BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KIPIGO CHA SIMBA SC DHIDI YA TOTO AFRICAN NUSURA MWENYEKITI WAKE AKUMBANE NA KIPIGO KUTOKA KWA MASHABIKI.


Dar es Salaam. Wakati Simba ikishindwa kufurukuta mbele ya Toto Africans kwa kukubali kichapo cha bao 1-0, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya wekundu hao, Zacharia Hanspoppe amenusurika kipigo kutoka kwa mashabiki wenye hasira.

Tukio hilo lilitokea dakika chache kabla ya mchezo kumalizika, wakati Hanspoppe alipokuwa akitoka wakati huo zikiwa zimesalia dakika tano mpira kumalizika.

Baada ya kuzongwa na mashabiki waliokuwa wakiimba; ‘Tunataka timu yetu’, kiongozi huyo wa Simba alijaribu kuwatuliza kutaka wamsikilize anachotaka kuzungumza.

Hata hivyo, mashabiki hawakutaka kumsikiliza na kumzonga huku wengine wakiambizana kuanza kumpiga pamoja na viongozi wengine. Wakati mashabiki wakimbananisha Hanspope, Makamu wa Simba,Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alikuwa amekwishaondoka.

Wakati wakiendelea kuzoazana naye, mashabiki hao walimwagia mchanga ndipo akaamua kuingia kwenye gari yake. Baada ya hapo alilitoa kwa kasi bila kujali umati uliokuwa umejaa hapo ambao wote ulitawanyika.

Wakati analitoa kwa kasi, mashabiki walilirushia mawe na alipofika lango kuu alikuta foleni akageuza kurudi ndani kwa kasi huku watu wakikimbia ovyo na aligeuza kurudi lango kuu na wakati huo magari yalikwishakusogea.

Baada ya kutoka nje ya lango kuu, mashabiki walianza kulifukuza na kurusha mawe, chupa za maji kwenye gari lake huku wakisema wanalivizia kwenye foleni kuelekea Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu, Duce.

Wakati umati ukilikimbiza gari hilo, polisi wa kuzuia ghasia walifika na kuwatawanya, lakini hata hivyo mashabiki hawakusikia waliendelea kulifuatilia gari hilo huku wakirusha mawe.

Kuona hivyo, polisi walilazimika kufyatua mabomu manne ya machozi yaliyowasambaratisha mashabiki hao nje ya uzio kabla ya kuwarudia wengine waliokuwa ndani ambao waliamriwa kuondoka na walitii.

Baada ya mchezo kumalizika kabla ya kutawanywa na polisi, kulikuwa na vikundi mbalimbali vya mashabiki vilivyokuwa vikiambizana kutaka kuwapiga viongozi kwa kushindwa kusimamia timu huku wengine wakitaka timu apewe Mohamed Dewji.

Wakati hayo yakitokea kwa mashabiki, baada ya mpira kumalizika, wakiwa vyumbani, kipa wa Simba, Vincent Agban alimchapa makofi Hassan Kessy kwa kitendo chake cha kucheza rafu iliyosababisha kulimwa kadi nyekundu.

Kipa huyo alionekana mwenye ghadhabu ya kufungwa na hasira zaidi akizielekeza kwa Kessy ambaye amesababisha wacheze pungufu.

Hali ilivyokuwa uwanjani
Simba imeshindwa kurudi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kukubali kupigo cha bao 1-0 dhidi ya Toto Africans kwenye mchezo huo wa jana.

Simba walifungwa bao hilo dakika ya 20 kupitia kwa Waziri Junior kwa mkwaju wa mbali katika mchezo ambao beki wake, Hassan Kessy alizawadiwa

kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya Edward Christopher.

Kwa matokeo hayo, Simba imebaki katika nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi Kuu kwa kuwa na pointi zake 57, ikiiacha Yanga kileleni yenye pointi 57 na mchezo mmoja mkononi.

Simba ilianza kwa kasi mchezo huo na kipa wa Toto kufanya kazi ya ziada kuokoa mchomo wa Danny Lyanga dakika ya 11 ya mchezo.

Hata hivyo, Simba ambayo ilipata nafasi nyingi itajilaumu kwa kushindwa kuibuka na pointi tatu katika mchezo huo licha ya kucheza vizuri kwa muda mrefu wakiwa pungufu.

Lakini tukio hilo la kutolewa kwa Kessy lilifuatana na lile la Kocha wa Simba, Jackson Mayanja kuondolewa katika benchi la ufundi kutokana na kushindwa kuzuia hasira zake na kupinga uamuzi wa mwamuzi, Ahmada Simba wa Shinyanya.

Licha ya kuwa pungufu, Simba waliendelea kucheza vizuri lakini hawakuwa na mipango katika umaliziaji.

Kwa matokeo hayo, Toto Africans imefikisha pointi 30 na kubaki katika nafasi ya 11 kwenye msimamo.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: