BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MGOMBEA URAIS WA CCM DK MAGUFULI AWAOMBA UKAWA KURA YA NDIO NA IMNYIME EDWARD LOWASSA.


Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli
Mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli akiwahutubia wakazi wa Manispaa ya Morogoro na vitongoji vyake katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri, jana. Picha na Juma Mtnada

Morogoro.
Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli amesema anataka kuwa rais wa Watanzania wote na kuwataka wafuasi wa kaulimbiu ya peoples inayoitikiwa power (nguvu ya umma), akimaanisha Chadema, wampe kura ili alete mabadiliko.

Katika kampeni zake, Chadema, kilichoungana na vingine vitatu kuunda Ukawa, kimekuwa kikisisitiza mabadiliko katika uchaguzi huu kwa kumchagua mgombea wake, Edward Lowassa.

“Kuna hawa watu wanatumia neno peoples halafu wanaitikia power... sasa nipeni hiyo power nifanye kazi. Uwe Chadema, CUF au ACT – Wazalendo, mimi kwangu ni kazi tu kwa maendeleo ya watu wote,” alisema na kuongeza: 


“Hivyo wale wa Chadema wanaosema ‘people’s power’ wanipe hiyo ‘power’ (nguvu) ili niwe rais wao, CUF nao huwa wanakunja ngumi wakimaanisha tano, wanipe hiyo miaka mitano nikawaletee maendeleo na wale CCM wanaonyesha dole gumba kubwa basi wanipe kura nyingi niweze kuleta mabadiliko bora, “ alisema.

Kauli hiyo ya Dk Magufuli imekuwa ikichagizwa mara kwa mara na wito kuwa maendeleo ni changamoto na hayana chama, dini wala kabila akiwataka vijana wasiharakie mabadiliko yasiyokuwa na tija.

Makamba awashukia Lowassa, Sumaye

Aliyekuwa Katibu wa CCM, Yusuph Makamba amemshukia mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowassa kuwa alikataliwa kuwa mgombea wa chama hicho tangu mwaka 1995.

Akizungumza kwa mara ya kwanza kwenye majukwaa ya kampeni mwaka huu, Makamba aliyesema alikuja kwa kazi moja tu ya kuwaelezea anavyomfahamu Lowassa alisema hakutosha kuwa rais wakati huo na hata sasa.

Akimzungumzia, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye alisema Rais Benjamin Mkapa alikuwa mvumilivu kwa kuwa alimpa wadhifa huo kwa hisani na alitumia madaraka yake kuhodhi maeneo makubwa ya ardhi.

Kabla ya mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli kupanda jukwaani, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete aliwataka wananchi kutodanganyika kwamba yupo aliyeonewa kwenye mchakato uteuzi wa chama hicho akisema hata Lowassa alipiga kura kupitisha jina la Dk Magufuli baada ya mchakato wa awali kupita.

“Tulijadiliana tukakubaliana tukatoa watu watano na Lowassa alipiga kura, Magufuli alipata kura nyingi, hata walipoingia kwenye tatu bora alipata kura zaidi ya 2,000 anakubalika anazo sifa zote na kutosha kuwa rais, nikistaafu nikamkabidhi Magufuli nakwenda kulala kwa amani,” alisema.

Dk Magufuli na mabadiliko

Akizungumza na wakazi waliofurika kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dk Magufuli alisema Tanzania ina watu milioni 50, lakini ni wachache wanaobana uchumi na kuahidi kupambana nao.

Alisema Watanzania wanataka mabadiliko ambayo yatapatikana ikiwa tu watafanya kazi kwa bidii na kuleta maendeleo.

“Hata mimi ninataka mabadiliko, ninataka kuona Watanzania wafanya kazi, siyo wanaoingia saa 2.00 asubuhi na kutoka saa 3.00 asubuhi... ninataka wananchi waishi kwa raha, mabadiliko yao wayafurahie,” alisema na kuongeza:

“Tanzania inahitaji mabadiliko siyo bora mabadiliko, nimekuwa waziri kwa miaka 20 sijawahi kufukuzwa wapo wengine wakijaribu miaka miwili tu wanafukuzwa, ninafahamu nini cha kufanya hasa katika kuwashughulikia mafisadi na wengine wameanza kukimbia. Ninaitwa Magufuli ili kuwafunga mafisadi.

“Hii inawezekana ingawa wengine wanasema inawezekana mimi nisiwe mwanasiasa mzuri mimi kwangu ni kazi, baraza la mawaziri litakuwa baraza dogo lakini hao mawaziri watakuwa hiiiiii.... watachapa kazi.”

Aliwavunja mbavu wananchi waliohudhuria mkutano huo alipotaja idadi ya mifugo mbalimbali wakiwamo mbwa na kusema idadi yao ni zaidi ya milioni 4.5, hivyo anajua mahitaji ya ardhi yaliyo makubwa katika mikoa mingi ikiwamo Morogoro ambako kuna migogoro baina ya wakulima na wafugaji.

Awali, akiwahutubia wakazi wa Ruaha, Kilosa jana Dk Magufuli aliahidi kuongeza idadi ya viwanda vya sukari akisema: “Unapokuwa na kiwanda kimoja tu cha sukari, kinaanza kujidai na kujiona chenyewe ni chenyewe, katika serikali ya Magufuli nitajenga viwanda vikubwa, vya kati na vidogovidogo.”

“Hakuna sababu miwa inalimwa hapa halafu bei ya sukari inauzwa sawa na Dar es Salaam. Kama kiwanda kiko hapa kwa nini bei ya sukari isiwe ya kiwandani? Hii ni kwa sababu sukari inatoka hapa inakwenda Dar es Salaam na tena kurudishwa hapa, kwenye serikali yangu hilo halitakuwepo, “ alisema na kushangiliwa.

Bila kuwataja majina, Dk Magufuli aliahidi kuwashughulikia vigogo wenye mashamba makubwa yasiyofanyiwa shughuli zozote za kiuchumi katika mikoa ya Morogoro na Tanga huku wananchi wakitaabika kwa kukosa ardhi.

Alipoingia Mikumi alipokewa kwa shangwe katika eneo hilo ambalo upinzani unaonekana kuimarika baada ya msanii wa muziki wa kizazi kipya, Joseph Haule ‘Profesa Jay’, kujitosa kugombea ubunge kupitia Chadema akipambana na Jonas Nkya wa CCM.

Akiwa hapo, Dk Magufuli alisema kazi yake kubwa ni kupambana na mafisadi ambao ni wachache lakini wana fedha nyingi wakati wengine hawana hata kidogo.

“Hata wakati huu wa kampeni kuna watu wameweza kununua mabasi 30 wamepata wapi fedha kama hawajaiba humuhumu serikalini? Nikipata urais nitawashughulikia wote,” alisema mgombea huyo.

Kama ilivyo ada, mgombea huyo ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, akiwa Kilosa aliahidi kujenga kwa lami Barabara ya Kilosa - Mikumi na ile ya Dumila - Handeni, Tanga ili wafanyabiashara wanaotoka Arusha kwenda Nyanda za Juu Kusini wasipitie Chalinze mkoani Pwani.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: