BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

NSSF YAWASTUKIA WANACHAMA WAKE ZAIDI YA 1,000 KWA UDANGANYIFU

 
MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umesema zaidi ya wanachama wake 1,000 wamekamatwa nchini kwa kughushi nyaraka ili wawe na sifa ya kulipwa fao la kujitoa.

Aidha, kuna kesi sita za watu wanaojiita mawakala wa kusaidia watu walioacha kazi ili wajitoe kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, zilizofikishwa mahakamani na kuripotiwa polisi, imeelezwa.

Akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalumu jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara, alisema nyaraka ambazo wanachama wao wamekuwa wakighushi ni barua za kuacha au za kufukuzwa kazi.

Aidha, mkurugenzi huyo alisema uchunguzi wa NSSF ulibaini kuwapo kwa baadhi ya wafanyakazi wa mfuko huo ambao hushurikiana na mameneja waajiri kuandika barua za kuonyesha wanachama husika wameacha au kufukuzwa kazi ili walipwe michango, lakini baada ya kufuatilia walibaini bado wapo kazini.

“Wapo walioleta barua za kuacha au kufukuzwa kazi zilizoandikwa na HR (Idara ya Utawala) lakini unapohoji kwa meneja, unabaini mfanyakazi husika bado yupo kazini," alisema.

"Tulivyobaini udanganyifu huo, tuliamua kila anayeleta barua kuwa ameacha kazi tunamfuatilia kwa karibu na tukabaini 'madudu' hayo."

Mkurugenzi huyo alisema uchunguzi wao pia ulibaini baadhi ya wafanyakazi wa mfuko huo wasio waaminifu walihusika katika kuwasaidia wanachama hao kujipatia fedha hizo.

Alisema kuna watu walianzisha kampuni za uwakala (hakuzitaja) kwa ajili ya kusaidia wanachama wa mifuko ya jamii, ikiwamo NSSF, kuandaa nyaraka zinazoonyesha wameacha au kufukuzwa kazi ili wapate fedha hizo.

Alisema mawakala hao walikuwa wanalipwa na wanachama wa mfuko gharama za kufanikisha mchakato huo, wa mwanachama husika kupatiwa michango yake na mfuko husika.

Prof. Kahyarara aliitaja mikoa na wilaya husika na idadi ya kampuni zilizobanika na kuchukuliwa hatua kwenye mabano kuwa ni Kinondoni (2), Temeke (2), Mwanza (3), Arusha (2), Kilimanjaro (1).

“Vishoka hawa baada ya kuwabaini kwa kushirikiana na vyombo vya dola, walikamatwa. Pia baadhi ya wanachama wetu walikamatwa na wengine uchunguzi unaendelea," alisema na kufafanua zaidi:

"Watu waelewe udanganyifu wowote watakaofanya NSSF, utabainika na watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria."

WANAOBADILI KAMPUNI
Aliwaonya waajiri wanaoshirikiana na wafanyakazi kutengeneza nyaraka za kughushi ili kuonyesha wamefukuzwa au kuacha kazi na wale wanaobadili kampuni au taasisi ya kufanyia kazi na kukimbilia kuchukua michango yao.

Alisema lengo la mifuko ya hifadhi ya jamii siyo kufanya kazi ya benki ya kutunza fedha kwa ajili ya mwanachama kuzichukua muda wowote, bali kuwahudumia kwa mafao mbalimbali yakiwamo ya matibabu na kujifungua ambayo hutolewa wakati mwanachama akiendelea na kazi.

Aliongeza kuwa hakuna fao la kujitoa, bali kustaafu ambalo hutolewa baada ya mwanachama kumaliza muda wake wa utumishi kwa mujibu wa sheria ili apatiwe fedha za kumsaidia kipindi ambacho hana kazi na hana nguvu za kufanya kazi tena.

Alifafanua kuwa watu wengi hutaka kuchukua fedha hizo na wengi wao wanapozeeka huishi maisha magumu.

Alisema taarifa za mfuko zinaonyesha Tanzania inakadiriwa kuwa na wazee milioni tatu ambao wanaishi maisha magumu kutokana na kutokuwa na pensheni na baadhi ni wale waliochukua michango yao wakati wakiwa vijana.

Mkurugenzi huyo alisema NSSF inatoa elimu zaidi kwa umma kutambua malengo ya mifuko siyo kutunza fedha kwa muda mfupi na kuzichukua, bali kuangalia maisha ya wanachama baada ya kustaafu au kupatwa na majanga makubwa.

Alisema masharti ya kutoka kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ni magumu na wengi wanakiuka na kupoteza haki zao, na kwamba licha ya kushauriwa kuendelea kuwapo kwa kuangalia maisha ya baadaye, wengi hao huangalia kupata fedha kwa haraka.

“Baadhi wanatumia nyaraka za kughushi ili kudanganya amefikisha umri wa kustaafu, amefukuzwa na kuacha kazi. Ni uhalifu, na wapo tuliowakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria,” alibainisha.

Prof. Kahyarara alisema wengi hawajui wanapojitoa kwenye mifuko hiyo wanaathiri maisha yao kwa kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuwasaidia wanapokuwa wazee au kupata ajali.

“Tungependa watu waweke fedha zao, wakifikisha umri wa miaka 55 au wamechangia miaka 15 mfululizo, wataishi maisha mazuri kuliko kuchukua fedha kabla ya hapo. Na anapopata majanga anaaibika," alisema.

“Tunapowapigania wasitoke siyo kwamba tunataka kushikilia fedha zao, bali kuwaonea huruma kwamba alikuja tumsaidie baadaye, lakini anataka kuondoa mapema…

"Dunia nzima hili halikubaliki."
Mwezi uliopita vyama vya wafanyakazi na asasi za kiraia zilitoa tamko la kupinga pendekezo la sheria ya kuondolewa kwa fao la kujitoa na kuingizwa fao la kukosa ajira. 


Hoja hiyo iliyotolewa kabla ya serikali kuwasilisha muswada wa mabadiliko ya sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii ukiwa na kipengele cha kuzuia wanachama kujitoa katika mifuko hiyo.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: