WANANCHI WATAKA WAZIRI WA RAIS JOHN MAGUFULI AKAWATUMBULIA JIPU HANDENI MKOANI TANGA
Handeni. Wakazi wa vijiji vitatu vilivyopo katika Kata ya Malezi, Halmashauri ya Mji wa Handeni wamemtaka Waziri wa Maji, Gerson Lwenge kushughulikia utata wa utekelezaji wa mradi wa Bwawa la Maji la Malezi ambao haujaanza, licha ya Benki ya Dunia kutoa Sh740 milioni.
Wakizungumza na waandishi wa habari waliokuwa wanafuatilia utekelezaji wa mradi huo, wakazi hao walisema hawaoni sababu ya kutoanza kwa kuwa fedha zimekwishatolewa.
Wakazi hao hulazimika kutembea kilomita tano kufuata maji au kulala katika vyanzo vya maji vilivyopo katika eneo hilo wakisubiri huduma hiyo.
“Haturidhiki na maelezo tunayopewa,” alisema Diwani wa Kata ya Malezi, Shaaban Ramadhani.
Alisema mradi huo ulipaswa kuanzia mwaka 2008 wakati huo wakiwa chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Ramadhani alisema taarifa alizonazo zinaonyesha miaka mitatu iliyopita Benki ya Dunia iliingiza Sh400 milioni kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo, ambalo hata hivyo halijaanza kujengwa. Gharama za ujenzi wake ni Sh880 milioni.
Alisema mwaka jana Sh340 milioni ziliingizwa katika akaunti na kufanya jumla ya fedha kuwa Sh740 milioni.
Diwani huyo alielezea kushangazwa na mradi huo kuendelea kutekelezwa na halmshauri ya wilaya hiyo wakati mamlaka yake yamehamishiwa katika Halmashauri ya Mji wa Handeni.
Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Muhaji Mlaki alisema mara nyingi hupokea wataalamu wanaokwenda kuangalia eneo la mradi, lakini hakuna kinachoendelea, licha ya kuwaambia watu wenye maeneo ambayo yamechukuliwa kuacha kuyatumia.
“Tunapata lawama kwa wananchi kwa sababu tunawaelewesha hadi mwisho wanatuambia kuwa na sisi tumekuwa wanasiasa,” alisema.
Mkazi wa Malezi Kwedinguzo, Cecilia Ibrahimu alisema ametoa eneo kwa sababu maji ni kero inayowagusa watu wote.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Handeni, Mgaya Twaha alisema wanashangazwa kusuasua kwa utekelezaji wa mradi huo.
Twaha alisema mzabuni wa kwanza aliyepewa kazi hiyo alikimbia baada ya kuona eneo na baadaye kupewa mwingine ambaye naye hakufanya kazi yoyote.
“Tulimuagiza mhandisi wetu wa maji afuatilie na akaambiwa kuwa mzabuni amepatikana na amesaini kuhusu mradi huo tangu Februari 2, mwaka huu,” alisema.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya mji huo, Fabian Massawe alisema kama mamlaka mpya ya kiutawala hawajakabidhiwa mradi na hawawezi kutoa jibu sahihi la sababu zinazokwamisha kuanza utekelezaji.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment