KANISA KATOLIKI NA WANAVIJIJI VYA MALINYI WAINGIA KATIKA MGOGORO WA ARDHI
Dk. Khaji Mponda, Mbunge wa Jimbo la Malinyi
WAKAZI wa Kaya 22 zilizopo katika Kijiji cha Munga, Tarafa ya Mtimbila wilayani Malinyi, Morogoro wameiomba Serikali ya Wilaya, Mkoa na Taifa kuingilia kati katika kutatua mgogoro wa ardhi uliopo baina yao na Kanisa Katoliki Mtimbila, anaandika Christina Haule.
Deotilia Mtolela (57) Mkazi wa Kijiji cha Munga amesema, alizaliwa katika kijiji hicho na wazazi wake ambao walihamia maeneo hayo muda mrefu huku akiwa na wakubwa zake watatu ambao wote walizaliwa hapo.
Amesema, baadaye walifika wazungu wakidai wanatoka misheni na kuomba kumegewa sehemu ya ardhi ambapo baadhi ya majirani zao waliwauzia ambapo mwaka 1963-64 walijenga baadhi ya majengo ikiwemo kanisa na kituo cha ufundi cherahani kwa ajili ya wakinamama wawata.
Hata hivyo amesema kuwa, akiwa na umri mkubwa baba yake ambaye sasa ni marehemu, Mzee Exavery Likakafu aliitwa na viongozi wa kanisa na kuombwa kuwamegea sehemu ya uwanja wake ili waingize kwenye eneo la kanisa na ndipo baba huyo alipokataa.
Hilary Chipeto, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mtimbila alipozungumza na mwandishi wa habari hii, aligoma kueleza chochote kwa madai yupo nje ya ofisi.
Geofrey Haidhuru, Paroko wa kanisa hilo Mtimbila licha ya kuonwa na waandishi katika eneo la kanisa hilo, mtumishi wa kanisa hilo alisema kwamba, ameondoka.
Dk. Haji Mponda, Mbunge wa Jimbo la Malinyi amekiri kuwepo kwa mgogoro huo wa muda mrefu ambapo amesema, wakazi hao wameishi zaidi ya mika 50 katika maeneo hayo.
Amesema, taarifa aliyonayo hadi sasa “Kanisa linayo hati miliki ya eneo hilo licha ya kuwapo kwa mgongano wa sheria na kanuni kufuatia kuwa, kama kweli wakazi hao wangekuwa wamevamia, kungekuwa na mazingira ya uvamizi.”
Dk. Mponda amesema kuwa, aliwahi kupokea malalamiko ya wananchi hao, lakini kufuatia suala hilo kukaa kisheria zaidi, aliwashauri waonane na uongozi wahusika wa masuala ya ardhi ili waweze kupata utatuzi wa tatizo hilo jambo ambalo kwa sasa linafanyiwa kazi.MWANAhalisi Online.
0 comments:
Post a Comment