BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

ZITTO KABWE ATAKA VYAMA VYA UPINZAJI KUJIPANGA UTAWALA WA RAIS MAGUFULI.


KIONGOZI Mkuu wa Chama cha Act-Wazalendo, Zitto Kabwe ameeleza kuwa ukali wa Mwenyekiti mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Joseph Magufuli itakuwa ni faida kubwa kwa mfumo wa vyama vingi kwa sababu upinzani wa kweli utaimarika kuliko wakati mwingine wowote.
 
Akizungumzia juu ya ujio wa Rais Magufuli CCM, Kabwe alisema kuwa kunatoa changamoto kwa upinzani sasa kujadili “hoja” ili kujiimarisha zaidi tofauti na ilivyo sasa.

“Rais Magufuli kama anaweza kutamka hadharani kuwa angewapoteza watu na tena wanachama wa chama chake cha CCM kwa kuonyesha kutokubaliana na maamuzi ya chama hicho ndani ya vikao vya chama, ni mtu hatari,” alisema Zitto, "hivyo mbinu za kushindana naye lazima ziwe tofauti.

“Huu ndiyo wakati muafaka wa kujenga mfumo madhubuti wa vyama vingi kuliko wakati nyakati zozote zile katika historia ya nchi yetu.

“Naweza kueleza viongozi wenzangu kuwa viongozi wote wa upinzani tujisomee kwanza tujue mbinu na medani, pia tuwe wavumilivu zaidi kuliko CCM kwa kuruhusu maoni tofauti kwenye vyama vyetu badala ya kuwa na tabia zile zile kama za CCM.”
 

Kabwe alisema kuwa huu ndiyo wakati wa kusambaza Azimio la Tabora linalohuisha Azimio la Arusha kwa umoja na nguvu.

Akizungumza baada ya kuchaguliwa kwa asilimia 100 ya kura halali 2,398 zilizopigwa mjini Dodoma juzi, Rais Magufuli alimsifu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Jakaya Kikwete kwa uvumilivu ambao yeye, alikiri, hana walau nusu yake.

Alisema hayo akirejea ‘uasi’ uliojitokeza katika mkutano mkuu maalumu wa CCM mwaka jana ambapo Kikwete alikaribishwa ukumbini na pambio la ‘Tuna imani na (Edward) Lowassa’.

Zitto alizungumzia pia kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (UDP), John Cheyo kwenye Mkutano
Mkuu Maalumu wa CCM uliomchagua Rais Magufuli kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho juzi kwamba upinzani kuing’oa CCM madarakani ni vigumu.

Zitto alisema hilo si jambo la ajabu kwa Cheyo kwa sababu tangu Rais Mwinyi akiwa Mwenyekiti wa CCM hadi Kikwete anakabidhi uongozi amekuwa akitoa kauli za namna hiyo.

Aidha, Zitto alisema katika historia ya dunia wanasiasa kama hao hawakosekani.

“Siwezi kushangaa Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Austino Mrema na Cheyo wa UDP, kama ni msomaji wa siasa ya dunia wala hutasumbuka maana watu ni mambo yamefanyika sana,” alisema Zitto.

Alisema pamoja na kwamba wamekuwa wenyeviti wa vyama vyao, lakini bado hawaoni soni kuisifia CCM.
RAis Magufuli alipokea kijiti cha Uenyekiti wa CCM juzi kutoka kwa Kikwete na kuwa Mwenyekiti wa tano.

Baada ya kukabidhiwa kijiti hicho, Rais Magufuli alibainisha changamoto 12 za kuakabiliana nazo katika kipindi chake cha uongozi, kwa ajili ya ustawi wa chama chake.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni uimarishaji chama, kuboresha katiba, kuondoa utitiri wa vyeo, watendaji vihiyo, rushwa, mpasuko, maslahi ya watendaji, ufisadi mali za chama, ada ya uanachama, mvuto kwa vijana, usaliti na tishio la upinzani.NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: