo kwa kina ili washirikiane naye katika kulisukuma gurudumu la maendeleo.
Kwa upande wake, Mhandisi Ramo Makani alisema wakati umefika kwa wahandisi wa Tanzania kuongeza nguvu za ziada katika utendaji wao ili kuhakikisha wanasaidia kusukuma gurudumu la maendeleo na kuliondoa taifa kwenye umaskini.
“Tunajisikia vibaya kuona nchi yetu haiendelei na kwenye mkutano huu tumekubaliana kuacha kulalamika na kutimiza majukumu yetu kama wahandisi katika harakati za kuleta maendeleo katika taifa hili,”alisema Makani ambaye ni mbunge wa Tunduru kwa tiketi ya CCM.
Wakati Dk Magufuli akiwaahidi neema wahandisi makini, mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan alifanya ziara maeneo kadhaa wilayani Kinondoni ambako aliahidi kuchimbua mifereji na kuchimba Mto Ng’ ombe ili kuondokana na adha ya mafuriko.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Mwananyamala, Samia alisema kumekuwa na kero ya mafuriko kwa miaka mingi, hivyo Serikali ya awamu ya tano italifanyia kazi suala hilo kwa kutumia fedha ya Benki ya Dunia kuchimba mifereji yote, kuchimba mito na kuzibua njia zote za maji ili yapate njia ya kupita na yasiingie kwenye makazi ya watu.
Alisema suala la kupata maji safi na salama litakuwa la uhakika kutokana na mradi mkubwa wa maji wa Ruvu Juu ambayo yataongezeka kutoka asilimia 65 ya sasa kufikia 98. Pia, Samia aliwaahidi wakazi wa eneo la Chasimba kuwa eneo lao litapimwa na wananchi kupewa hati zao.
Samia pia aliahidi kushughulikia kero ya afya kwa kuboresha hospitali za Kawe na kuhakikisha kila kata ina hospitali na kujenga wodi mpya ya wazazi kwenye hospitali hiyo.
“Lengo langu ni kuhakikisha Watanzania wapya wakija wanapokewa katika eneo zuri; watoto wetu wachanga ni Watanzania wapya; nitaiboresha wodi ya wazazi ya hospitali ya Kawe,” alisema Samia.
Vilevile, aliahidi kuboresha soko la Makumbusho ili kuwaondolea kero ya eneo la kufanyia biashara wafanyabiashara ndogondogo. Kadhalika alisema litatengwa eneo maalumu la waendesha bodaboda badala ya kuwa vijiweni.
“Watatambuliwa kisheria na kuwaunganisha na mabenki ili iwe rahisi kukopeshwa kwani zimetengwa zaidi ya Sh10 bilioni kuwasaidia wafanyabiashara wadogowadogo,” alisema.
Ahadi nyingine zimemwagwa kwa madereva wa bodaboda na bajaji kwamba watapitia upya suala la kushindwa kufika mjini kwa kutizama mahali pa kuishia, kuzipaka rangi kwa kuzitofautisha kiwilaya ili kudhibiti uhalifu.
Kuhusu suala la bima ya afya, Samia alisisitiza kuwa watahakikisha watu wengi wanaipata ili iwapunguzie gharama za matibabu. Pia, kuhusu usafi wa jiji la Dar es Salaam alisema watahakikisha kunakuwa na magari ya kutosha ya kubeba taka.MWANANCHI
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / siasa /
slider
/ MGOMBEA URAIS AWATISHA NA KUWACHIMBIA MKWARA NZITO WAHANDISHI WA BARABARA JIJINI DAR ES SALAAM.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment