MATUMIZI ya mitandao ya kijamii yana faida na changamoto zake hivyo umakini zaidi unatakiwa ili kuona jamii inanufaika zaidi na kuepusha athari kwa mienendo ya jamii hasa wanafunzi wanaotumia muda mwingi kufuatilia haya na yale. Miongoni mwa mitandao hiyo, ambayo ni zao za uvumbuzi na ubunifu wa kisayansi na teknolojia ni WhatsApp, Facebook, Twitter na Istagramu ambayo baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakiitumia ndivyo sivyo na kujikuta wakifeli masomo.
Baadhi ya wanafunzi wanaoutumia vizuri mitandao hiyo, wamekuwa wakifanya vizuri katika masomo yao kutafuta na kupata vitui vingi vya kujisomea kulingana na masomo yao, lakini kwa wanaoutumia vibaya wamekuwa wakifeli.
Mambo hayaiishi hivyo,kwa baadhi ya wasichana wamejikuta katika matatizo makubwa ikiwamo kupata ujauzito.
Miongoni mwa waathirika wakuu ni wanafunzi hasa wa shule za sekondari wanaokwenda na simu shuleni zikiwamo zenye uwezo wa kufungua mitandao ya kijamii, na kupata vitu ambavyo ni kinyume na maadili yakiwamo masuala ya ngono na kujikuta wakitekwa na kuzembea katika masomo.
Shekhe Msafiri Kitumbo wa msikiti wa Mshikamano mjini Shinyanga, akizungumzia mwenendo huo, anakemea tabia ya baadhi ya wanafunzi kuitumia mitandao hiyo vibaya na kuchangia kuporomosha maadili kwa watoto hata kushusha taaluma zao.
Akizungumza katika mahafari ya wanafunzi wa Sekondari wa Jumuiya ya Kiislamu (TAMSYA), mjini Shinyanga hivi karibuni wanaotarajiwa kuhitimu masomo yao Novemba mwaka huu, anadai kuwa mitandao hiyo ya kijamii imechangia kuharibu baadhi ya watoto kwa kutaka kujifunza mambo ya wakubwa na kujikuta wakifeli masomo yao.
“Siku hizi hata baadhi ya watoto wetu wa Kiislamu hawana maadili kabisa, kutokana na mitandao hii ya kijamii kwa kuposti picha za uchi. Mtoto wa kiislamu anatakiwa kujistiri mwili wake asiuache wazi kabisa ,” anasema Kitumbo
Anaongeza ” hata kwenye mahudhurio ya masomo ya kiislamu madrasa yamekuwa hafifu, utandawazi umeshaharibu wanafunzi na wakati shule hii ya kidini hua inawafunda watoto kuwa na maadili mazuri ya kiroho na dunia.”
Mkuu wa shule ya sekondari Uhuru mjini Shinyanga, Rwegasila Jasoni anasema katika shule yao wamepiga marufuku wanafunzi wake kwenda na simu shuleni, lakini kwa sababu wanafunzi tayari ni waathirika wa simu hizo, wamekuwa wakienda nazo kwa kificho na kuchati mambo ya kipuuzi.
Anasema katika mkutano huo na wazazi wa shule hiyo Jasoni anasema, wamekubaliana mwanafunzi atakayekamatwa akiwa na simu shuleni ipondwe kwa mawe hadi kuharibiwa kabisa.
Tangu makubaliano hayo yafikiwe,tayari simu saba na CD moja zilizokuwa na picha ya ngono zimevunjwavunjwa.
Anasema licha ya kuwaelimisha wanafunzi kuhusu madhara ya kuwa na simu shuleni na kutumia mitandao ya kijamii vibaya, baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakiwapiga vijembe, kuwa wao wamezeeka na kupitwa na wakati kwa kile kinachodaiwa kuwa hii ni karne yao, mazingira yanayochangia kusababisha tatizo hilo kuendelea kuwa sugu.
“ Kisaikolojia mwanafunzi anapoperuzi mambo ya filamu ama picha za ngono kwenye mitandao lazima atataka kujaribu kufanya na yeye ili aone kitakachotokea na kujikuta taratibu anazama kwenye mapenzi na kusahau masomo,” anasema Jasoni.
Anafafanua kuwa, mwanafunzi akizama kwenye mapenzi, lazima atashuka kitaaluma hata kama alikuwa anafanya vizuri huko nyuma kimasomo, kutokana na ubongo wake kuchanganya na vitu ambavyo havimstahili kwa wakati huo , kujikuta akifanya vibaya hatimaye kufeli na kupoteza kutimiza ndoto zake.
Katika suala hilo la kukomesha wanafunzi kuwa na simu zenye uwezo wa kuperuzi mitandao ya kijamii, anasema linapaswa kushirikiana na wazazi kuwataka kuwa karibu na watoto wao kwa kuwaeleza madhara yake pamoja na kuwakagua kama wanamiliki simu hizo.
“Mfano siku moja tulienda kwenye tamasha la michezo, cha ajabu nikaona kila mwanafunzi ana simu nikabaki kujiuliza wamezitoa wapi wakati shuleni tumewakagua. Walikuwa wakipigana picha ovyo na kupost kwenye mitandao ya kijamii,” anasema Jasoni
Naye Mwalimu wa shule ya sekondari Buluba Shinyanga, Suleiman Shagata, anakiri mitandao ya kijamii inachangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi kukosa maadili hata kushuka kitaaluma kutokana na ukweli kuwa, akili yao kuipeleka kwenye mambo ya wakubwa na kujikuta hawazingatii masomo darasani.
Katika katika shule yao ya Buluba nao walipiga marufuku simu hizo, lakini wanafunzi wanaporudi kwao huanza kuzitumia na kuacha kutafuta mafunzo ya kujiongezea maarifa, na kuwasiliana masuala maovu na kutongozana ovyo.
“Mwanafunzi anapoperuzi upuuzi lazima ataathirika, na akiingia darasani kusoma mawazo yake yatakuwa mbali sana na kujikuta hajaelewa kinachofundishwa na mtihani unapokuja lazima atafeli tu, maana ameingia kwenye ulimwengu mwingine,” anasema Shagata
Naye mwanafunzi wa shule ya sekondari Uhuru, Omar Omary anasema, mitandao ya kijamii imekuwa tatizo kwa wanaoitumia vibaya kuperuzi mambo ya wakubwa hivyo wamekuwa wakishuka kitaaluma.
Anasema wanafunzi wanaoitumia vizuri kwa kutafuta masomo ya kujifunza na kujisomea kwa njia hiyo ya mitandao, wengi wao wamekuwa wakiinuka kitaaluma maana sio kitu katika mitaala ya wanafunzi kinatoka kwa mwalimu, bali vitu vingine lazima ujitafutie mwenyewe kwa kutumia maktaba na mitandao ya kompyuta.
Mzazi mmoja aitwaye Evarist Kabalo, anasema watoto wa siku hizi ni wajanja sana wamekuwa wanamiliki simu tena za gharama kubwa bila ya wao kujua au kufahamu wamezitoa wapi. Wamekuwa wanazitumia kwa kificho hasa nyakati za usiku wao wamesha lala, au siku za mwisho wa wiki.
Kabalo anasema, kinachopaswa ni kuendelea kushirikiana kati ya wazazi na walimu kutoa elimu kwa wanafunzi ya kuwaeleza madhara ya matumizi mabaya ya mitandao kijamii, ili waitumie vizuri katika kujadili masomo yatakayowafanya watimize ndoto zao.
Kwa upande wake, Ofisa elimu mkoa wa Shinyanga Mohamed Kahundi, anasema sheria za elimu zinazuia mwanafunzi kuwa na simu shuleni na kipindi wanapotaka kujiunga na masomo huwa wanapewa miongozo na mwanafunzi atakayekamatwa na simu anastahili kufukuzwa.
Kahundi anasema, kutokana na ubinadamu inabidi walimu wakuu walegeze masharti hayo na kutoa adhabu kwa wanafunzi wahusika ikiwamo kunyang’anywa simu zao, lakini tatizo hilo linaendelea kuwa kero mashuleni na kusababisha hata baadhi ya wanafunzi wa kike kutekwa katika mazingira hayo na kujikuta wakipachikwa mimba na kukatisha ndoto zao.Nipashe

0 comments:
Post a Comment