Juma Mtanda, jphtjuma@gmail.com
Tanzania imekuwa na utamaduni wa kuadhimisha sherehe za wakulima tangu mwaka 1993 hadi sasa kwa kila mwaka ifikapo Augosti 1hadi 8 kwa wakulima, wafugaji, wavuvi makundi mengine kuonyesha maonyesho bidhaa ikiwemo mazao.
Maonyesho hayo yamekuwa na lengo la washirikika kupata mafunzo na fursa ya kubadilishana uzoefu wa mbinu na teknolojia mbalimbali za kuendeleza kilimo, ufugaji na uvuvi bora kutoka kwa wenzao huku taasisi za utafiti za umma na binafsi, mashirika na watu binafsi zikieneza utalaamu kwa wananchi katika maonyesho hayo.
Moja ya siri ya mtu ama kampuni kufikia mafanikio, imejificha kwa watalaamu waliobebea katika moja ya jambo lakini kwa upande wa wakulima, maonyesho ya wakulima yanayofanyika katika kanda mbalimbali hapa Tanzania yamekuwa na siri kubwa ya mafanikio.
Moja ya Siri kubwa ya mafanikio ili kufikia malengo ya utajiri ili binadamu kuishi maisha yasiyo ya kubahatisha ni lazima apitie katika jungu la uvumilivu na kupata ushauri kutoka kwa watalaamu.
Afisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika halmashauri ya wilaya ya Handeni mkoa wa Tanga, Rosemary Buge anaeleza kuwa mkulima anaweza kuondokana na umasikini na kujiongezea kipato hata kuwa tajiri endapo atashika mambo mawili na kuyafanyia kazi kwa vitendo.
Buge anaeleza kuwa ni lazima mkulima awe karibu na mtalaamu wa kilimo na umwagiliaji ili kabla ya kuanza kuanza kilimo cha kutegemea mvua za msimu wa masika au kilimo cha umwagiliaji aweze kupata mbinu za namna ya kulima.
“Mafanikio ya mkulima yapo mikononi mwa watalaamu wa kilimo ambao wapo hadi ngazi ya kata lakini ili kufikia mafanikio yatamlazimu kuwa mvumilivu na kufuata mbinu za kilimo zinatolewa na watalaamu.”alieleza Buge.
Mkulima ili kufikia mafanikio hasa kilimo cha biashara anashauri kupata ushauri kutoka kwa bwanashamba kwa kuanza kilimo na mvua za masika lengo ikiwa kutafuta mtaji wa fedha ili kuendeleza kilimo husika.
Mazao ya biashara yapo mengi yakiwemo ya kilimo cha mihogo, magimbi, viazi vitamu, migomba, miembe, michungwa na mahindi ambayo mkulima anaweza kutumia mvua za masika kulima kilimo hicho kwa lengo la kupata fedha za mtaji ili kuingia katika kilimo cha umwagiliaji.
Kilimo cha umwagiliaji kikifuatwa vizuri misingi yake kina faida kubwa kwa upande wa biashara hasa kwa kutumia umwagiliaji wa asili na umwagiliaji wa matone.aliongeza Buge.
Zipo njia nyingi za umwagiliaji ambazo zinahitaji mtaji wa fedha ili mkulima kufanikisha kilimo cha umwagiliaji katika kilimo cha kiangazi.
Njia hizo ni pamoja na umwagiliaji wa kutumia mifereji ili maji kuifikia mimea, kunyunyuzia maji kwa njia ya bomba, kunyunyuzia maji kwenye shina la mmea na njia ya kumwagilia mimea kutumia majaruba.anaeleza Frank Ngonyani.
Ngonyani ambaye ni mtaalamu wa umwagiliaji kutoka jiji la Tanga anaeleza kuwa mkulima anaweza kutumia kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya mbogamboga aina zote pamoja na matikiti, mipapai, persion, matikiti maji, matango, machungwa, migomba.
Kuna faida za umwagiliaji kwa njia ya matone kwani ukuaji wa mazao hutumia maji kidogo na kuzalisha mazao kwa wingi na njia hiyo maji kutumika kikamilifu katika mme kwa 90%.
Mambo ya kuzingatia katika kilimo cha biashara kwa bustani ambapo mkulima ataandaa kwa kutengeneza matuta marefu na kuweka mtaro kipimo cha sentimeta 15-30, kutandaza majani mabichi kwenye mtaro kiasi cha sentimeta 15 na kuweka mbole kisha kufunika kabla ya kupanda mimea.
Mwanahawa Hamis (36) mkazi wa Mkuranga kijiji cha Kiziko kata ya Mwarusembe ni mmoja wakulima wadogo waliotembelea maonyesho ya wakulima kanda ya mashariki viwanja vya Mwl Julius Nyerere yanayofanyika Morogoro kwa lengo la kujifunza.
“Nimefika katika maonyesho haya ya Nane Nane Morogoro kwa lengo la kujifunza na mimi ni mkulima wa zao la nyanya nimekuja kujifunza na nimeingiwa na tama na mazao niliyoyaona namna yalivyostahi na kutoa matunda mazuri.”alisema Mwanahawa.
Nasomesha watoto shuleni kwa kilimo cha nyanya na kimenisaidia baada ya kutengena na mume wangu ukiwa ni msimu wangu wa pili.aliongeza.
Katika msimu wake wa kwanza Mwanahawa anaeleza kuwa aliandaa shamba la robo tatu ya heka na kupata miche na baada ya mavuno aliweza kupata fedha kiasi cha sh300,000/- wakati msimu wake wa pili alipata fedha kiasi cha sh450,000-
“Msimu wangu wa kwanza nilitumia sh100,000 kama gharama za kuandaa shamba na msimu wa pili nitumia sh150,000 za gharama na nilikuwa sijatumia mtalaamu yoyote zaidi ya kulima kilimo cha mazoea.”alisema Mwanahawa.
Mwanahawa alieleza kuwa baada ya kukaa Morogoro kwa siku mbili na kuhudhuria maonyesho kwa lengo la kujifunza kilimo cha nyanya katika vipando vya mabanda vya maonyesho hayo.
“Kitu nilichodhamilia ni kushirikisha watalaamu wa kilimo wilayani kwangu ili nipate elimu ya namna ya kulima kilimo cha nyanya lakini kuongeza zao la kebiji ili kupata mavuno mengi.”alisema Mwanahawa.
Waziri mkuu, Kassim Majali wakati wa ufunguzi wa shereha za maonyesho ya wakulima kanda ya mashariki Morogoro alieleza kuwa katika maonyesho hayo amebaini waoneshaji wengi wao ni vijana na wameitikia falsafa ya rais Magufuli ya hapa kazi tu.
Majaliwa alieleza kuwa kama Taso itajikita zaidi katika mapinduzi ya kilimo cha kisasa na cha biashara kwa upana wake yapo mambo ambayo wanapaswa kuyafuata ili kufikia malengo hayo.
Alitaja malengo hayo kuwa ni matumizi ya kanuni bora za kilimo, uvuvi na ufugaji ikiwemo matumizi sahihi ya pembejeo kama mbolea, viatilifu na madawa yaliyopendekezwa na watalaamu hapa nchini.
Kulima kwa kuzingatia aina ya udongo, hali ya hewa katika kanda za mazao, kuzalisha mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuzingatia ubora wa kimataifa katika masoko, kuendeleza kilimo cha kisasa kwa kutumia zana bora na za kisasa na kuweka mifumo na taratibu nzuri za kuzimamia utekelezaji wa shughuli.
Mengine ni kuimarisha mbinu za uvunaji wa maji ya mvua na miundombinu ya umwagiliaji maji mashambani ili kuongeza eneo la uzalishaji na tija kwa mkulima pamoja na kuimarisha hifadhi ya chakula kwa matumizi ya familia, kukidhi mahitaji ya soko ndani na nje ya nchi.alisema Majaliwa.
“Wito wangu kwa wananchi kuwa muwe na tabia ya kutembelea maonyesho ya kikanda na kitaifa kwa lengo la kujifunza, kuwa tayari kuanza kutumia teknolojia na maarifa mtayoyapata ili kujiletea mapinduzi halisi katika nyanja za kilimo, ufugaaji na uvuvi.”alisema Majaliwa.
Majaliwa alieleza kuwa mapinduzi ya sekta ya kilimo na usindikaji wa mazao yanaweza kumkomboa mwananchi kutokana na kuiga fursa za kuona teknolojia zinazoonyeshwa katika maonyesho ili kuifanyia kazi kwa mtu mmoja au kikundi.
Akizungumzia tija ya ufugaji na kudhibiti migogoro ya ardhi, waziri mkuu alisema kuwa wafugaji wengi wa Tanzania wameendelea kuwa wachungaji wa mifugo kwa kuhamahama sehemu moja kwenda nyingine na kusababisha mifugo mingi kufa kwa magonjwa na kuingia katika migogoro na wakulima.
Mifugo inatembezwa muda mrefu matokeo yake wanyama wanakonda na kuuzwa kwa bei ndogo kwa hasara kutokana na kuchoka na kukosa muda wa mzuri wa kupata chakula.
“Natoa wito kwa wafugaji kufuga mifugo michache tena kwa njia za kisasa ikiwemo kuwanenepesha kwa kutumia mbegu bora ili iwe na afya na kuuzwa kwa bei nzuri lakini itapunguza migogoro.”alisema Majaliwa.
Majaliwa aliwakumbusha watendaji wa mikoa na halmashauri kutekeleza agizo la rais Magufuli la kutenga maeneo kwa matumizi ya mbalimbali yakiwemo ya wafugaji na kilimo kwani tukiwa na mifugo bora, mifugo haitapata magonjwa hovyo, mfugaji na taifa litapata mazao mazuri ya nyama, ngozi na maziwa.
Kukithiri kwa tozo katika mauzo ya mazao ya wakulima na vipimo vya mazao (Lumbesa), Majaliwa ameeleza kuwa serikali ipo katika mpango wa mapitio ya tozo kwa mazao yote ili zisizo na tija ziondolewe.
Kwa upande wa vipimo vya ujazo kupita kiasi maarufu kama lumbesa, Majaliwa alieleza kuwa anawaagiza watendaji wote wa halmashauri nchini kuhakikisha hakuna mazao ya wakulima yanayouzwa kwa mfumo wa lumbesa na badala yake utumike mizani.
“Naagiza lumbesa ni marufuku na wanaochezea mizani kwa lengo la kumpunja mkulima wakamatwe na kufikishwa vyombo vya sheria na minada yote iwe na mizani za kupimia mifugo na kuweka maelezo ya bei kulingana na uzito wa mnyama.”alisema Majaliwa.
Maonyesho ya 24 ya wakulima ya mwaka 2016 kanda ya mashariki Morogoro yamekisiwa kuwa na wakulima wa kujifunza elfu hamsini (50,000) na washiriki 250 kati ya hao 85% wataonesha teknolojia mbalimbali za kilimo wakati 15% wakiwa watoa huduma za burudani.
Kaimu Mwenyekiti wa Taso kanda ya mashariki Morogoro, Jovin Ndimbo ameeleza kuwa maonyesho hayi yana lengo la kuwa shamba darasa kwa kutoa elimu kwa wakulima kutoka halmashauri 35 za mikoa ya kanda ya mashariki.
Maonyesho ya wakulima ya mwaka 2016 yamebeba kaulimbiu ‘Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni Nguzo ya Maendeleo, Vijana Shiriki Kikamilifu (Hapa Kazi Tu) huku uwanja wa Mwl Julius Nyerere ukikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya vipando, barabara kukosa taa za umeme na wadau kutolipa madeni.
Ndimbo alisema kuwa changamoto hizo zimekuwa chanzo cha Taso kushindwa kuboresha baadhi za miundombinu za uwanja wa maonyesho na kuwa upo mchakato wa kuchimba visima ili kupunguza moja za changamoto.
Changamoto zinazotarajiwa kupunguzwa na Taso ni pamoja na kujenga maegesho na kujenga barabara, kupata maji ya uhakika kutoka mto Morogoro na kinachosubiriwa ni kupata fedha ili kuanza kutekeleza mipango hiyo.CHANZO/MTANDA BLOG
0 comments:
Post a Comment