Juma Mtanda, Morogoro.
Morogoro.Wananchi wa kijiji cha Ipera Asilia wilayani Malinyi wameuomba uongozi wa serikali ya mkoa wa Morogoro kuunda kamati maalum ya uchunguzi ili kuupatia ufumbuzi mgogoro wa wafugaji na wakulima uliosababisha kifo cha mfugaji mmoja
Ombi hilo la wananchi limekuja kufuatia migogoro ya mara kwa mara kati ya wafugaji na wakulima inayotokea kijijini hapo.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika kijiji cha Ipera Asilia wilayani Malinyi, wananchi hao walieleza kuwa wanaiomba serikali ya mkoa wa Morogoro kuwaondoa wakulima katika eneo hilo kwani ni eneo la wafugaji kwa ajili ya malisho.
Mmoja wa wananchi hao, Mipawa Chibubu Jilala (80) alisema kuwa serikali ya mkoa inapaswa sasa kuingilia kati na kuwaondoa wakulima waliovamia eneo hilo lililotengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo.
Chibubu alidai kuwa serikali ya wilaya imeshindwa kutatua mgogoro huo hivyo wanamuomba mkuu wa Mkoa kuingilia.
“Huu mgogoro mwaka jana ulisababisha mtoto wa mdogo wangu, Jilungu Ilindilo (28) kufa kwa kupigwa risasi tumboni”alisema Jilala.
Mwenyekiti wa chama wa wafugaji Tanzania tawi la Malinyi na Ulanga (CCWT) mkoa wa Morogoro, Michael Pawa, (mwenye fulana nyeupe) akizungumza na wafugaji hao katika eneo linalodaiwa kuwa ni mali ya mafugaji.
Wakulima wanaodaiwa kuvamia maeneo ya malisho kwenye kijiji cha Ipera Asilia wanadaiwa kutoka kwenye vijiji vya Kipenyo, Madibilo Chini na kufanya shughuli za kilimo katika maeneo yalitengwa kwa ajili ya ufugaji.
“Ofisi ya mkuu wa mkoa tunataka iunde tume ya uchunguzi wa kubaini mipaka ya kijiji chetu, kwa sababu umavamizi huu unasababishwa wakulima wa vijiji vya jirani kudhani eneo lililotengwa lipo wazi na halina mwenyewe. alisema Likondeni.
Akizungumzia mgogoro huo Richard Ikalango, Diwani kata ya Mtimbira, alisema kuwa mgogoro huo unatokana na ongezeko la idadi ya watu ambapo wananchi wamevuka na kuingia katika eneo hili na bahati mbaya wamekutana na wenzao (wafugaji) ambao wanamiliki hekari zaidi ya elfu tano katika eneo hilo.
Muda mrefu tumemuomba Mkuu wa Wilaya kushughulikia swala hili lakini bado Wilaya imekuwa inasuasua sana, ni vyema swala hili likashughulikiwa ili kuepusha migogoro.
Alipotakiwa kuzungumzia hatua zilizochukuliwa na Wilaya ili kutatua mgogoro huo Mkuu wa wilaya ya Ulanga na Halmashauri ya wilaya ya Malinyi, Christina Mndeme alisema kuwa hana taarifa ya uwepo wa mgogoro huo.
Mndeme alisema kuwa hana taarifa wa uwepo wa wakulima kuvamia maeneo ya wafugaji ambapo aliwataka wananchi wa kijiji cha Ipera Asilia kupeleka malalamiko yao kwenye ofisi yake aweze kutatua.
“Sina taarifa ya uwepo wa mgogoro wa ardhi baina ya wakulima na wafugaji eneo la Ikotakota kijiji cha Ipera Asilia na kama upo mgogoro viongozi wanafahamu namna ya kuwasilisha malalamiko katika ofisi yangu na nasema waje tu ili tuweze kutatua nataka amani itawale katika wilaya yangu.”alisema Mndeme.

0 comments:
Post a Comment