BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

UIIMARISHAJI WA USAFI WA USO NAMNA INAVYOTOA KINGA KATIKA KOPE ZA MACHO

Mratibu wa Huduma za macho mkoa wa Lindi, Dk Mwita Machage akimpima mgonjwa wa macho wakati wa Sikukuu ya Nanenane katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi. Huduma hii ya upimaji wa macho inafadhiliwa kwa ushirikiano wa shirika lisilo la kiserikali la Sightsavers Tanzania na sekretarieti ya mkoa wa Lindi, idara ya afya mkoa. Lindi ni moja ya mikoa yenye maambukzi ya ugo njwa wa vikope. 
Mratibu wa Huduma za macho mkoa wa Lindi, Dk Mwita Machage akimpima mgonjwa wa macho wakati wa Sikukuu ya Nanenane katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi. Huduma hii ya upimaji wa macho inafadhiliwa kwa ushirikiano wa shirika lisilo la kiserikali la Sightsavers Tanzania na sekretarieti ya mkoa wa Lindi, idara ya afya mkoa. Lindi ni moja ya mikoa yenye maambukzi ya ugo njwa wa vikope. 

KURANI, yaani msahafu wa Waislamu unataja macho kama vipenzi viwili vya mwanadamu.

Hebu fikiria umezaliwa unaona kwa macho yako, lakini baada ya miaka kadhaa unapoteza vipenzi hivyo viwili kiasi kwamba huwezi tena kuona, kusoma na sasa unageuka kuwa mtu wa kuongozwa au kutegemea fimbo. 


Mbaya zaidi, hupati upofu huu kwa sababu ya ajali, kwa sababu ya mapenzi ya Mungu au kupata ugonjwa ambao huna namna ya kujikinga nao, bali ni kutokana na ugonjwa ambao ungeweza kabisa kujikinga nao, tena kwa jambo dogo tu na muhimu, kufanya usafi.

Ndio maana Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaeeleza kuwa licha ya Tanzania kuendelea kupata mafanikio katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa vikope (trachoma) wananchi bado wana jukumu la kufuata na kuzingatia kanuni za afya. 


Ni kanuni gani hizo? Kuhakikisha kuwa wananawa uso kwa maji safi na sabuni na kufanya usafi wa mazingira yanayowazunguka ili kuepuka maambukizi ya ugonjwa huo.

Katika kuhakikisha kuwa ugonjwa huo unatokomezwa kabisa nchini, wadau walio katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutoka ndani na nje ya nchi wanaunganisha nguvu zao, lengo likiwa kuzifikia jamii ambazo bado zinakabiliwa na changamoto ya athari za ugonjwa wa vikope.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Neema Rusibamayila anasema Tanzania imepiga hatua katika kupunguza athari za ugonjwa huo kwa wananchi katika nchi za Afrika, jambo linalowavutia wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano hayo.

Dk Rusibamayila anasema idadi ya wagonjwa wanaougua vikope imeendelea kupungua mwaka hadi mwaka kupitia afua mbalimbali chini mpango ujulikanao kama “SAFE” ambao unahusisha huduma za upasuaji, utoaji wa dawa za antibayotiki, kuosha uso pamoja na usafi wa mazingira.

Anasema wizara kwa kushirikiana na wadau hao imeweza kufanikisha upunguzaji wa ugonjwa wa vikope na magonjwa mengine yasiyopewa kipaumbele kwa kutoa dawa na tiba ya kinga kwa wananchi katika maeneo yaliyoathirika ambapo mwaka 2013 zaidi ya watu milioni 19 walitibiwa huku tiba milioni 45 zikitolewa. Anafafanua kwamba tiba hizo zilihusisha dawa aina ya Ivermectin, Albendazole, Praziquantel na Zithromax.

Aidha anasema mwaka 2014 zaidi ya watu milioni 23 walifikiwa kwa dozi milioni 55 za dawa hizo zikatumika. Anafafanua kuwa tafiti zilizofanyika kuhusu ugonjwa huo katika wilaya 22 zinaonesha kwamba ugonjwa wa vikope umepungua sana kiasi cha wananchi wa maeneo hayo kutohitaji dawa za tiba kinga. 


Dk Rusibamayila anasema kuwa juhudi za sasa za wizara ni kuendelea kuwaelimisha wananchi wachukue tahadhari kwa kuzingatia usafi pamoja na kuwaangalia wale waliokwishaugua ugonjwa huo ili waweze kufanyiwa upasuaji.

“Baada ya mtu kupata ugonjwa huu, kope zake huingia ndani na kuanza kukwaruza jicho, kwa mazingira ya kawaida kope za mtu ambaye hana ugonjwa huu hutoka nje, zikiingia ndani hukwaruza jicho na mtu asipofanyiwa upasuaji mapema wa kurekebisha kope zake hupata upofu,” anasema Rusibamayila.

Anafafanua kuwa mashirika mbalimbali yamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia fedha za kufanikisha zoezi hilo likiwemo Shirika na la Msaada la Kimataifa la Uingereza (DFID) pamoja na Mfuko wa Malkia ya Uingereza (The Queen Elizabeth Diamond Jubilee Trust). Mikoa inayonuifaika ni sita; Pwani, Manyara, Lindi, Mtwara, Dodoma na Arusha ambayo imekuwa na kawaida ya maambukizi ya ugonjwa huo.

Mashirika mengine ni Sight Savers Tanzania, Shirika la Helen Keller International (HIK) Tanzania pamoja na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali ambayo mengine yapo Kongwa mkoani Dodoma na Kilimanjaro ambao hushirikiana na wizara kuwatafuta wagonjwa kwa lengo la kutoa matibabu. 


Anasema mpaka sasa kuna wilaya 18 ambazo zinakabiliwa na ugonjwa huo na kufafanua kuwa juhudi za kuwapata wale walioathirika zinaendelea ili waweze kufanyiwa upasuaji na kupatia dawa za tiba na kinga pamoja na elimu ili waweze kubadili tabia kwa kuwa wasafi.

“Serikali tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo uelimishaji wa wananchi wa maeneo husika wachukue hatua. Tunajua ugonjwa huu unaletwa na nzi, tunawahimiza wananchi wanawe uso kuondoa uchafu na kuzuia nzi wanaosambaza ugonjwa huo ambao hutua kwenye macho yao kwa sababu ya uchafu,” anasema Dk Rusibamayila. 


Aidha, anawashukuru wadau hao wa maendeleo kwa kuendelea kutambua mchango wa Tanzania katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele pamoja na kutimiza malengo ya kidunia ambayo yanatoa mwito kwa Tanzania kuwa imetokomeza ugonjwa wa vikope ifikapo mwaka 2020.

Anazitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili kampeni ya kuwafikia wale walioathirika katika maeneo yenye maambukizi ya ugonjwa kuwa ni ile ya maeneo ya jamii za wafugaji kuishi kwa kuhamahama, sababu za mazingira hasa miundombinu ya barabara ambayo imekua kikwazo cha kuzifikishia huduma jamii hizo katika kipindi cha mvua.

Kwa upande wake, Mratibu wa Taifa wa Magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Upendo Mwingira anasema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za Bara la Afrika ambazo zimekuwa zikinufaika na fedha kutoka Shirika la Kimataifa la Uingereza na DFID na mfuko wa ulioanzishwa wa kumuenzi Malkia wa Uingereza kwa miaka 60 ya Utawala wake unaojihusisha na utokomezaji wa ugonjwa wa Trakoma katika Afrika.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mwingira anasema ugonjwa wa vikope nchini Tanzania kwa mujibu wa takwimu uko katika wilaya 56. Lakini anasema kutokana na juhudi ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Serikali kuanzia mwaka 1990 hali inaonesha kuwa maambukizi yameshuka hasa katika wilaya 22 ambako wananchi hawahitaji tena kugawiwa dawa. 


Anasema hali ya maambukizi katika maeneo hayo imewapata zaidi watoto na wanawake walio katika maeneo yenye ukame na yale yenye shida ya maji ikiwemo mkoa wa Manyara na Dodoma.

Anabainisha kuwa mpaka sasa ni wilaya 18 ambazo zinahitaji huduma ya dawa zilizo katika mkoa wa Arusha, Manyara na Dodoma (katika wilaya ya Kongwa, Chemba na Chamwino).


“Jitihada tunazofanya ni kubwa, bado tuna kazi hasa maeneo ya wafugaji ambayo baadhi wananchi wamekuwa wakitumia baadhi ya vifaa kunyofoa kope zinazowasumbua ili kuondoa usumbufu bila kujua hali hiyo inatengeneza tatizo zaidi, ni changamoto kwetu, tunahitaji kuendelea kuwaelimisha,” anasema.

Anaeleza kuwa kutokana na juhudi mbalimbali zilizofanywa na Serikali na wadau, sasa wanajiandaa kufanya tathmini katika wilaya zipatazo 10 katika kipindi cha mwaka huu kuangalia maambukizi yamefikia wapi kwa lengo la kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo wa vikope na kupunguza hali ya maambukizi katika wilaya hizo. 


Anasema kuwa takribani watu 160,000 wameambukizwa vikope na kubainisha kwamba kuna mikakati mbalimbali imefanywa na wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuendesha upasuaji kwa wagonjwa wenye tatizo hilo, hali iliyoshusha kiwango hicho hadi kufikia wagonjwa 80,000 mwaka huu.

Anafafanua kuwa chini ya ufadhili wa miaka mitano wa wadau kutoka mashirika hayo ya Marekani na Uingereza, wagonjwa takribani 50,000 wenye tatizo la vikope watafanyiwa upasuaji, huku serikali na wadau wengine ikiendelea kutafuta fedha za kuwafikia wagonjwa 30,000 watakaobaki. 


Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kimataifa ya Maendeleo nchini Tanzania (DFID), Vel Gnanendra anasema kuwa wao kama wadau wa maendeleo wataendelea kuiunga mkono Tanzania kwa kuhakikisha ugonjwa wa vikope unatokomezwa nchini.

“Tunafurahia ushirikiano huu kutoa mchango wetu kuisaidia Tanzania kutokomeza ugonjwa wa vikope, kuzuia maumivu na mateso yanayosababishwa na ugonjwa huu yanayowafanya watu kuangukia katika lindi la umasikini, tunaiahidi Serikali ya Tanzania kuwa kupitia ushirikiano huu tutautokomeza ugonjwa huu na kubadili maisha ya wengi miaka ijayo,” anasema Gnanendra.

Mkurugenzi Mkuu wa mfuko wa Malkia wa Uingereza unaojihusisha na utokomezaji wa ugonjwa wa vikope katika nchi mbalimbali za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania, Dk Astrid Bonfield anasema kuwa mfuko huo utaendelea kuisaidia Tanzania kwa kuwa Tanzania inafanya vizuri katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.


Anasema Mfuko wa Malkia Elizabeth utafanya kazi bega kwa bega na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuhakikisha kuwa hakuna mtanzania anayepoteza haki ya kuona kutokana na ugonjwa wa vikope.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: