SERIKALI YA RAIS MAGUFULI YACHACHAMAA, YASAKA WASOMI HEWA KILA KONA KATIKA VYUO VIKUU.
Moja ya vyuo vikuu vya Tanzania.Picha ya maktaba.
WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, amesema operesheni ya uhakiki wa wanafunzi hewa wanaopatiwa mikopo imeanza kuonesha mafanikio, kwani wanafunzi hewa wameanza kubainika.
Akizungumza baada ya kufungua Maonesho ya 11 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) jana, alisema uchunguzi wa awali umebaini wanafunzi hewa 139 katika vyuo vitano vilivyofanyiwa uhakiki.
“Tunaendelea kuhakiki na tayari tumehakiki vyuo vitano ambapo wanafunzi hewa 139 walibainika kati yao wamo marehemu, walioacha shule, waliosimamishwa shule na waliohamishwa,” alisema bila kuvitaja vyuo hivyo kwa maelezo kuwa, taarifa haijawa kamili.
Aidha, alisema katika jitihada za kuboresha elimu inayotolewa nchini wizara hiyo inafanya mapitio ya Sheria ya Vyuo Vikuu ili itoe fursa kuchukulia hatua vyuo vya kitapeli. Alisema kupitia sheria hiyo, serikali itaanzisha mfumo wa kuratibu na kudhibiti uanzishwaji wa vyuo kwa lengo la kuwabana wanaoanzisha vyuo kwa lengo la utapeli.
Hivi karibuni, Rais John Magufuli aliwasimamisha kazi watendaji wakuu wa Kamisheni ya Tume vya Vyuo Vikuu (TCU) baada ya kubainika kamisheni hiyo inadahili wanafunzi wasio na sifa, wakiwemo wenye ufaulu wa daraja la nne, kujiunga na vyuo vikuu na kuwapatia mikopo.
Serikali pia ilibaini uwepo wa wanafunzi hewa wanaotafuna mikopo ya elimu ya juu, jambo lililosababisha Profesa Ndalichako kutangaza vita dhidi yao na kuanza operesheni ya uhakiki katika vyuo vyote vikuu nchini.
Aliungwa mkono na Rais John Magufuli aliyetangaza kuwa serikali yake imejipanga kumaliza makosa yote yaliyojitokeza huko nyuma, ikiwemo tatizo la watumishi na wanafunzi hewa lililoibuka hivi karibuni.
Profesa Ndalichako alianza kuchukua hatua kwa kusimamisha kazi viongozi wanne waandamizi kwa tuhuma za kudahili wanafunzi wasio na sifa.
Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya TCU, Awadh Mawenya naye alisimamishwa kazi kwa kosa la kushindwa kuwachukulia hatua watumishi waliodahili wanafunzi hao wasio na sifa.
Profesa Ndalichako alichukua hatua hizo baada ya TCU kudahili wanafunzi 489 waliopata daraja la 4.32 katika mitihani yao ya kidato cha nne lakini walijiunga na chuo kikuu na kupatiwa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 784.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment