BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAKULIMA WAGOMA KUNUNUA MBEGU ZA MAZAO RUKWA.


WAKULIMA mkoani Rukwa wameeleza kutokuwa tayari kununua mbolea na mbegu kutoka katika maduka binafsi wakihofia kuuziwa pembejeo zisizo na ubora huku wakiomba serikali pembejeo zote ziuzwe kupitia Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC).

Hayo yaliibuka wakati wa kikao kilichopitia na kujadili rasimu ya mkakati wa kilimo katika mkoa wa Rukwa msimu wa mwaka 2016/2017 kilichoketi mjini hapa na kuhudhuriwa na wadau na wataalamu wa kilimo.

Meneja wa TFC Mkoa wa Rukwa, Stephen Mtweve alisema kuwa hadi sasa mbolea ya ruzuku iliyosambazwa ni tani 1,300 kati ya 2,444 zilizotengwa kwa ajili ya mkoa huo huku akisisitiza kuwa kampuni hiyo inahifadhi na kusambaza mbolea ya ruzuku pekee.

Mkulima Zeno Nkoswe akichangia mada aliitaka serikali ione uwezekano wa pembejeo za ruzuku na zisizo za ruzuku kuhifadhiwa na kuuzwa kwa wakulima na TFC pekee kwa kuwa hatua hiyo itawanusuru kuuziwa pembejeo feki ikiwemo mbegu za mahindi na mbolea.

“Msimu uliopita mbolea na mbegu zisizo na viwango tulizonunua madukani zilituangusha sana, tunaiomba serikali itutizame kwa jicho la huruma na sisi wakulima ambao hatuhusiki na pembejeo za ruzuku basi pembejeo zisizo za ruzuku ziuzwe na TFC kwa bei ya soko kuliko kuzinunua madukani ambazo ubora wake hatuna uhakika nao,” alisisitiza.

Kauli hiyo iliungwa mkono na wadau wengine wa kilimo ambao walisisitiza kuwa tani za pembejeo za ruzuku zilizotengwa kwa wakulima wa mkoa huo ni kidogo wakitaka ziongezwe.

“Wanaouza pembejeo feki madukani ni wajanja sana kwani nao wanahifadhi mbolea na mbegu za mahindi katika vifungashio vyenye alama za kampuni kubwa zinazosambaza mbegu bora za mahindi,” alisema Ozema Chapita.

Ofisa Kilimo kutoka sekretarieti ya mkoa wa Rukwa, Hamza Mvano alisema kuwa mbegu za mahindi zimeadimika madukani kutokana na msako uliofanyika kubaini mbegu feki za mahindi zinazouzwa madukani.

Aliwashauri wakulima kununua mbolea zilizothibitishwa ubora na Wakala wa Udhibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI) ambapo vifungashio vimebandikwa alama maalumu ya kibandiko 'sticker'.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: