Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda aliwataja waliokufa ni Kabula Joseph (23) na Ndalo Luhejela (28), wote wakiwa ni wake wa watoto wa mganga huyo wa kienyeji.
Mwingine ni mwanamume ambaye alitambuliwa kuwa ni Idulu Masanja (30). Kamanda Nyanda alieleza kuwa vifo hivyo, vimetokea Oktoba 13, mwaka huu saa nne usiku katika kitongoji cha Senta ya Maradona, kijijini Kabange, kata ya Sibwesa katika wilaya mpya ya Tanganyika.
Aliongeza kuwa mganga huyo wa kienyeji, anatafutwa na Polisi baada ya kutoroka na kujificha kusikojulikana baada ya kutenda uhalifu huo.
“Tulipopekua nyumba yake tulikuta nyara kadhaa za serikali,” alieleza. Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Mpanda , Dk Mohamed Mpunja alieleza kuwa uchunguzi wa kitatibu, umebaini kuwa chanzo cha vifo vya watu hao watatu, walikunywa dawa ya kienyeji ya aina moja iitwayo nyungu.
Akisimulia mkasa huo, Dk Mpunja ambaye alienda eneo la mganga huyo wa kienyeji, alisema watu wote watatu walikufa papo hapo baada ya kunywa dawa hiyo ya kienyeji nyumbani kwa mganga huyo.
Alisema usiku huo wa tukio, mganga huyo wa kienyeji alimpatia mke wa mtoto wake mdogo aitwaye Kabula dawa ya kienyeji ya kusafisha tumbo. Aliongeza kuwa baada ya kunywa dawa hiyo, Kabula alianza kutapika na kupoteza nguvu mwilini hatimaye alifariki.
“Mganga huyo alimpatia mke wa mtoto wake mkubwa aitwaye Ndalo dawa ya kienyeji ya kusafisha tumbo mara baada ya kunywa alianza kuharisha na hatimaye akafariki dunia,” alieleza.
Dk Mpunja alieleza kuwa mtu mwingine aliyepoteza maisha ni mwanamume aitwaye Masanja, ambaye alifika katika kitongoji hicho kuhani msiba, ambapo kabla ya kurudi nyumbani kwake alienda kwa mganga wa kienyeji , Jaheda, ili atibiwe tumbo la ngiri.
“Mganga huyo wa kienyeji alimpatia Masanja dawa ya kienyeji iitwayo nyungu ambayo aliinywa, ndipo akaanza kutapika na kuharisha alifariki dunia muda mfupi baadaye,” alieleza. Alibainisha kuwa mganga huyo wa kienyeji, hajasajiliwa wala hakuwa na kibali cha awali kinachomruhusu kutoa tiba mbadala.
Dk Mpunja aliwataka wakazi mkoani humo, wakihisi dalili za ugonjwa, waende kwenye vituo vya afya vinavyotoa huduma kwa matibabu, huku akiwataka waganga wa kienyeji hususan wa tiba mbadala, wajisajili.Habarileo

0 comments:
Post a Comment