BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

VYAMA VYA SIASA VYA AKINA JAMES MAPALALA VYAFUTWA


Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi

MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amefuta usajili wa kudumu wa vyama vya siasa vitatu kutokana na kupoteza sifa za usajili wa kudumu kwa kukiuka masharti ya sheria ya vyama vya siasa.


Vyama hivyo ni Chama cha Haki na Ustawi (CHAUSTA), The African Progressive Party of Tanzania (APPT-Maendeleo) na Jahazi Asilia.

Chausta ni chama kilichopata usajili wa kudumu Novemba 15, 2001 na kilikuwa kinaongozwa na James Mapalala akiwa Mwenyekiti, APPT - Maendeleo kilipata usajili Machi 4, 2003 kikiongozwa na Peter Mziray kama Rais Mtendaji wakati Jahazi Asilia kilipata usajili Novemba 17, 2004 na Mwenyekiti wake ni Kassim Bakari Ali.

Kufutwa kwa vyama hivyo vitatu, kunaifanya Tanzania ibaki na vyama 19 vyenye usajili wa kudumu, kwa mujibu wa orodha ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini. Jaji Mutungi alisema kila chama kilipewa taarifa ya nia ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kufuta usajili wa kudumu na kutakiwa kueleza kwa nini kisifutwe.

Alieleza kuwa katika utetezi wao, vyama hivyo vilishindwa kutoa sababu za kuridhisha kuwa havijakiuka sheria na bado vinazo sifa za usajili wa kudumu.

Jaji Mutungi alisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi kuhusu hatua hiyo na kuongeza kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 7( 3) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, taasisi yoyote hairuhusiwi kufanya kazi kama chama cha siasa, kama haijasajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa.

“Kwa mamlaka niliyopewa chini ya Kifungu cha 19 cha Sheria ya Vyama vya Siasa Namba 5 ya Mwaka 1992, nimefuta usajili wa kudumu wa vyama vya siasa vitatu kuanzia leo (jana),” alisema Jaji Mutungi.

Alisema mchakato wa kufuta usajili wa vyama hivyo, unatokana na kazi ya uhakiki wa utekelezaji wa masharti ya usajili na matakwa mengine ya sheria ya vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu lililofanyika kuanzia Juni 26 hadi Julai 26, mwaka huu.

Jaji Mutungi alisema katika uhakiki huo, ilibainika kuwa vyama hivyo vimepoteza sifa za usajili wa kudumu kwa kukiuka masharti ya sheria ya vyama vya siasa.

Alisema mapungufu kwa ujumla wake, ambayo yameoneshwa katika kila taarifa ya kufuta usajili wa kudumu kwa vyama hivyo kuwa ni pamoja na kutokuwa na ofisi ya chama Tanzania Bara na Zanzibar kwa mujibu wa kifungu cha 10(d), kutokuwa na wanachama Zanzibar kwa mujibu wa kifungu cha 10(b), kushindwa kuweka kumbukumbu za mapato na matumizi ya chama kwa mujibu wa kifungu cha 14 (1) (a).

Alisema mapungufu mengine ni kushindwa kuwasilisha hesabu zao za mapato na matumizi ya mwaka kwa mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) ili zikaguliwe kwa mujibu wa kifungu cha 14 (1) (b)(i), kushindwa kuwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa tamko la orodha ya mali za vyama vyao na kushindwa kutekeleza matamko ya Kifungu 15 (1) kwamba mapato yote ya fedha ya chama yawekwe katika akaunti ya chama.

Jaji Mutungi alisema pamoja na kuvifuta vyama hivyo, pia anaviasa vyama vilivyobaki kuendelea kutekeleza matakwa ya sheria ya vyama vya siasa ili kuepukwa kufutwa.

Kadhalika, aliwakumbusha waliokuwa wanachama na viongozi wa vyama vilivyofutiwa usajili kuwa hawapaswi kufanya shughuli yoyote ya kisiasa, kwa kutumia jina la chama cha siasa kilichofutwa. 


Alisisitiza kufanya hivyo ni kukiuka sheria za nchi, ikiwemo Sheria ya Vyama vya Siasa vya mwaka 1992.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: