KAYA 350 ZAHIFADHIWA KATIKA SHULE BAADA YA MAFURIKO KUTIKISA KILOSA.
Kilosa.Zaidi ya kaya 350 katika kijiji cha Mambegwa kata ya Msowero Wilayani Kilosa zimeifadhiwa katika shule ya msingi Mambegwa kufuatia nyumba zao kuathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Morogoro .
Waathirika wa tukio hilo la mafuriko wakizungumza na waandishi wa habari jana kijijini hapo walisema kuwa mvua hizo zilianza kunyesha tangu Aprili 19 huku zikiambatana na upepo mkali ambao uliangusha baadhi ya nyumba kijijini hapo.
Walisema mvua hizo pia zilisababisha maji kujaa ndani ya mayumba yao na kuwafanya kukosa makazi ya kudumu.
Lucy Cosmas mmoja wa waathirika wa mafuriko hayo alisema kuwa hivi sasa hawana chakula,watoto wanakabiliwa na njaa jambo linalowafanya wao kama wazazi wakishindwa la kufanya.
“Tunashindwa hata kwenda shambani na kufanya shughuli za uzalishaji kutokana na maeneo yote kujaa maji katika maeneo yote ya kijiji hiki,”alisema Cosmas.
Aidha Cosmas alitumia nafasi hiyo kuiomba serikali ya wilaya na mkoa pamoja na wadau wengine kusikia kilio chao kwani hawana pakukimbia na hapo shuleni walipo hawajui watakula nini na watoto watasoma katika mazingira gani kwani chakula walichopewa cha msaada na serikali ya wilaya kimeharibika na kingine kuchukuliwa na maji ya mvua.
Naye Jackson Mchome alisema kuwa eneo kijiji cha Mambegwa maeneo yote ambayo ni salama yamezungukwa na wawekezaji hivyo kuiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuchukua mashamba pori na kugawa kwa wananchi ili kuondokana na adha ya mafuriko wanayopata kila inapofika msimu wa mvua.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mambegwa,Said Ally alisema kuwa kaya zaidi ya 355 hazina mahali salama za pakuishi,huku mvua zikiendelea kunyesha na kukaa na serikali ya kijiji na kuwachukua wananchi kuwaweka katika shule ya msingi Mambegwa kwa usalama zaidi.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment