BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

GIZA NENE LAKUBIKWA KIFO CHA BONDIA WA NGUMI ZA KULIPWA TANZANIA THOMAS MASHALI

 MAKUBWA yamefichuka kwenye msiba wa aliyekuwa bondia machachari wa ngumi za kulipwa nchini, Thomas Mashali ‘Simba Asiyefugika’ aliyefariki usiku wa kuamkia jana Jumatatu kwa madai ya kushambuliwa na watu wasiofahamika.

Mashali aliyewahi kunyakua mataji kadhaa likiwamo wa Dunia wa UBO, alikumbwa na mauti wakati akiwahishwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kupewa rufaa kutoka Hospitali ya Sinza Palestina, jijini Dar es Salaam.

Inadaiwa Mashali alishambuliwa na watu hao usiku wa manane katika eneo la Kimara Bonyokwa kiasi cha kupasuliwa vibaya kichwani kabla ya vijana kwenda kutoa taarifa kwa baba yake eneo la Tandale.
Baba wa marehemu Christopher Malifedha, aliliambia Mwanaspoti kwenye msiba wa mwanae nyumbani kwake, kuwa saa 8;30 usiku alikuja kujulishwa juu ya kujeruhiwa kwa mwanae na dada wa Mashali akaenda Palestina na kujulishwa kuwa amewahishwa Muhimbili ambapo, kabla ya kufikishwa huko alifariki dunia, huku baba huyo akifichua mambo mengi.

Malifedha alisema mwanae alikuwa mtoto wa tano na aliacha shule tangu darasa la tano kutokana na utukutu uliokithiri kabla ya kutumbukia kwenye mchezo wa ngumi ambao, hakuwahi kuhudhuria hata pambano lake moja.

Mzee huyo alifichua kuwa ni miaka mingi hakuwahi kuonana uso kwa uso na Mashali zaidi ya kuwasiliana naye kwenye simu na hata juzi jioni kabla ya kukumbwa na mauti aliwasiliana naye saa 11;24 jioni kumuulizia dili lake la pambano lililokuwa mbele yake.

KAACHA WATOTO WATANO
“Mwanangu kaacha watoto watano, Rose, Rachel, Lilian, Lidya na Jacqueline, lakini ni kama aliwatekeleza kwangu, nikiwalea na kuwasomesha na ulikuwa ni ugomvi mkuu enzi za uhai wake, ni mwanangu lakini sikufurahishwa na tabia zake,” alisema mzee huyo. 


Alisema hakuwa anajua mwanae anaishi wapi wala kujua tabia zake kwani, alishahama kwake kitambo na hakuwa akimtembelea kumjulia hali zaidi ya kuwasiliana naye kwa simu tu.

Kuhusu mazishi alisema bado walikuwa wakiendelea kufanya taratibu ikiwamo kupata kibali cha Polisi kisha kuona kama watamzika hapa ama kwao Songwe.

“Kwa sasa tunamsubiri kaka mkubwa wa marehemu tujue kama azikwe hapa ama Songwe, ila kifo chake kinaniuma sana,” alisema Mzee Mashali.

Mtoto mkubwa wa marehemu, Rose (17) alisema mara ya mwisho kuonana na baba yake ilikuwa Agosti mwaka huu, alipoenda kumpeleka kununua vifaa vya shule. Anasoma kidato cha Tatu Shule ya Sekondari Tegeta. 


Bondia Mada Maugo na Francis Cheka, wamekiri kuguswa na kifo cha mwenzao ambao walikuwa katika maandalizi ya kupigana naye kati ya Novemba 26 na Desemba 25, mwaka huu, huku akisema ni pigo kwa mchezo wa ngumi nchini.Chanzo/Mwanaspoti
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: