BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

NJIA YA KUMSAIDIA MWANAFUNZI ANAYEFANYA VIBAYA KATIKA MASOMO SHULENI NDIO HII

Siyo jambo la kufurahisha kwa mzazi unapoona mtoto hafanya vizuri masomoni.

Unapofahamu kuwa maendeleo ya mwanao siyo kama vile ulivyotarajia, ni rahisi kupatwa na simanzi, wasiwasi na hasira.

Ni dhahiri mzazi unatamani mtoto awe na mustakabali mzuri kimaisha. Matumaini hayo yanakufanya uchukulie kushindwa kwake masomo kama kiashiria cha kuharibika kwa maisha yake ya baadaye. Hakuna mzazi anayependa mtoto awe na maisha yasiyoeleweka.

Kwa sababu ya matarajio makubwa uliyonayo kwake, ikitokea vinginevyo, inakuwa sababu kubwa ya kuzorotesha uhusiano wenu. Kufeli kunaleta maana ya mtoto kujiharibia maisha yake kwa mikono yake mwenyewe.

Wakati mwingine mtoto hufanya vibaya hata baada ya kuwa umeshaongea naye mara kadhaa. Katika hali kama hii, huwezi kuwa na utulivu kuona mambo yanaharibika.

Kufeli ni fursa ya mafanikio zaidi

Katika kila tatizo kuna fursa. Kufanya vibaya darasani kunaweza kumuamsha mtoto usingizini akajifunza somo muhimu litakalobadilisha maisha yake.

Inawezekana mwanao alikuaminisha kuwa anafanya juhudi shuleni. Lakini kumbe anachokifanya shuleni ni tofauti na imani aliyokujengea. Kufanya vibaya hufunua ukweli unaokusaidia mzazi kuelewa hali halisi.

Pia, kufanya vibaya kunaweza kuwa fursa ya mtoto kujifunza mapema matokeo ya kutoweka juhudi masomoni.

Hatua madhubuti zinapochukuliwa mapema zinamnusuru mtoto na matokeo mabaya zaidi siku za usoni.

Ipo mifano mingi ya wasomi maarufu walioanza safari yao ya kielimu kwa kufanya vibaya darasani. Hawakukata tamaa wala kukubali kushindwa. Kufanya vibaya kuliwatengenezea njia ya kujikagua na kurekebisha makosa. Kufeli siyo mwisho wa mafanikio.

Mruhusu mwanao kufanya vibaya

Kufanya vibaya darasani humfanya mtoto ajisikie vibaya. Kujiona hajafikia malengo yake binafsi, matarajio ya wazazi na viwango vya shule humjengea wasiwasi na hatima ya maisha yake.

Hali hiyo, hata hivyo, inaweza kugeuka kuwa hamasa ya kukabiliana na changamoto kwa ufanisi zaidi.

Mtoto huyu anayejisikia vibaya kwa kushindwa kufaulu, hatapenda kujikuta katika mazingira hayo siku zijazo. Atahamasika kusoma kwa bidii ili aepuke kujisikia vibaya kwa mara nyingine.

Aidha, matokeo mabaya yanaweza kuwa sehemu ya safari ndefu ya kielimu kwa mwanao. Akishindwa kufikia malengo, siyo tiketi ya kukatisha safari bali fursa ya kujikagua na kujipanga upya.

Pamoja na ukweli kuwa ungejisikia fahari mwanao kufanya vizuri darasani, hali halisi inapokuwa kinyume, usione kuwa huo ndiyo mwisho wake. Mruhusu afanye vibaya kama fursa ya kujifunza.

Ajifunze kwa nini amefeli

Mtoto asipojifunza kwa nini hakufanya vizuri hawezi kubadilika. Lazima atambue wapi alipojikwaa ili apate somo kupitia kushindwa kwake.

Huenda ni kukosa mazingatio darasani, kushindwa kushirikiana na wenzake darasani na hata kushindwa kutumia muda wake vizuri. Msaidie kujitathmini.

Kwa kawaida, ni vigumu mtoto kujitathmini bila kuwabebesha wengine wajibu wake. Hufanya hivyo kama jitihada za kujinasua na makosa yake. Anaweza kutafuta kuwabebesha lawama watu wengine kama walimu, wanafunzi wenzake na hata wewe mzazi. Usiruhusu afanikiwe kujinasua.

Ingawa anaweza kutoa sababu zinazoshawishi kuhalalisha matokeo mabaya, kukubaliana na visingizio vyake ni kujenga mazoea yasiyofaa. Ni vyema ajenge uelewa kuwa hakuna mtu mwingine anayewajibika na mafanikio yake kielimu isipokuwa yeye.

Awajibikie matokeo yake mabaya

Kumpenda mtoto si kumdekeza na kumlinda hata pale anapokosea. Unapomdekeza unamjengea mazoea yasiyofaa ya kuwanyooshea vidole watu wengine kwa makosa yake mwenyewe. Hii kwa hakika si tabia ya kufumbia macho.

Kumpenda mtoto ni pamoja na kufanya ajisikie hatia na kujutia makosa yake. Anaposhindwa mtihani, aelewe kuwa kufaulu ni matokeo ya matendo yake mwenyewe. Kwa mantiki hiyo, aelewe kuwa hana mtu mwingine wa kuwajibika isipokuwa yeye mwenyewe.

Ikiwa matokeo yake mabaya yanaambatana na adhabu, hakuna sababu ya kumtetea.

Inawezekana kweli mtoto amefanya vibaya kwa sababu ya mfumo wa elimu, aina ya walimu wanaomfundisha, mazingira mabaya ya shule na hata tabia za wanafunzi wenzake.

Hata hivyo, ni muhimu kumfanya mtoto awajibike kwa sehemu yake. Kama shule inamtaka arudi mapema kabla ya wenzake kumaliza likizo, huko ndiko kuwajibika.

Kama matokeo yake yanamlazimisha kuhama shule, atajifunza vizuri zaidi ikiwa atahama. Kumtetea mtoto aliyepoteza sifa za kuendelea kusoma mahali alikoshindwa kuonyesha bidii, ni kumfundisha tabia ya kuhalalisha makosa. Hatojifunza.

Atengeneze mikakati kujirekebisha

Kuelewa makosa yake na kuyawajibikia hakuwezi kuwa na faida ikiwa mtoto hataweza kujua kipi anapaswa kufanya ili abadilike. Mbinu chanya za kutatua tatizo aliloligundua zinahitajika.

Hatua ya kwanza kumuwezesha kupata mbinu zinazomfaa, ni kumsaidia kutathmini ari na motisha yake kimasomo.

Mpe fursa ya kutafakari namna anavyojituma na pia anavyoelewa uhusiano wa juhudi zake na mafanikio yake kimasomo.

Tathmini nzuri itamsaidia kuweka mikakati madhubuti ya kujinusuru na makosa yaliyochangia kufanya vibaya. Kama anahitaji kutunza muda awapo shuleni, achukue hatua ya kupanga na kuheshimu ratiba.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: