ASKARI WA KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI AFARIKI DUNIA BAADA YA KUGONGWA NA GARI AKIWA KAZINI
Picha ya maktaba ikimuonyesha askari wa kikosi cha usalama barabarani akiendelea na majukumu yake ya kazi.
Kibaha. Askari wa Jeshi la Polisi mkoani Pwani kituo cha Kibaha, EX.F 8471 PC Joseph Mchiwa amefariki baada ya kugongwa na gari usiku wa kuamkia jana eneo la kwa Mbonde mjini Kibaha wakati akishughulikia tukio la ajali ya basi mali ya kampuni ya Champion ililokuwa limeacha njia na kuingia kwenye mtaro uliopo eneo hilo.
Ajali hiyo ya basi ilisababisha msongamano mkubwa wa magari katika barabara kuu ya Dar es Salaam- Morogoro kwa zaidi ya saa mbili na hivyo ilimlazimu askari huyo pia kuyaongoza magari yaliyokuwa yamekwama kutokana na kuwepo foleni katika eneo hilo.
Kamanda wa Polisi Pwani, Boniveture Mushongi alisema askari huyo ambaye ni Trafiki wa Mailimoja na mkazi wa Kimara alikua zamu usiku huo na kama kawaida ilipotokea ajali ya basi la kampuni ya Champion alifika eneo la ajali kuishughulikia na wakati akitekeleza kazi hiyo ndipo saa 3:30 usiku alipogongwa na gari ingine iliyokuwa katika mwendo kasi na kufariki papo hapo.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment