BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

JAKAYA KIKWETE AKILI KUWA EDWARD LOWASSA ALIVUMVUGA HASWA 2015KATIKA MCHAKATO WA KUPATA WAGOMBEA URAIS NDANI YA CCM MJINI DODOMA


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais mstaafu Jakaya Kikwete amekiri kiaina kwa mara ya kwanza kuwa kada wa zamani wa chama hicho, Edward Lowassa na watia nia wengine walimvuruga kwa kiasi kikubwa.


Wakati wa mchakato wa vikao vya kumpata mgombea wao wa urais kuelekea uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.

Akizungumza katika kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho mjini Dodoma jana, Kikwete anayetarajiwa kung’atuka leo ili kumpisha Rais John Magufuli kuongoza chama hicho, alisema wakati huo chama kiliyumba na kwamba, kilichokuwa kikimchanganya ni pamoja na watu kuwaimba baadhi ya wagombea pale alipokuwa akiongoza vikao hivyo vya mchujo.

Hata hivyo, Kikwete alisifu kuwapo kwa Baraza la Wazee linalowahusisha viongozi wastaafu, akiwamo Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, ambalo lilisaidia kwa kiasi kikubwa katika kukabili changamoto hiyo iliyotishia kukivunja chama.

Mbali na Mkapa, Baraza la Ushauri la Wazee wa CCM lililosaidia mambo kwenda sawa linaundwa pia na viongozi wengine wastaafu ambao ni Rais wa Awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Makamu wenyeviti wastaafu, John Malecela na Pius Msekwa.

Hata hivyo, katika maelezo yake hayo, Kikwete hakumtaja Lowassa moja kwa moja na wala mgombea mwingine yeyote kati ya 38 waliojitosa kwenye kinyang’anyiro hicho, akiwamo mgombea mwingine aliyekuwa na nguvu kubwa wakati wa mchakato huo, Bernard Membe.

“Na maadam CCM haikuvunjika mwaka wa jana, haivunjiki tena… maana pale ndo mafisi yalikaa, yanasubiri mkono udondoke… haukudondoka.

Na maadam haukudondoka mwaka jana, CCM haidondoki,” alisema Kikwete.

Rais Kikwete alisema hayo jana ikiwa ni mwaka mmoja tangu Julai 10 wakati Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilipoengua jina la Edward Lowassa na wagombea watia nia wengine kadhaa waliokuwa kwenye mbio za kuwania urais kupitia chama hicho.

Uamuzi huo uliibua mtikisiko mkubwa, ikiwamo baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu (CC) kutoka nje ya kikao na kufichua mbele ya waandishi wa habari kuwa hawakujadili majina ya wagombea wote 38 waliokuwa wameomba kugombea urais bali ni matano tu, jambo ambalo walidai ni kinyume cha katiba ya CCM.

Wajumbe waliopingana na uamuzi wa CC na kuzungumza hisia zao mbele ya waandishi wa habari ni aliyekuwa Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sofia Simba.

Magufuli ndiye aliyeibuka kinara katika mchakato huo wa kumpata mgombea wa CCM na mwishowe kushinda katika uchaguzi mkuu wa urais kwa asilimia 58.46 ya kura zilizopigwa.

Kufuatia kuenguliwa katika mbio za urais CCM, Lowassa alihama chama hicho na kujiunga Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambako mwishowe aliteuliwa kuwa mgombea urais wa chama hicho aliyewakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) -- vya Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na Chama cha Wananchi (CUF).

Aliweka rekodi ya kuwa mgombea wa upinzani aliyepata kura nyingi zaidi baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuonyesha kuwa alivuna zaidi ya asilimia 39 ya kura zilizopigwa.

Akieleza zaidi wakati akifungua kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho jana, Kikwete alisema kutokana na chama hicho kuyumba sana wakati wa mchakato wa kumpata mgombea wao, hali ilikuwa mbaya na jambo pekee lililowaokoa ni baraza la ushauri la wazee wa CCM walilomo kina Mkapa na sasa yeye atakuwa miongoni mwa wajumbe baada ya kukabidhi kofia ya uenyekiti kwa Rais Magufuli.

“Mwaka jana chama chetu kilikuwa kinapita kwenye misukosuko mikubwa, unaingia hapa watu wanaimba hivi, hawa wanaimba hivi… mjadala mkali. Lakini nikasema tutavuka tu maadam tupo, na ndiyo changamoto yenyewe ya uongozi.”

Alisisitiza kuwa wakati huo, wapinzani wao kisiasa walikuwa wakisubiri kwa hamu kuona CCM ikivunjika lakini hilo kamwe halikutokea na kwamba, kwa sababu hiyo, kamwe hilo halitatokea tena.

WIMBO ULIOTIKISA JULAI 10
Kufuatia kukatwa kwa jina hilo la Lowassa, kikao cha halmashauri kuu kiliingiwa na dosari baada ya wajumbe kuanza kumtaja Lowassa mfululizo kupitia wimbo uliotikisa ukumbi mzima.

Wimbo huo maarufu ni ule usemao: “tuna imani na Lowassa… oyaa, oyaa, oyaa…. Lowassa, kweelii, kwelii, kweli Lowassa.”

Wimbo huo ulishika kasi wakati mwenyekiti (Kikwete) akingia ukumbini kuendesha kikao hicho.

Kwa kawaida, katika vya aina hiyo, wakati mwenyekiti akiingia ukumbini, wajumbe huimba ‘Tuna imani na mwenyekiti (Kikwete), oyaa, oyaa, oyaa.”

AWAAGA WAJUMBE NEC
Katika hatua nyingine, Kikwete aliwaaga wajumbe wa halmashauri kuu kwa kusema kuwa hicho ni cha mwisho kwake
“Kikao kama hiki hatumwi mtoto, unakuja mwenyewe… ni kikao cha kihistoria na kikao changu cha mwisho.

Nitakuja kwenye NEC mkinialika, lakini tulikubaliana wazee wameshatumikia vya kutosha sasa tuwaache wapumzike.”
Akieleza zaidi, Kiwkete alikumbushia nafasi ya wastaafu hapo kabla na ilivyo sasa.

“Kulikuwa na utaratibu huko nyuma ukimaliza uenyekiti unakuwa mjumbe wa kudumu wa kamati kuu na halmashauri kuu. Mzee Mkapa akasema Bwana Rais na Mwenyekiti sisi tumeshamaliza kazi, mnatuita kila siku kwa nini? Sisi tulishakuwa wazee unakaa mpaka saa saba za usiku… hebu mtuacheni,” alisema Kikwete akimnukuu Mkapa.

Alisema baada ya ushauri huo, akasema hawezi kuwaacha na badala yake, ndipo alipotengeneza baraza la ushaur ili wawaite pale wanapowahitaji.

“Yakasemwa maneno mengi, nikajaribiwa lakini nikasema bwana, ni uamuzi wa msingi… maana anachosema Mzee Mkapa kwamba sisi tumeshafanya kazi, tumeendesha hivyo vikao… sasa nyie mnataka tuwe kwenye hivyo vikao tuangalie mnavyoendesha?”

“Kwa hiyo na mimi sasa kesho (leo) namaliza… kesho mwisho kabisa. Naingia na mimi kwenye baraza la wazee. Na uzuri wa baraza hili la wazee, wanapohitajika ni wakati muhimu. Kuna masuala makubwa ya chama chetu na uhai wake,” alisema.

Kikwete alisema kuwa kuna gazeti limeandika ‘CCM itaishia 2020’, lakini kamwe hilo halitatokea.

“Utake usitake, CCM itaendelea kuwapo. Siyo kwa nguvu. Ni kwa sababu tunafanya mambo ya msingi, tunatambua mahitaji ya watu, changamoto za watu, tunapanga mipango vizuri na serikali katika utekelezaji wake zimekuwa makini katika kutekeleza masuala ya watu na ndio maana hatuna tabu,” alisema.

AMTAHADHARISHA MAGUFULI
Kikwete alimtahadharisha mrithi wake kwa nafasi ya uenyekiti, Rais Magufuli, kwa kumueleza kuwa ajiandae na changamoto za kikao cha NEC kwa sababu husifia sana mambo yakienda vizuri lakini huwa wakali ikiwa kinyum chake.

“Wanasifia sana hawa mambo yakienda vizuri (wajumbe wa NEC), maana na wao wanaona fahari mambo yakienda vizuri.

Lakini yasipoenda vizuri wanakuwa wakali pia, lakini ni kwa nia njema kwa sababu wanataka mambo yafanyike vizuri.

“Naomba muendelee kumpa ushirikiano huo na msaada mwenyekiti mpya ndugu John Pombe Magufuli,” alisema.

Wakati huohuo, chanzo kimoja kiliiambia Nipashe kuwa Kikwete alimtaka Magufuli kuwa na subira kwa badhi ya maamuzi.

Alisema wakati wa uongozi wake, alikuwa akitumia muda mrefu kuchukua hatua pindi jambo linapotokea kwa sababu ya lengo hilo la kuhakikisha anachukua tahadhari.

Chanzo kimedai kuwa kwa upande wake, Magufuli mbali na kumshukuru Kikwete kwa jinsi alivyokiongoza chama hicho, alisema moja ya sababu zilizochelewesha yeye kukabidhiwa chama hadi sasa ni yeye mwenyewe aliyetaka Kikwete amalizie muda wake wa kikatiba wa kuongoza miaka mitano na kwamba.

Kikwete alitaka kumkabidhi uongozi wa chama mapema zaidi.

MAGUFULI APITA KWA KISHINDO
Akziungumza mara baada ya kumalizika kwa kikao cha NEC, Msemaji wa chama hicho, Christopher Ole Sendeka, alisema wajumbe wa kikao hicho kwa kauli moja wamempitisha Dk. Magufuli kuwa Mwenyekiti wa chama hicho na hatua iliyobaki ni Mkutano Mkuu kupiga kura.

Alisema katika mkutano huo wajumbe wawili watasimama kumuombea kura ili awe Mwenyekiti kwa kuwa yeye hakujaza fomu kuomba bali chama ndioY kimependekeza hivyo.

Alisema Magufuli anapaswa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura halali zilizopigwa na kwamba hana shaka katika hilo kwa sababu anaamini wajumbe watashawishiwa kupiga kura zote za ndiyo ili awe kiongozi wao.

Alisema kwa kazi nzuri iliyofanywa na Magufuli, hakuna sababu ya wajumbe kumnyima kura kwa sababu amesimamia uadilifu, uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa ili kurudisha misingi ya nchi. 


Sendeka alisema Magufuli ana uzoefu wa kutosha kukiongoza chama kwa kuwa amepita ngazi zote za uongozi isipokuwa ujumbe wa Kamati Kuu na Nec ambao ameupata baada ya kuwa Rais.Nipashe
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: