SIRI YA KKKT KUPENDEKEZA MAJINA YA WANAWAKE KUWA WACHUNGAJI YAFICHUKA
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo akizungumza kwenye ibada ya kuadhimisha miaka 25 ya wachungaji wanane wanawake wa Doyosisi ya Kaskazini wakati wa ibada iliyofanyika katika Usharika wa Moshi mkoani Kilimanjaro juzi. Picha na Dionis Nyato
Moshi. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Fredrick Shoo ametoboa siri ya namna pendekezo la kubariki wanawake kuwa wachungaji lilivyopata upinzani mwaka 1991.
Askofu Shoo alitoboa siri hiyo katika Usharika wa Moshi mjini wa Dayosisi ya Kaskazini wakati wa Jubilee ya miaka 25 ya huduma ya wachungaji wanawake katika dayosisi hiyo.
Alisema wakati Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ambaye sasa amestaafu, Dk Erasto Kweka alipoweka pendekezo hilo mbele ya mkutano mkuu lilipata upinzani mkali.
“Tulikuwa kwenye mkutano mkuu kule Siha wakati Askofu Kweka alipoweka patano lile. Lilipata upinzani mkali hadi alifika mahali akafikia kutaka kusema kama hamkubali najiuzulu,” alisema.
Hata hivyo, mkuu huyo wa Kanisa alisema baadaye azimio lile lilipitishwa na wajumbe wa mkutano mkuu, na anamshukuru Mungu kuwa hadi leo, Dayosisi ina wachungaji 34 wanawake.
Dk Kweka alieleza namna suala la kubariki wanawake kuwa wachungaji lilivyokabiliana na upinzani mkali si ndani ya Dayosisi tu, bali hata ndani ya kanisa lenyewe.
Askofu mstaafu wa dayosisi hiyo, Dk Martin Shao alisema katika kipindi cha miaka 25 ya huduma ya wanawake wachungaji, idadi yao imeongezeka kutoka sita mwaka 1991 hadi kufikia 34 mwaka huu.
Hata hivyo, alisema kwa takwimu za washarika wanawake watu wazima wanafikia 90,000 wa dayosisi hiyo, idadi ya wachungaji 34 ni ndogo kwani inawakilisha asilimia 0.04 ya washarika wanawake.
“Kitakwimu inamaanisha kuwa kila wanawake 100 hakuna hata mmoja mwenye wito au aliyepokea wito wa kuwa mchungaji. Tunapaswa kujiuliza wanawake hawaoni fursa hii au hamasa hakuna?” alihoji.
Akisoma risala, mwenyekiti wa wachungaji na wanawake Watheolojia wa Dayosisi hiyo, Mchungaji Joyceline Njama alitaka wachungaji wenzake kuhamasisha wanawake kuacha kuwa wanyonge.
“Kama katika kanisa wanawake ni theluthi mbili ya waumini wote, mbona tusiwatie moyo kushika nafasi za uongozi wa juu katika jamii. Sasa hivi kuna mjadala wa 50-50.
Huu ni unyonge,” alisema. Mchungaji Njama alisema hiyo ni njia moja au nyingine hii ni kuendeleza unyonge na kuona kuwa mwanamke ni wa kusaidiwa tu na kupendelewa tu kana kwamba hastahili.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment