MAHAKAMA Kuu imeamuru Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe asikamatwe wala kuwekwa kizuizini na Jeshi la Polisi hadi maombi na kesi yake ya Kikatiba aliyofungua jana yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Hata hivyo, Mahakama hiyo ilisema polisi inaweza kuendelea na mahojiano ama uchunguzi dhidi ya Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, mkoani Kilimanjaro.
Amri hiyo ilitolewa jana na mahakama hiyo iliyoketi chini ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na mwenyekiti Jaji Sekiet Kihiyo, akisaidiana na Lugano Mwandambo na Pellagia Khaday.
Katika Mahakama hiyo, upande wa mlalamikaji Mbowe uliongozwa na wakili Tundu Lissu akisaidiana na Peter Kibatala na John Mallya.
Mlalamikaji aliwasilisha maombi ya kuomba zuio la kukamatwa na kuwekwa kizuizini na kutaka Jeshi la Polisi kusubiri usikilizwaji wa kesi ya msingi.
Mbowe kupitia mawakili wake anaiomba mahakama hali ibaki kama ilivyo sasa, kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa maombi ya zuio la kumkamata.
Walalamikiwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (kwa sasa Paul Makonda), Kamanda wa Polisi (ZPC), Kanda Maalum ya Dar es Salaam (Simon Siro) na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO)
(Camillius Wambura).
Upande wa walalamikaji uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Gabriel Malata.
Aidha, mawakili wa mlalamikaji walipinga Wakili Malata kuingia mahakamani kuendesha kesi hiyo kwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG)siyo sehemu ya kesi.
Hata hivyo, Malata alidai anastahili kusimama mbele ya jopo hilo licha ya kwamba AG siyo sehemu ya kesi hiyo, kwa sababu serikali imeshtakiwa akiwamo Mkuu wa Mkoa, ZPC na ZCO.
Alisema viongozi hao hawajashtakiwa kama watu binafsi bali kupitia nafasi walizonazo serikalini.
"Watukufu majaji, tunaomba kubadilisha hati za maombi pamoja kesi ya kikatiba iliyopo mahakamani ili tuweze kumuongeza AG katika orodha ya walalamikiwa," alidai Lissu.
Jopo hilo lilisema maombi ya kuomba zuio la kukamatwa na kuwekwa kizuizini Mbowe yatasikilizwa leo.
Juzi mahakama hiyo ilitoa wito wa kuwaita mahakamani RC, ZPC na ZCO jana.
Mbowe alifungua kesi hiyo kufuatia hatua ya Mkuu wa Mkoa, Makonda kumtaja katika orodha yake ya watuhumiwa 65 wanaojihusisha na dawa za kulevya kwa namna tofautitofauti, na kumtaka afike katika Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalum Dar es Salaam, kwa ajili ya mahojiano.
Katika kesi hiyo namba 1 ya mwaka 2017, Mbowe pamoja na mambo mengine anapinga mamlaka ya RC kukamata na kile anachokiita kudhalilisha watu.
Hivyo anaiomba mahakama hiyo, pamoja na mambo mengine, itamke kuwa vifungu vya Sheria ya Tawala za Mikoa vinavyowapa mamlaka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuwakamata watu na kuwatia mbaroni viko kinyume cha Katiba.
Katika maombi ya msingi, yaliyosajiliwa kwa namba 21/2017, Mbowe anaiomba mahakama iwazuie wadaiwa kutekeleza azma yao ya kumtia mbaroni, pamoja na mambo mengine, akidai kuwa kuna kesi ya kikatiba ambayo tayari ameifungua mahakamani hapo.
Pia, anaiomba mahakama itoe amri ya kuwazuia kumkamata hadi hapo kesi hiyo ya kikatiba itakapomalizika na kwamba Mahakama Kuu imwachie na polisi wasiendelee na mchakato wowote dhidi yake hadi hapo kesi hiyo itakapomalizika.
Katika kesi ya Msingi ya Kikatiba Mbowe anapinga kitendo cha Polisi kumtaka afike kituoni kwa madai kuwa ni utekelezaji wa amri ya Mkuu wa Mkoa.
Anadai kuwa sheria inayompa Mkuu wa Mkoa mamlaka ya kutoa amri ya kumkamata na kumweka ndani mtu ipo kinyume cha katiba kwa madai kuwa ilitungwa katika mazingira ambayo hapakuwa na vituo vya polisi vya kutosha.
Hivyo anadai kuwa kwa mazingira ya sasa sheria hiyo imeshapitwa na wakati na anaiomba mahakama itamke kuwa ni kinyume cha katiba.
Mbowe anadai hata kama Mkuu wa Mkoa alikuwa anatekeleza mamlaka yake kwa mujibu wa sheria hiyo, hakutimiza matakwa ya kisheria, ambayo ni pamoja na kutoa taarifa kwa Hakimu wa Mahakama ya Wilaya au ya Hakimu Mkazi.
Hivyo anaiomba mahakama kama itaona kuwa Mkuu wa Mkoa alikuwa sawa kutoa amri hiyo basi imwamuru afuate matakwa ya kisheria, ikiwa ni pamoja na kulinda haki za binadamu katika kutekeleza madaraka yake hayo.
MOKONONI POLISI
Mbowe aliaangukia mikononi wa Jeshi la Polisi juzi baada ya kupiga danadana kwa siku kadhaa tangu atajwe katika orodha ya watuhumiwa 65, ya awamu ya pili ya vita dhidi ya dawa za kulevya, ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, wiki tatu zilizopita.
Febrauri 8 Makonda alimtangaza Mbowe kuwa mmoja wa watu wanaotakiwa kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa mahojiano baada ya saa 48.
Lakini Mbowe, ambaye ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, aliitisha mkutano na waandishi wa habari siku mbili baadaye akisema hatoripoti kwa kuwa Makonda si mamlaka ya ukamataji na kwamba angefungua kesi ya kikatiba dhidi yake.
Kufuatia mvutano huo, Ijumaa Kamanda wa Kanda Maalum alimpa Mbowe saa 48 awe ameripoti Kituo Kikuu.
Mbowe alikamatwa na Jeshi hilo juzi majira ya saa 9:00 alasiri jijini Dar es Salaam na kushikiliwa kwa saa 10 hadi usiku wa manane, katika Kituo Kikuu. Lakini sasa Polisi haiwezi kumkamata tena Mbowe kwa kuwa shauri hilo lipo mbele ya mahakama.NIPASHE
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / kitaifa /
slider
/ FREEMAN MBOWE NAMNA ANAVYOWAKASIRISHA BURE JESHI LA POLISI KUPITIA MAHAKAMA
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment