BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

BARAZA LA WAISLAMU TANZANIA LATETEA ADHABU YA KIFO KWA WATU WANAOKUTWA NA HATIA YA MAUAJI YA KUKUSUDIA

Tokeo la picha la PHOTOS OF ADHABU YA KUNYONGWA
BARAZA la Waislamu Tanzania (Bakwata), limetetea hukumu ya adhabu ya kifo kwa watu wanaokutwa na hatia ya mauaji ya kukusudia kwa nia ya kuiepusha jamii na athari zitokanazo na kushamiri kwa vitendo vya aina hiyo.

Aidha, wakati Bakwata ikieleza msimamo huo unaolingana na ule wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) limetoa mapendekezo ya kupinga adhabu hiyo na kutaka iondolewe huku Tume ya Haki za Binadamu akitaka adhabu mbadala itafutwe na siyo ya hukumu ya kifo kwa sababu kuendelea kuitoa kwa watu wanaokutwa na hatia ni sawa na kukiuka haki ya kuishi ya kila binadamu.

Akizungumza kwa niaba ya Bakwata kwenye kongamano la kumbukumbu kupinga adhabu ya kifo duniani jijini Dar es Salam jana, Sheikh Ally Ngeruka alisema adhabu ya kifo itakapofutwa nchini itatoa mwanya kwa baadhi ya watu ndani ya jamii kutenda zaidi makosa hayo kwa kujua kuwa hata wakikutwa na hatia bado wataendelea kuachiwa kwa kupata adhabu zisizolingana na thamani ya uhai wa watu wanaowapotezea maisha.

Ngeruka alisema Bakwata inaunga mkono kuwapo kwa sheria hiyo, ambayo lengo lake ni kuifunza jamii kuwa jambo hilo halifai na kwamba, anayekiuka haki ya kuishi ya mwingine ajue kuwa naye akikutwa na hatia atapewa adhabu hiyo ya juu zaidi.

Hata hivyo, Ngeruka alisema kuwa licha ya kutaka sheria hiyo ya adhabu ya kifo iendelee kuwapo, bado sheria hiyo peke yake haitoshi katika kukomesha vitendo vya mauaji dhidi ya watu wasio na hatia na hivyo ipo haja ya kuiongoza jamii katika njia sahihi ili suluhu ipatikane kabla ya vitendo hivyo kufanyika.

“Kumtetea muuaji aliyekusudia kuua si sawa… kwa mfano, magaidi wanavyoua watu katika umati mkubwa sokoni au popote, kamwe wasisamehewe. Adhabu iwakute. Waadhibiwe ili jamii ijifunze,” alisema Sheikh Ngeruka.

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) imesema kuwa adhabu hiyo bado ipo nchini ingawa haijatekelezwa tangu mwaka 1994, licha ya kutolewa hukumu kwa watu 472 waliokutwa na hatia ya mauaji.

Ilielezwa na ofisi ya DPP kuwa adhabu hiyo haijatekelezwa kutokana na marais waliokuwa katika muda huo kutoweka saini hati ya utekelezaji wa adhabu hiyo kwa mujibu wa ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1997.

Adhabu ya kifo imewekwa kama adhabu ya lazima kwa mtu atakayepatikana na hatia ya mauaji na uhaini, chini ya vifungu vya 39 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Wakili Mwandamizi wa Serikali kutoka ofisi ya DPP, Neema Haule, alisema licha mahakama kuendelea kutoa hukumu ya adhabu hiyo, utekelezaji wake haujafanyika kwa kipindi chote hicho ambacho ni zaidi ya miaka 20.

Alisema Serikali, katika kutekeleza majukumu yake ya kisheria kupitia ofisi ya DPP, itatekeleza adhabu hiyo kwa mujibu wa sheria na kwamba ipo haja ya wadau kukaa pamoja na kujadili namna ya kuiondoa adhabu hiyo.

“Sheria ya adhabu ya kifo imesisitiza kunyongwa hadi kufa kwa wahaini, magaidi waliofanya mauaji… na inatekelezwa kwa mujibu wa sheria. Kuna matukio ya ukatili ambayo yanaendelea kutokea ndani ya jamii, watu wasio na hatia wanauawa hivyo sheria ipo kwa ajili ya kutoa haki,” alisema Haule.

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bahame Nyanduga alisema ipo haja ya kuondoa adhabu hiyo kwa kuwa inapingana na mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa ikiwamo Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kisiasa na Kiraia ibara ya 6, na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu.

Alisema tayari nchi 149 duniani 22 za barani Afrika ikiwamo, Rwanda, Burundi, Togo, Afrika Kusini, Congo Brazaville zimefuta adhabu hiyo, ili kulinda haki za binadamu kwa kuwa adhabu hiyo ni ukatili na inatekelezwa pasipo utu.

“Katiba ya Tanzania inatambua haki ya kuishi… wakati huohuo kuna adhabu ya kifo, adhabu hii bado haijatuaminisha vya kutosha kwamba inazuia matukio ya mauaji badala yake watekelezaji wa adhabu hii wanakuwa wanaungana na muuaji pale wanapomuadhibu,” alisema Nyanduga.

Mkurugenzi Idara ya Haki na Amani kutoka TEC, Cassian Lushinge, alisema bila kujali aina ya uhalifu, iwapo jamii inaweza kujilinda bila kupoteza uhai wa maisha ya watu, hakuna haja ya utekelezaji wa adhabu hiyo.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba alisema adhabu ya kifo, ni ukiukwaji wa haki ya kuishi, haki inayolindwa kikatiba na ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.

“Haki ya kuishi imewekewa mipaka na sheria nyingine za nchi, adhabu ya kifo inakiuka haki ambayo ni ya msingi kuliko nyingine,” alisema Dk. Bisimba. 


Alisema kuna haja ya kuongeza uelewa na ufahamu ndani ya jamii kuhusu adhabu hiyo, kwa kuzingatia ulinzi wa haki ya kuishi nchini na kwamba inaweza kutolewa adhabu mbadala kwa wanaofanya makosa hayo ikiwamo kifungo cha maisha.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: